Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKENGEZA: Dini duni kama siasa duni

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwishiwa Makengeza,

Nimejaribu kuchuma kati ya vyuma hadi nikapigwa navyo pasi. Nimepambana na hali yangu hadi hali ikanikimbia, nimejiajiri pasipo na ujira, yaani nimefanya juu chini hadi kubaki chini nikisubiri kukanyagwakanyagwa. Nikataka kukata tamaa nakwambia. Ndipo malaika aliponijia na kuniambia:

‘Amka wewe mdhaifu wa wadhaifu. Ya nini kusota muda wote huu? Mungu amekuchagua, amekuteua ulete mwanga pale gizani na kuwapa matumaini waliojiona hawawezi kujikwamua kabisa.’

Nilitetemeka.

‘Una maana gani mheshimiwa malaika?’ ‘Mungu amekutuma uanzishe kanisa jipya, kanisa ambalo litawashirikisha wote hawa wadhaifu wanaofikiri kwamba wanaweza kuwashawishi watu kwa maneno yao ya kibinadamu tu.’

Nikiwa bado nimesujudu nikazidi kuuliza.

‘Nani hawa, ewe mheshimiwa malaika.’ ‘Huwajui? Ni hawa ambao wanaongea na kuongeaga na kuongeagagagaga kila siku. Ni hawa ambao wanaona wanajua kila kitu na wana haki ya kuingilia kila kitu. Ni hawa ambao wanajidai wataalamu bila hata kusomea utaalamu huu.’

Nilipoelewa nikaruka juu na kusahau hata kuabudu tena.

‘Una maana ya wanasiasa?’

‘Sawasawa. Baada ya kuona kwamba watu wamekosa imani nao, Mungu amewahurumia. Hivyo amenituma kwako uamke na kuanzisha kanisa ya Mtakatifu Siasa.’ Ikabidi nicheke.

‘Mtakatifu wakati wao ni watakavitu.’

‘Kwani kuna tofauti gani kati yao na hawa manabii, na mitume na nani sijui wa siku hizi? Kitu muhimu ni kuuza lugha. Manabii hadi wanawakanyaga watu ili wasiguse chini maana wao wako juu na waumini wao si kitu … ili mradi watoe sadaka.Na mwanasiasa yukoje? Anajiona juu ya kila kitu, anaweza kusema neno lolote, na kutoa vitisho vyovyote kwa kuwa ni muumini wa siasa.’

‘Ni kweli.’ ‘Manabii wanatoa ahadi za ajabuajabu ili watu wawafuate. Ukiwafuata utapata utajiri, au gari la fahari, au watoto mapacha. Utaponyeshwa magonjwa. Chochote kile unachokitaka utakipata ili mradi uwafuate. Wanasiasa si wako vilevile?’

‘Ni kweli mheshimiwa malaika. Yaani wanavyotoa ahadi kwamba wanatufikisha katika nchi ya maziwa na asali. Ndiyo maana sisi tunapenda kutania kwamba sisi kweli ni nchi ya ahadi hata kama ahadi ni duni.

Halafu, kama manabii, wanatulazimisha kutoa hata kile kidogo tulichonacho ili wazidi kuneemeka katika mahekalu yao. Kweli hakuna tofauti kabisa.’

Malaika akatingisha mabavu yake kama ishara ya kufurahia usemi wangu, ndipo nikaanza kuamini kwamba kweli nitaweza kuanzisha kanisa hili. Kisha malaika akaendelea.

Amri nyingine za kipumbavu kabisa ili mradi amri. Amri nyingine nzuri, yenye lengo zuri kwa binadamu lakini kwa kuwa inatolewa kwa amri tu, bila mpango wala mpangilio, bila uchambuzi wa kina, amri za mkurupuko, badala ya kuleta mafanikio yaliyotegemewa na wale niliowaumba, yanaharibu hata yale mazuri yaliyokuwepo. Hatuwezi kukubali hali ya namna hiyo.

Mwisho hivi vikundi vyote viwili vina umimi sana. Viko tayari kukanyaga popote ili mradi wapate wanachokitaka.’

Hapo ikabidi niulize swali.

‘Sasa mheshimiwa malaika, hili kanisa la Mtakatifu Siasa itawasaidia nini?’

‘Kwani makanisa mengine yanawasaidia nini manabii wote hawa? Wananeemeka na kunenepa juu ya migongo ya waumini wao. Kwa kuanzisha kanisa lako, ambamo kila mwanasiasa atakuwa anaitwa nabii badala ya mheshimiwa, utaweza kupanua sana wigo wa manabii.’

‘Lakini mbona wote hawa ni feki?’

‘Hujui msemo wangu kwamba watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Inabidi waangamie zaidi na zaidi hadi waamke na kutambua kwamba hawa wote ni feki, ndipo wataamka na kuanza kujenga ufalme wangu duniani. Hawawezi kufanya hivyo hadi watambue nani anawadanganya na kwa vipi.’

‘Unisamehe mheshimiwa malaika, bado sijakuelewa. Mbona watu wameshaanza kutambua unafiki na uongo wa wanasiasa wengi?’

‘Wametambua kweli? Kila siku kashfa, kila siku mengine yanafichuliwa lakini uchaguzi unapofika wanakimbilia kuwachagua walewale waliofichuliwa. Wanavumilia ujinga na upumbavu wa kila aina. Kwa hiyo somo halijawaingia hadi sasa. Ndiyo maana ni muhimu kuwaunganisha na hawa wataalam wengine wa kutambia uongo chini ya kivuli cha dini, tuwe na dini pana ya waongo hadi watu wangu waamke. Ndivyo anavyosema Mwenyezi.’

‘Watanikubali kweli kama kiongozi wa kanisa hili. Mimi si mwanasiasa.’

‘Ni kweli wewe si mwanasiasa lakini waganga ambao wanafuatwa kabla ya uchaguzi si wanasiasa pia. Kaa na mimi, sikiliza vizuri maneno yangu kisha utaamka na kutoa waraka wa nabii mwishiwa kwa wanasiasa. Unajua wana kiherehere kwa sasa, na kiherehere ni msingi wa kudanganywa.

Ukiwaonesha katika waraka wako kwamba watavuna kura lukuki katika uchaguzi ujao watakufuata moja kwa moja. Watakuletea fungu la kumi na hata ishirini kama kondoo. Na kupitia kwao utavuna pia pesa za wafuasi wao ambao wanashabikia bila hata kuelewa.’

‘Lakini mheshimiwa malaika, mbona huu ni udanganyifu?’

‘Udanganyifu mtakatifu. Baada ya kukazua vyuma na kurudisha hali, nategemea utatumia fedha hizi kutengeneza muvi, hadithi, mashairi, nyimbo vyenye lengo la kuwafanya watu waamke.’

‘Hapa si ndio mwisho wa kanisa langu.’

‘Pamoja na makanisa yote mengine maana watu watakuwa wameyafichua na hawatakuwa na haja ya huo uongo tena. Wataamka na kuamua na kufanya kweli wao wenyewe.’

Umesikia hayo mwishiwa mwenzangu? Huoni kwamba nimeukata? Sasa unaonaje nikukatie na wewe unisaidie kutangaza kanisa langu jipya la Mtakatifu Siasa.

Wako Nabii Chizi Chipukizi

Dah! Sijui kama huu ni mpango wa Mungu, au ni mwendelezo wa ushetani. Hebu nisaidieni.

[email protected]

@MabalaMakengeza



Columnist: mwananchi.co.tz