Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA ZA MALOTO: Alaa Salah amemuenzi Josina Machel kwa mapinduzi Sudan

54963 Pic+josia

Wed, 1 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna mapinduzi bila wanawake. Maneno hayo aliyatamka binti mdogo mwenye umri wa miaka 22, Alaa Salah.

Huyu alikuwa kionjo kilichokoleza mapinduzi ya hivi karibuni yaliyomng’oa aliyekuwa Rais wa miongo mitatu Sudan, Omar al-Bashir.

Alaa ni mwanafunzi wa uhandisi, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Sudan. Picha zake za video akiwa amesimama juu ya gari, akiwaimbisha waandamanaji wenzake, nyingine akiongoza msafara, zimesambaa na kumfanya binti anayefuatiliwa sana.

Dunia inamuona Alaa shujaa. Wasudan wanamwita Malkia wa Nubi. Hata hivyo, anasema amekuwa akipokea vitisho vya uhai.

Hilo linamwogopesha lakini anasema alilelewa kuipenda nchi yake na ushiriki wake katika maandamano ya kumshinikiza Al-Bashiri kung’oka ni kwa sababu ya mapenzi aliyonayo kwa taifa lake.

Alichokifanya Alaa kinaweza kuibua swali. Je, nani anasema wanawake ni goigoi? Pengine wenye kuwaza hivyo, hawajui jinsi Bibi Titi Mohamed alivyosimama mstari wa mbele kuongoza harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika, wakati wanaume wengi waliufyata.

Josina Machel

Huyu anatukumbusha Josina Machel. Mke wa kwanza wa Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel. Harakati za kuongoza madai ya uhuru wa Msumbiji kutoka kwa Wareno, Josina alizianza akiwa na umri wa miaka 13.

Josina akiwa na umri wa miaka 18, alifanya jaribio la kwanza la kutoroka Msumbiji ili kujiunga na chama cha ukombozi wa nchi hiyo, Frelimo, kikiwa Tanzania. Miongoni mwa watu waliotoroka na Josina ni Rais aliyepita wa nchi hiyo, Armando Guebuza.

Baada ya kutembea umbali wa maili 800 (kilometa 1,287), Josina na wenzake walikamatwa na wakoloni wa Uingereza katika eneo la maporomoko ya Victoria, Rhodesia ya Kusini, sasa Zimbabwe, walikamatwa na kurejeshwa Msumbiji.

Josina alikaa jela miezi sita bila kufikishwa mahakamani, kutokana na hali hiyo, maandamano yalifanyika Msumbiji ambayo yalihamasishwa na Frelimo, na kusababisha aachiwe huru muda mfupi kabla hajatimiza umri wa miaka 19.

Baada ya kumwachia, wakoloni walimweka katika uangalizi lakini badaye kwa kumuona ni mwanamke, vilevile umri wake walimdharau. Dharau za Wareno ziliwaponza, kwani Josina alipata mwanya na kutoroka tena akiwa na wanafunzi wenzake.

Baada kuvuka Msumbiji, walitembea na kuvumilia dhiki kwenye kambi za wakimbizi nchini Swaziland na Zambia. Walifanya hivyo ili kukwepa ushushushu wa askari wa Wareno ambao walikuwa wakiwafuatilia.

Josina akiwa na umri wa miaka 20, aliteuliwa kuwa msaidizi wa mkurugenzi wa Taasisi ya Msumbiji jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi mwenyewe alikuwa Janet Mondlane, mwanamke wa Kimarekani, aliyekuwa mke wa Mondalne.

Janet na Josina wakawa marafiki, kisha wakaanzisha taasisi ya Wanawake wasio na Fursa, Women’s Detachment. Josina na wanawake wenzake walisimama kama wapambanaji msituni. Alitoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wa Msumbiji.

Ni Cabo Delgado alipokuwa anatoa mafunzo ya kijeshi kwa wapiganaji wa ukombozi, ndipo alikutana na Samora aliyekuwa mkurugenzi wa mafunzo. Na kuanzia hapo penzi la Samora na Josina lilichanua.

Mwaka 1969, alifunga ndoa na Samora, kusini mwa Tanzania, Novemba mwaka huyo alijifungua mtoto wao wa kiume, Samito.

Josina alifariki dunia jijini Dar es Salaam, Aprili 7, 1971, akiwa na umri wa miaka 25. Inaelezwa kuwa sababu ya kifo ni ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid).

Samora aliandika shairi kumlilia Josina: “Yaani zaidi ya mke, ulikuwa dada kwangu, rafiki na kamanda katika jeshi...”

Baadaye Samora alimpata Graca na kumuoa. Mwaka 1998, Graca naye aliolewa na Nelson Mandela, ikiwa ni miaka 12 tangu Samora alipofariki dunia mwaka 1986.

Hakika wanawake majasiri hawakuanza leo, alichokifanya Alaa Salah kwa Sudan bila shaka amemeenzi vizuri Josina Michael.



Columnist: mwananchi.co.tz