Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAONI: Vituo vya televisheni vitoe haki kwa wasiosikia

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maonyesho ya Nane Nane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu yaliibua tatizo linaloendelea katika maeneo mengi nchini kwa watu wasiosikia.

Kwenye habari za televisheni alionekana mtu asiyesikia aliyekuwa na shauku ya kujifunza kupitia kwa ofisa aliyekuwa anaeleza mbinu za kilimo cha kisasa na utunzaji bora wa shamba.

Mtaalamu alikiri kushindwa kumsaidia mwananchi huyo ili afahamu anachoeleza kwa kuwa haijui lugha ya alama.Hilo lilipita na Serikali iliagiza maonyesho ya kitaifa yafanyike katika viwanja hivyo kwa miaka mitatu mfululizo.

Mwananchi huyo bado atakaa kando ya televisheni na kuangalia picha nzuri za mashamba ya kilimo bila kuelewa maelezo yake kwa kutengwa na lugha inayotumika.

Huyu ni sehemu ya wakulima waliolengwa kunufaika na fursa zote zinazopatikana kwenye maonyesho yaliyoandaliwa kwa ajili yao, ikiwa ni pamoja na kuelimishwa na kupata haki ya kuuliza maswali.

Kundi hili limetengwa hata kwenye taarifa za habari za televisheni ambazo zimepuuza kuweka wataalamu wa lugha ya alama ili nao wapate haki ya kupata habari.

Maelekezo yote ya viongozi kupitia taarifa za habari kwenye televisheni hutolewa kwa ujumla wake bila kujali kuwa kuna kundi halifikiwi na ujumbe uliokusudiwa.

Nchi haiwezi kuwa na uhaba wa wataalamu wa lugha ya alama kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya kundi hili kwa muda wa saa moja tu wakati wa taarifa ya habari.

Hili ni kundi ambalo tayari linapambana na changamoto tofauti ikiwa ni pamoja na kushindwa kupata huduma kwenye taasisi mbalimbali kwa kuwa hakuna wataalamu wa lugha yao na hivyo kuzikosa baadhi ya haki zao.

Mwananchi asiyesikia anaweza kukosa haki ya huduma ya matibabu kutoka kwenye hospitali ya umma inayoendeshwa kwa sehemu ya kodi yake, kwa sababu daktari haifahamu lugha ya mgonjwa.

Pamoja na changamoto hiyo bado wanaikosa fursa ya kuelimishwa kupitia vipindi na taarifa za habari kwenye televisheni ambazo urushwaji wake hauzingatii mahitaji yao.

Mbali na kunyimwa haki ya kupata habari kwa kutoweka wataalamu wa lugha ya alama, kundi hilo tayari linaikosa fursa ya kuelimika kupitia mafunzo ya ujasiriamali ili wajikwamue na kujiongezea kipato.

Watu wasiosikia wananyimwa haki ya kushiriki kwenye uamuzi wa mambo yanayowahusu kupitia kwenye vikao na badala yake tunaamua kwa niaba yao.

Kama mahitaji yao yangekuwa yanazingatiwa kwenye maonyesho hayo lingekuwepo banda la huduma ya lugha ya alama.Hii ndiyo sababu hata habari ya televisheni haikumpa mkulima huyo sauti.

Inawezekana asiyesikia asijue kuandika, lakini anapofundishwa kwa vitendo anajengewa uwezo wa kufanya kazi kama walivyo wananchi wengine wasio na ulemavu.

Mathalani Mkoa wa Kagera una walemavu wasiosikia 100 waliotambuliwa kupitia chama cha watu wenye ulemavu(Chawata).

Idadi hiyo inafikia 400 kwa kuwa wenye umri chini ya miaka 18 hawakusajiliwa.

Hili ni kundi kubwa la Watanzania wanaokosa fursa hata za kujua maagizo ya viongozi wao.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine inaweza kuondoa vikwazo vilivyo ndani ya uwezo wake na katika hatua hii tunaweza kuanza na wataalamu wa lugha ya alama wakati wa taarifa ya habari.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoani Kagera. 0767489094

Columnist: mwananchi.co.tz