Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAONI YA MHARIRI: Mvutano wa Makonda, TRA haukustahili

14261 MAKONDA TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilichapisha kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, tangazo ikiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.

Tangazo hilo la TRA, chombo pekee chenye mamlaka ya kukusanya ushuru wa forodha nchini, liliwataka wamiliki wa mali hizo kuhakikisha wanazitoa katika muda wa siku 30, vinginevyo kwa mamlaka waliyonayo kisheria, itapigwa mnada ili Serikali ipate kodi yake kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

TRA katika tangazo hilo iliorodhesha makontena zaidi ya 800 yaliyotakiwa kuondolewa huku jina la Paul Makonda likijitokeza mara 20 kama mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na samani kama meza, viti na mbao za kuandikia kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Uthibitisho wa Paul Makonda mpokeaji wa makontena 20 kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam uko katika maeneo matatu.

Kwanza, Februari 16 Makonda alikaririwa katika mtandao wa gazeti la Serikali la Habari Leo akisema alipokea makontena 20 yenye samani kwa ajili ya ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa. Pili, aliwachukua baadhi ya walimu akaenda nao yaliko makontena hayo bandarini ili kuwaonyesha. Zaidi ametishia kumlaani mtu atakayeyanunua.

Makonda alisema makontena hayo yalikuwa sehemu ya shehena ya makontena 36 yenye samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni akidai kuwa ni msaada kutoka kwa Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

Mkuu wa mkoa amefikia kutoa onyo kali kwa yeyote atakayenunua makontena hayo ambayo TRA ilitaka kuyanadi Jumamosi ingawa yalikosa mnunuzi. Makonda amesema atakayenunua makontena hayo atalaaniwa yeye pamoja na uzao wake wote.

Pengine kutokana na sakata hilo, jana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliagiza makontena hayo 20 yapigwe mnada na kwamba hajali vitisho vya mkuu huyo wa mkoa na akaapa kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.

Alitoa maelekezo hayo jana alasiri baada ya kufanya ziara ya kukagua makontena hayo katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD).

Jambo hili kwa ujumla limetusikitisha na tunadhani halijakaa sawa kwa sababu kwa namna fulani linaweza kuwagawa Watanzania bila sababu za msingi.

Makonda anataka makontena yasitozwe kodi katika kile anachodai aweze kuboresha mazingira ya kufanyia kazi walimu ikiwa ni kumuunga mkono Rais aliyeamua kutoa elimu bure kwa Watanzania na hasa watoto wa masikini, lakini pia Waziri wa Fedha naye anasema atahakikisha anasimamia sheria na huenda naye anataka kuunga mkono jitihada za Serikali za kusimamia mapato yake.

Mgogoro huu wa Makonda kwa upande mmoja na TRA na Wizara ya Fedha kwa upande mwingine haukustahili kuwepo kwa sababu wote wanafanya kazi katika Serikali moja na wakiwa na malengo yanayofanana kuhakikisha kuwa maisha ya Watanzania katika sekta zote yanakuwa bora.

Tunasikitika na hali inayotokea kwa sababu kama viongozi wa Serikali ambao tunaamini wanajua sheria na nini cha kufanya wanaweza kuvurugana kiasi hicho, je Mtanzania wa kawaida ambaye hana nafasi katika mamlaka za juu atahisi vipi?

Kama tafsiri ya kodi na misamaha yake inaweza kuwavuruga viongozi wa Serikali itakuwaje kwa wananchi wa kawaida.

Columnist: mwananchi.co.tz