Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA YA MALOTO: Majibu yaondoe utata katika matukio ya utekaji nchini

56271 Pic+utata

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Akiwa Marekani mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi wakati huo akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, aliwaambia Watanzania wanaoishi nchini humo kuwa utata wa waliompiga risasi, Tundu Lissu si wa kwanza katika historia.

Kabudi alisema, Marekani yenyewe marais wake wanne waliuawa na wahusika hawajakamatwa. Lissu alipigwa risasi Septemba 7, 2017 na mpaka leo hakuna mshukiwa hata mmoja amekamatwa.

Usahihi, anzia Rais wa 16, Abraham Lincoln mwaka 1865, Rais wa 20, James Garfield (1881), Rais wa 25, William McKinley (1901) hadi Rais wa 35, John Kennedy (1963) ndio marais wa Marekani waliopigwa risasi na kuuawa. Na waliowapiga risasi baadhi waliuawa, wengine walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifo.

Lincoln alipigwa risasi Aprili 14, 1965 na John Booth. Mpango wa kumuua Lincoln ulitokana na njama za majimbo saba yaliyokuwa yakimiliki watumwa, yaliyopingana na azimio la Lincoln la kukomesha biashara ya utumwa. Lengo la majimbo hayo lilikuwa kujitenga na Marekani ili kuwa huru kuendelea na biashara ya watumwa.

Booth alichora mpango wa kumuua Lincoln, makamu wake, Andrew Johnson na Waziri wa Mambo ya Nje, William Seward chini ya Confederate. Johnson alijeruhiwa. Seward alikoswakoswa. Booth aliuawa baada ya kukataa kujisalimisha. Wengine wote walioshiriki njama hiyo walikamatwa na kunyongwa.

Garfield alipigwa risasi na mwanasheria Charles Guiteau. Sababu ilikuwa mgogoro wa mgawo wa vyeo serikalini. Guiteau alishiriki kampeni za urais wa Garfield. McKinley alipigwa risasi na Mmarekani mwenye asili ya Poland, Leon Czolgosz. Alikamatwa na kunyongwa kwa kiti cha umeme. Alikiri kumuua McKinley kwa maelezo kuwa alikuwa adui wa watu wazuri na wachapakazi.

Kennedy alipigwa risasi na mkomunisti, Lee Oswald, ambaye alikuwa mtiifu wa falsafa za Karl Marx. Oswald alipokamatwa, akapigwa risasi na mfanyabiashara, Jack Ruby alipokuwa makao ya polisi, Dallas, Texas. Ruby alihukumiwa kunyongwa lakini alikufa kwa ugonjwa wa saratani ya pafu kabla ya kunyongwa.

Hivyo si kweli kuwa waliowaua marais wa Marekani hawajulikani na hawajawahi kukamatwa.

Hata kama ingekuwa kweli kuwa wauaji hao hawakukamatwa na hawajulikani, hoja hiyo haihalalishi kutopatikana waliomshambulia Lissu.

Serikali inatakiwa kueleza mikakati yake ya kubaini waliomshambulia Lissu, iwafanye wahalifu wawe matumbo joto na wananchi wapate matumaini. Jibu la kwamba “mbona Marekani imeshindwa” ni kuwafanya wahalifu waone Serikali ina vyombo goigoi na imeshakubali kushindwa.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema bungeni hivi karibuni kuwa kutopatikana kwa watu waliomshambulia Lissu si ajabu, maana Marekani haijawapata waliompiga risasi mwanamuziki Tupac Shakur mwaka 1996 na mwigizaji Elizabeth Short mwaka 1947.

Kangi akasema dereva wa Lissu anatakiwa ahojiwe ili polisi wafanye kazi yao. Kangi mpaka hapo anajenga tuhuma kuwa kuna mpango. Kangi ndiye waziri wa mambo ya ndani, kwa nini hatua zisichukuliwe na watu wafikishwe mahakamani?

Kama polisi wanaona dereva wa Lissu ana kesi ya kujibu, nini kinazuia kuchukua hatua kumkamata? Ikiwa Kangi anaona kuna uwiano wa matukio kutoka Wangwe mpaka Lissu, kwa nini hatua stahiki zisichukuliwe?

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alisema bungeni kuwa anashangaa watu kuhoji kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda wakati watu wengi walipotea Kibiti. Je, kwa vile Kibiti walipotea wengi hakuna uhalali wa kuhoji kuhusu Azory?

Kangi naye alisema polisi hawawezi kumtafuta Azory kwa sababu alijipoteza mwenyewe kwa sababu za kimaisha. Kimsingi majibu haya huongeza utata kuliko kuleta ufumbuzi. Ni vizuri tukijikita katika majibu ya kuondoa utata badala ya kuuongeza.



Columnist: mwananchi.co.tz