Nilistuka kusoma habari gazetini, kuwa kumbe sababu ya wahitimu wa kidato cha sita katika shule ya wasichana Jangwani, ni wanafunzi shuleni hapo kujihusisha na vitendo vya uasherati.
Pamoja na mambo mengine, hiyo ndiyo sababu iliyotamkwa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Suleiman Jaffo, wiki iliyopita.
Ni sababu nzito inayohitaji mkakati kabambe wa kuwanusuru wanafunzi sio tu wa shule hiyo lakini shule zote kwa jumla.
Hata hivyo, najiuliza shule inapokuwa na wanafunzi walioshindikana kwenye utovu wa nidhamu, walimu wao wanafanya nini? Lakini zaidi wako wapi wazazi wa watoto hawa?
Sitaki kuwazungumzia walimu, uchambuzi huu unamtazama zaidi mzazi au mlezi, nikisukumwa na maswali je, wazazi ama walezi wanawajibika ipasavyo katika kufuatilia maendeleo ya taaluma shuleni? Aidha, ni kwa kiwango gani wazazi wanakuwa chachu ya ufaulu kwa watoto wao?
Haya ni maswali yasiyo na majibu kutoka kwa wazazi wengi. Uzoefu wangu unaonyesha wazazi wengi nchini hatuna habari na kinachoendelea shuleni kuhusu watoto wetu. Ndio maana ni jambo la kawaida mzazi kushindwa kukanyaga shuleni ndani ya miaka saba au minne ambayo mtoto wake ameitumia shuleni. Wapo wanaojipa udhuru usiokwisha kiasi cha kushindwa hata kuhudhuria vikao shuleni.
Huwezi kwenda shule lakini unashindwaje kuwa na mawasiliano na mwalimu hata mmoja unayeweza kumtumia kujua maendeleo ya mtoto wako? Kama mawasiliano na walimu yanakushinda huna ndugu, jamaa au rafiki wa karibu unayeweza kumtumia kujua mwenendo wa mtoto wako shuleni?
Zipo taarifa za wanafunzi wanaosimamishwa masomo kwa miezi kadhaa; wazazi hawajui kwa sababu watoto wao wamewaficha. Lakini kwa mzazi makini hawezi kukaa zaidi ya miezi mitatu pasipo kujua kinachoendelea shuleni kuhusu mtoto wake.
Tukubali kuwa Watanzania wengi ni mabingwa wa kuzaa; malezi yanatupiga chenga na kibaya zaidi hatupo tayari kujifunza kutoka kwa wengine kuhusu malezi.
Wazazi wengi wanajua malezi ni kulipa ada, nauli, kununua sare na kugharimia vifaa vya shule. Wakishatimiza hayo, mengine wanawaachia watoto wenyewe; matokeo yake ndiyo yale ya mtoto anaaga kwenda shule kila siku lakini shule haonekani.
Mwanafunzi huyu anapofikia hatua ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu, mzazi hajui kwa sababu tangu mwanzo hakuwajibika.
Malezi ni zaidi ya chakula na mavazi. Ni kwa namna gani wazazi tunakuwa chachu ya mafanikio ya watoto wetu katika maisha yao ya sasa na baadaye?
Baba au mama mzuri hapimwi kwa kumlipia ada mwanawe au kumpeleka hospitali anapoumwa. Unamfinyanga vipi mtoto wako na kumuandaa kuwa mtu kamili kwa siku zijazo?
Wazazi tuache kuzaa na kuiachia dunia kutulelea watoto. Ni kosa kuishi kwa mazoea kuwa watoto watakua bila ya kuwapo kwa mchango wowote wa wazazi.
Kimsingi, mtoto anapaswa kujifunza kutoka kwa wazazi, ndio maana watoto waliofanikiwa baadhi hunasibisha mafanikio yao na msingi mzuri walioupata kutoka kwa wazazi wao.
Uko wapi mzazi mpaka mtoto wako anakuwa kinara wa utovu wa nidhamu shuleni?
Wazazi tubadilike kama kweli tuna dhamira ya kufanikisha ndoto za kimaisha za watoto wetu. Hamasa ya kwanza ya kufanya vizuri kwa mwanafunzi inapaswa kuanza nyumbani kwa mzazi au mlezi. Tuwajibike, tusisubiri matokeo mabaya kisha tuanze kuwanyooshea kidole walimu.