Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA YA MALOTO: Ripoti CAG: Wapo wanaotamani sheria za fedha zisiwepo

52767 PIC+CAG

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inawezekana kwako kuna mshangao mkubwa, kwamba mwaka wa nne, Rais John Magufuli akiwa madarakani, bado kuna matatizo mengi ya nidhamu ya usimamizi na matumizi ya fedha za umma, wakati nchi ina Rais mkali, mwajibikaji na mwajibishaji kuliko wakati wowote.

Huo unaweza kuwa mshangao kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2018, kuonyesha changamoto nyingi hasa nidhamu ya fedha za umma, utii wa Katiba na Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001.

Ukisoma Katiba ibara ya 135 na Sheria ya Fedha za Umma kifungu cha 11, utakuta maelekezo kuwa fedha zote zenye kukusanywa kwa ajili ya matumizi ya Serikali, zitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Ibara ya 136, inasema fedha hazitatoka Mfuko Mkuu wa Serikali mpaka zipatiwe idhini kwamba kweli zinatolewa kwa minajili husika.

Katiba ibara ya 143 inamtambulisha CAG kuwa ndiye atatoa idhini ya fedha kutolewa Hazina. Ripoti ya CAG, inasema kuwa katika makusanyo ya fedha za bajeti mwaka uliopita, kutoka kwenye kundi la misaada na mikopo ya nje, Sh5.3 trilioni zilikusanywa. Sh1.6 trilioni hazikuingia Mfuko Mkuu wa Hazina, badala yake zilikwenda moja kwa moja kwenye mradi.

Pamoja na CAG kumtaka Waziri wa Fedha kushughulikia hilo, swali ni hili; unadhani waliozielekeza fedha hizo kwenye matumizi bila kupita Hazina hawajui? Wanajua sana. Unaweza kubahatisha kwamba kuna watu huona sheria zinawabana, kwa hiyo wanatamani zisiwepo ili wawe wanachota na kutumia fedha kiholela.

Dhahiri, kwa vile fedha hizo hazijaingia Hazina, maana yake hazijakaguliwa na zimekosa idhini ya CAG. Unaweza kuona na tukio dogo lakini ukweli ni kuwa Katiba imevunjwa. Na hapa ndipo Bunge hutakiwa kukunjua makucha yake na kuhoji ni kwa nini Serikali inatumia fedha bila utaratibu? Mwaka jana tulikuwa na wimbo wa Sh1.5 trilioni.

Hilo la fedha kutowasilishwa Mfuko Mkuu wa Hazina, lipo pia kwenye makusanyo ya fedha kutoka balozi saba. Sh2.5 bilioni zilikusanywa lakini hazikuwasilishwa Hazina. CAG anasema kuwa mwaka wa fedha 2016-2017, Sh14.5 bilioni zilikusanywa na balozi 21 pasipo kuingizwa Hazina. Anasema tatizo hilo la kutotii sheria limekuwa kubwa kwa asilimia 82.5.

Kwa asilimia hizo, maana yake ni kwamba kama ingekuwa ni mtihani, Tanzania ingekuwa na alama A ya kutotii sheria zake yenyewe ya matumizi ya fedha za umma.

Nidhamu ya manunuzi kama inavyotakiwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma haipo. CAG ameandika kuwa Sh4.6 bilioni zilitumika katika kununua bidhaa, huduma, ushauri wa kitaalamu na kazi za ujenzi ndani ya wizara, idara na sekretarieti za mikoa pasipo kutumia taratibu za kushindanisha wazabuni.

Amesema hilo ni kinyume na kanuni ya 163 na 164 za Kanuni za Manunuzi ya Umma za mwaka 2013. Vilevile linaleta shaka katika kufikia thamani ya fedha katika Taasisi husika. Sehemu nyingine CAG ameeleza kuwa taasisi nane zilifanya manunuzi yenye thamani ya Sh5.4 bilioni bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ambayo ni kinyume na Kifungu cha 35(3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni 55 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013.

Hoja iliyopo

Yapo maeneo mengi yenye kuonyesha uzembe katika upungufu ulioonyeshwa na CAG. Hata hivyo, kikubwa ambacho kipo wazi ni kuwa ukiukwaji wa sheria na Katiba ni mkubwa katika matumizi ya Serikali.

Ni hapo unapata tafsiri kwamba wapo watendaji wanaona sheria zinawazuia kufanya mambo yao kwa haraka, kwa hiyo wanaamua kuzikiuka. Wangeweza wangezifutia mbali.

Ukisoma ripoti ya CAG mwanzo mpaka mwisho, jibu unalolipata ni kuwa kama sheria zingefuatwa, utaratibu wa matumizi ya fedha za umma ungezingatiwa. Na hivyo, tusingeona upungufu mkubwa kwenye ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Hali hiyo utaikuta Bandari ya Dar es Salaam ambayo ilifanyiwa kazi kubwa na Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwanzoni kabisa waliposhika usukani. Pamoja na hayo inaonekana bado tatizo halijapata ufumbuzi wa kudumu.



Columnist: mwananchi.co.tz