Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA YA MALOTO: Membe analo jambo la kumwambia Dk Slaa

73351 Pic+membe

Thu, 29 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Narejesha kumbukumbu mwaka 2007, Dk Willibrod Slaa akiwa Katibu Mkuu Chadema, yupo viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam anataja orodha ya aibu (list of shame), iliyotambulika zaidi kama orodha ya mafisadi.

Dk Slaa mwenye moto mkali, akaweka hadharani majina 11 ya vigogo aliowasema walikuwa wakiifilisi nchi.

Je, kuna shambulizi kubwa kuliko hilo? Hakusikika balozi yeyote akilalamika kuwa anapata tabu kuitetea nchi nje ya mipaka. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye ndiye kiongozi wa mabalozi, hakulalamika popote kuwa alitaabika kuitetea nchi.

Dk Slaa aliyesimama imara kuufichua ufisadi wa Sh133 bilioni Benki Kuu kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), akipiga kotekote, ndani na nje ya Bunge, si Membe wala balozi yeyote, aliyedai anapitia kipindi kigumu kutetea jina la nchi kwa sababu ya hoja ambazo alizitoa. Dk Slaa aliitwa shujaa na ameendelea kuvuna heshima kwa kazi kubwa aliyofanya.

Baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, Dk Slaa alitangaza na kunukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akisema nchi isingetawalika akidai aliibiwa kura.

Kuishia hapo kwa uchache, leo Dk Slaa sio Katibu Mkuu Chadema, wala si mwanachama wa chama hicho tena. Dk Slaa ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden.

Pia Soma

Ni kipindi hiki Dk Slaa anatokeza na kulalamika kuwa hoja za watu dhidi ya Serikali, zinawapa kazi ngumu mabalozi kuitetea nchi nje ya mipaka. Ni sawa pia kusema kuwa Dk Slaa anauona ubalozi mgumu kwa sababu ya wakosoaji. Anatamani wanyamaze ili apumue. Ni sahihi kuamini kwamba akiona watu wanaikosoa Serikali kwa sasa anakunja ndita. Anawaona wanamwongezea uzito wa kazi!

Mwaka 2007 Dk Slaa aliposimama Mwembeyanga, Tanzania ilikuwa na balozi Sweden kama alivyo yeye leo. Aliposema nchi haitawaliki mwaka 2010, nchi ilikuwa na mabalozi. Kama yeye anaona ni vigumu kuitetea nchi akiwa balozi, bila shaka na wenzake ugumu waliuona, ila walinyamaza. Afadhali Dk Slaa angekaa kimya, yaani angeuona ugumu na kuunyamazia, kwa kukumbuka na yeye aliwahi kuwapa ugumu wenzake lakini walinyamaza. Au inawezekana Dk Slaa, anakiri kuwa alikosea huko nyuma, lakini anatumia lugha yenye picha zilizokolea rangi, badala ya kunyoosha maneno.

SOMA ZAIDI

> Rais Magufuli afanya mazungumzo na Dk Slaa Ikulu

> Dk Slaa ateuliwa kuwa balozi

> Dk Slaa ajitosa sakata la Sh1.5 trilioni

> Dk Slaa amshukuru Mungu kwa uteuzi

Ambacho Dk Slaa alipaswa kusema ni kuwa anasikitikia nyakati zake za kuikosoa Serikali, kumbe alikuwa anawapa mzigo mabalozi kuitetea nchi nje ya mipaka. Tena ingewezekana angewapa pole.

Kukimbilia kuwasema wakosoaji wa sasa kuwa wanawapa wakati mgumu mabalozi, kisa yeye kwa sasa ni balozi, huo ni ubinafsi. Haya ndio yale ambayo wahenga walinena kuwa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu!

Yeye alipokuwa anarusha hoja zake, aliwaona mabalozi wanastahili ugumu aliokuwa anawapa, ila leo kwa vile balozi ni yeye, wakosoaji wanatakiwa kuacha, maana wanamuumiza.

Membe ana wakati mzuri wa kumjibu Dk Slaa, kwa sababu nyakati ambazo mwanasiasa huyo alikuwa wa moto mno katika jukwaa la upinzani, yeye ndiye aliyajua yote ya kuhusu nchi nje ya mipaka.

Kama kulikuwa na ugumu wa kuitetea nchi, Membe anaweza kumwambia Dk Slaa kuwa naye alipokuwa akirusha makombora yake majukwaani enzi hizo, yeye na mabalozi waliokuwepo walimenyeka kuinasua nchi dhidi ya hoja zake, lakini hawakulalamika.

Watanzania hawazuiwi kuikosoa Serikali yao, maana ukosoaji ni ujenzi. Wanaoshika mpini hutakiwa kupokea hoja hasi na kuzifanyia kazi.

Nchi haiwezi kujengwa kwa mapambio, kwamba kila mmoja amwage sifa. Ikitokea hivyo, wanaopaswa kutimiza wajibu wanaweza kubweteka, kwa kuona kila kitu kipo sawa. Nchi inahitaji watu wenye nongwa, wachokonoa makosa hata yenye kujificha. Hao ndio huchochea uwajibikaji.

Dk Slaa enzi zake alitimiza wajibu huo wa kuchochea uwajibikaji. Aliwafanya walioshika usukani wasibweteke. Ni zamu yake naye kuchochewa ili asibweteke. Asikimbilie kulaumu.

SOMA ZAIDI

> Membe amjibu Rostam urais mwaka 2020

> VIDEO: Membe avunja ukimya, amjibu Rostam

> Membe azungumzia Lissu kupoteza ubunge

> Kauli ya Membe kuhusu Lissu yaibua mjadala mtandaoni

Columnist: mwananchi.co.tz