Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKENGEZA: Matuzo ya tozo

35061 Pic+tozo Matrafiki

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hata katika nchi ya mabeberu, kuna vitu vingine ambavyo labda inafaa kuigwa. Tumeona rubani akituzwa kwa ujasiri wa ‘toroka uje’. Kwa nini tusipanue mtindo huu mwaka mpya uwe wa kuwatuza Wabongo mbalimbali ambao wamefanya jambo la kipekee, au la kishujaa, au la kikarimu zaidi.

Wako wengi ambao wamewasha mwenge wao wa kibongo duniani, wamepata tuzo za kimataifa au kutambuliwa kimataifa. Na wako wengi zaidi ambao wameonesha uzalendo wa hali ya juu katika jamii zao, kwa kufundisha vizuri, au kuokoa maisha ya wanawake wajawazito, au kujitolea kufanya jambo la kimaendeleo. Wako wachezaji (si wa mpira tu lakini nao wamo), wakimbiaji na wasanii wakubwa kwa wadogo ambao wameonesha umahiri wa hali ya juu na kuongeza kipato cha taifa pia.

Wako wakulima, na wafanyakazi ambao wametoa mchango mkubwa katika kuendeleza uchumi. Kwa nini pasiwe na matuzo mbalimbali ya heshima kwa ajili yao. Ila, kwa angalizo kubwa, wanasiasa wa kitaifa wasipewe maana watabaki wanajituza tu.

Usishangae, hata Makengeza anaweza kuwa siriasi mara mojamoja. Wako wengi ambao wanaMATAG sana, yafaa tuwape moyo kwa kuwapa mkono wa heri. Upande wa pili wa kutumbua ni kutambua.

Lakini, kwa kuanzia, ngoja nitoe matuzo yangu ya kimakengezamakengeza kwa mwaka huu nikitegemea kwamba siku ya Nyerere au mwaka mpya tutaanzisha mtindo wa tuzo.

Matuzo ya tozo

Hapa ningependa kutoa matuzo ya tozo kwa madereva walio wengi katika nchi hii kwa kuonesha uzalendo uso kifani maana wameendelea kuendesha magari yao, licha ya kusimamishwa na kubambikiwa faini kila siku. Yawezekana walikuwa na kosa, yawezekana walitafutiwa makosa lakini wameweza kuendelea kuchangia pato la taifa kwa shilingi elfu thelathini zao bila kuchoka.

Ndiyo maana wameweza pia kusaidia jeshi letu pendwa linalosimamia sheria na mashine ya risiti mkononi kutangaza kwamba wamefanya kazi vizuri zaidi maana wameweza kuongeza kipato cha taifa katika mwaka. Mnisamehe maana labda walitangaza pia kupungua kwa ajali lakini sikusisikia tangazo hilo.

Ninachojua ni kwamba madereva wamekuwa wakarimu sana na tayari kulipa faini bila shuruti wala sheria ukiacha wale wachochezi na vitoto vya mabeberu ambavyo wanaendelea kulalamika na hata kupiga picha mtu ambaye alitaka pesa za kubrashi viatu tu.

Lakini katika hayo, inabidi kutoa tuzo la matozo maalumu kwa madereva na makonda wa daladala. Sijui wanafanyaje ili waweze kusimamishwa kila siku kwa kuwa na kosa hili au lile.

Iwapo hawatengenezi magari yao ili waweze kutoa kodi ya ziada kila mwaka, heko yao. Bila wao, sijui uchumi wetu ungekuwa wapi. Aidha ningependa baadhi ya hawa wataalamu wa risiti kupandishwa cheo na kuhamishwa katika kitengo cha upelelezi maana kila siku ninawavulia kofia kwa kutambua hitilafu ambayo watu wengine wala hawaioni. Wakihamishwa kitendo cha upelelezi, ninao uhakika kwamba wahalifu wote watakamatwa mara moja.

Tuzo ya Pondapanda au Fungafungua

Hapa, kuna shirika moja tu ambalo linastahili tuzo hii. Mwaka mzima wamejitahidi sana kuponda kazi za wengine ili kazi zipande mioyoni mwa watu. Mara nyingine najiuliza iwapo hawa wanaopondwa wanatoa kitu kidogo ili wapondwe maana baada ya kupondwa nyimbo zao zinapanda kwenye chati mara moja.

Juzi nilisikia watoto wadogo wakiimba ile ya … ziiiii na kurukaruka kwa furaha. Wangeusikia wapi ingekuwa haujapondwa sawasawa. Wadumu katika kazi hii na mwaka huu nawaomba sana waponde vitabu vyangu vipya navyo vipate nafasi ya kupanda.

Tuzo ya Kinyonga

Hili tuzo ni muhimu sana katika kuwafariji watu ambao, kwa kuwa wanainama kulamba miguu, hawaoni mwelekeo wa watembeaji haraka ya kutosha. Ndiyo maana wakiona wenyewe wanalenga kushoto, wanashabikia mara moja, pamoja na kuwatukana watu wote walioona kwamba kulia ilikuwa bora. Kumbe kiongozi wa msafara alikuwa anaenda kulia hivyo wanalazimika kugeuka kulia bila kuonyesha haya na kushabikia kulia pamoja na kuwatukana watu wote ambao walisema twende kulia kabla.

Hawa vinyonga ni wataalamu pia wa kutunyonga na nyongo zao lakini wanashindwa kutambua yupi ni yupi. Ni wafadhili au mafedhuli? Wachochezi au wachachuzi? Wenye hujuma au huduma? Mpaka naona wengine wanachanganyikiwa kabisa hadi kutembea barabarani wakiimba:

Ni wafadhali … hapana … ni mafedhuli … umekosea … wafa … mafe … aaaagh!

Tuwafariji na tuzo jamani.

Tuzo ya Amri wa Kustaajabisha

Hili ni tuzo pekee ambayo inaweza kutolewa kwa wanasiasa hasa wale wa mikoani. Kwa hii tuzo nawaachia watu wapendekeze maana amri zimekuwa nyingi. Tuzo itaenda Dar es Salaam? Au Iringa? Au Manyara? Au Arumeru? Au Songwe? Au wapi? Au tuwe na kipindi maalumu cha Amri Star Search. Yatafurahisha jamani, yatafurahisha.

Lakini mbele ya safari, tusiwasahau wale wote ambao wamefanya maajabu ya kweli katika kujenga taifa letu.

Nawatakieni heri na mafanikio ya mwaka 2019 ili kila mmoja afikiriwe kwa tuzo ya heshima mwisho wa mwaka.



Columnist: mwananchi.co.tz