Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA YA MALOTO: Upendeleo wa maamuzi huzua maswali mengi utastaajabu Bunge

51522 Pic+maloto

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Double standard ni kifungu cha maneno ya Kiingereza, chenye maana ya upendeleo. Hapa ndipo utapenda utajiri wa Kiswahili, maneno mawili ya Kiingereza, yanaleta tafsiri sawa na neno moja la Kingereza.

Kwa kosa lilelile lililompeleka mtu jela, mwingine anasamehewa au analindwa hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yake. Mazingira yaleyale yaliyosababisha watu wabomolewe nyumba zao, wengine hawabomolewi. Huo ni upendeleo.

Septemba 2017, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, aliandika Twitter: “Bunge siku hizi ni Idara ya Tawi la Utawala.” Tafsiri ya maneno hayo ni kuwa Bunge limeacha wajibu wake wa kikatiba ambao ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali na kufanya kazi ya Serikali.

Kwa maagizo ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, Zitto alikamatwa, akafikishwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Alipelekwa kujieleza ni kwa nini alitoa matamshi yenye kulikosea heshima Bunge.

Baada ya kutoka kwenye mahojiano na kamati, Zitto aliweka mtandaoni majibu yake, namna alivyopangua hoja moja baada ya nyingine kuhalalisha maneno yake kwamba Bunge limekuwa likifanya kazi kama tawi la Serikali, badala ya kusimamia hadhi yake kama mhimilinhuru wa dola.

Katika majibu yake hayo ambayo wenye kumbukumbu, watayakumbuka jinsi yalivyosambaa mitandaoni, Zitto hakuomba radhi, bali alisema yeye alitoa maoni yake kama Mtanzania na kama ilivyo haki yake kikatiba.

Januari mwaka huu, mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof Mussa Assad ni kwa nini ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea?

Alijibu: “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huwenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”

Ndugai aliagiza aende kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge aeleze kwa nini alisema Bunge ni dhaifu. Alisema kuwa kama CAG hatakwenda mwenyewe, basi angekamatwa na kupelekwa kwenye kamati na pingu ili ajue Bunge siyo dhaifu.

Hukumu iliyotolewa

Kwa tafsiri, maneno Bunge limekuwa tawi la Serikali ni sawa tu na kusema Bunge ni dhaifu. Tofauti iliyopo hapo ni uchaguzi wa maneno. Bunge kutamkwa kuwa tawi la Serikali, huo ndiyo udhaifu wenyewe. Bunge linaisimamia Serikali, halifanyi kazi kama idara ya Serikali.

Imekuwaje kosa la Zitto mwaka 2017 halikuchukuliwa hatua, halafu la CAG mwaka 2019 lisababishe fadhaa kubwa hadi kuiingiza nchi kwenye mgogoro wa kikatiba? Bunge limeamua kutofanya kazi na CAG, wakati inafahamika kuwa kazi ya kukagua na udhibiti wa hesabu za Serikali, unafanywa na CAG kwa niaba ya Bunge.

Muhimu hapa ni kuhoji kama Zitto alitumia maneno ambayo yalitafsiri Bunge ni dhaifu, mbona hakuchukuliwa hatua, lakini CAG imeamuliwa hivyo? Mbona wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Goodbless Lema (Arusha Mjini), wameadhibiwa kwa kuunga mkono tu kauli ya CAG kuwa Bunge ni dhaifu?

Hasira dhidi ya CAG ni kuwa aliyasema maneno hayo nje ya nchi. Je, ukisema Bunge ni dhaifu ukiwa Tanzania siyo kosa? Mbona Mdee na Lema wameunga mkono kauli ya CAG wakiwa ndani ya nchi? Au kosa lao ni kuunga mkono kauli iliyotolewa nje ya nchi?



Columnist: mwananchi.co.tz