Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA ZA MALOTO: Agenda ya Sugu ibebwe na wapinzani wote

97999 Sugu+pic

Thu, 5 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema hata pasipokuwapo na Tume huru ya uchaguzi, atagombea na kushinda ubunge jimboni kwake kwa sababu wamejipanga kulinda kura.

Kipindi hiki wapinzani wakipigia kelele tume huru ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2020, kauli ya Sugu ya kushinda hata isipopatikana tume huru, ina nguvu kubwa. Nitaeleza!

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, aliyekuwa mgombea Urais wa Chadema na muungano wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, aliwaambia wapiga kura: “Mjitokeze mkapige kura kwa wingi, kuhusu tume itamtangaza nani mshindi, hilo niachieni mimi.” Je, nini kilitokea? Watanzania wengi walijitokeza kupiga kura. Katika watu 23 milioni walioandikishwa, zaidi ya 15.6 milioni sawa na asilimia 67, walipiga kura. Rais John Magufuli alipata kura 8.9 milioni, asilimia 58, Lowasa 6.1 milioni, asilimia 40. Ukirejea nyuma, Uchaguzi Mkuu wa 2010, idadi ya waliojiandikisha ilikuwa 20 milioni. Waliopiga kura walikuwa 8.6 milioni, sawa na asilimia 42.8. Jakaya Kikwete wa CCM kura 5.3 milioni, asilimia 62.8 na Dk Willibrod Slaa Chadema, kura 2.3 milioni, asilimia 27. Hiyo ni kwa kutojumuisha matokeo ya wagombea wengine. Nimeweka matokeo ya urais katika uchaguzi wa 2010 na 2015 ili kujisogeza kwenye hoja mahsusi. Ni miaka ambayo uchaguzi wake ulibeba nguvu kubwa ya upinzani kuliko uchaguzi wa 2005 na 2000. Mazingira ya 2015, unaweza kuyafananisha na yale ya 1995.

Tubaki kwanza kwenye uchaguzi wa 2010 na 2015. Kwa nini pamoja na uchaguzi wa miaka hiyo yote kubeba nguvu kubwa ya upinzani na mchuano mkubwa, lakini 2010 idadi ya wapiga kura ilikuwa ndogo kulinganisha na 2015? Jawabu lipo kwa Lowassa. “Pigeni kura, tume itamtangaza nani, hilo niachieni mimi.” Lowassa hakuwa imara kwenye kampeni. Hakumudu kuhutubia kwa muda mrefu. Hakutoa hamasa yenye nguvu alipokuwa jukwaani.

Lakini aliwajengea watu imani kwamba ana uwezo wa kutangazwa mshindi kama angepata kura za kutosha. Hii ndiyo hamasa iliyokosekana kwa Dk Slaa 2010. Dk Slaa alikuwa na hamasa na aliweza kuhutubia kwa muda mrefu na hotuba zake zilijenga hisia kwa wafuasi wake ambao walitembea wakijiamini. Hakuwaangusha waliojitokeza kwenye mikutano yake. Pamoja na hivyo, idadi ya waliopiga kura ilikuwa ndogo. Ila sababu kura kutokuwa nyingi ni kukosekana kwa imani kwa sababu hakuwa na matamshi ya uhakika kama ya Lowassa. Uchaguzi wa 1995 idadi ya waliopiga kura ilikuwa asilimia 77 ya waliojiandikisha. Sababu ni ilikuwa mgombea wa NCCR-Mageuzi wakati huo, Augustino Mrema alijenga imani kwamba angeweza kushinda na kukabidhiwa dola. Hotuba zake zilikuwa za kujiamini.

Ushawishi ni sanaa. Ujenzi wa imani ni kielelezo muhimu cha ushawishi, maana watu huvutiwa na wale wenye kujiamini. Mpiga kura hawezi kushawishika kama mgombea hana uhakika kuwa atashinda.

Pia Soma

Advertisement
Lowassa alishawishi idadi kubwa ya Watanzania kupanga foleni kwenye mistari ya kuingia kupiga kura kwa sababu alijenga imani kwa watu kuwa angeweza kushinda na kutangazwa kushinda. Angenadi hofu ya kuibiwa kura, pengine waliopiga kura wangekuwa pungufu ya waliojitokeza.

Matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanyika mfululizo kati ya 2016-2019 na Serikali za Mitaa 2019 na jinsi wapinzani walivyoambulia patupu, ni namna wanavyojinadi kuibiwa kura, wanawapa hofu wapiga kura kwamba kumbe kupanga foleni kuelekea vyumba vya kupigia kura si kitu kinachoweza kuleta mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Imani kwamba matokeo halisi hubadilishwa huwavunja moyo wapiga kura. Hudhani kwamba sauti zao hazitasikika, kwa hiyo huona bora kukaa nyumbani.

Mwaka 2015, watu wengi walijitokeza kupiga kura za urais kwa sababu Lowassa alionekana kuwa tishio na namna alivyowapa watu uhakika kwamba angeshinda na kutangazwa mshindi, ilisababisha mwamko upande wa CCM kujitokeza kwa wingi kumpigia kura nyingi Rais Magufuli.

Wapinzani kulalamika kuibiwa kura, na bila tume huru hawatapa chochote, inafanya vyama vyao vionekane vimejaa unyonge visivyoweza kuutetea ushindi wao, hii inawakatisha tamaa wapiga kura.

Columnist: mwananchi.co.tz