Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA YA MALOTO: Lugola kukejeliwa mitandaoni ni funzo la hulka za uongozi

94021 Pic+lugola MAKALA YA MALOTO: Lugola kukejeliwa mitandaoni ni funzo la hulka za uongozi

Mon, 3 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tangu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola atenguliwe nafasi yake na Rais John Magufuli, mitandaoni watu ni kama wameambizana. Wanamkejeli tu!

Kejeli si nzuri. Hata hivyo tunayo nafasi ya kufanya marejeo kwa wengine waliotenguliwa. Ni wangapi walikejeliwa kama Kangi? Kisha tujiulize; ni kwa nini sauti za kumhurumia hazisikiki?

Jibu ni moja; katika uongozi wa kijamii, wanajamii ni kioo. Endapo baada ya kutenguliwa, sauti nyingi za kumhurumia zingesikika sana, bila shaka wanajamii wangekuwa wanawasilisha hisia zao jinsi walivyompenda na uongozi wake.

Kwa vile wanajamii wanamnanga, ikiwemo kusambaza video zake za kusakata muziki, ni alama kuwa wanafurahia anguko lake. Hivyo, hawakupenda uwajibikaji wake.

Ni somo la hulka za uongozi. Watu wanapochaguliwa au kuteuliwa kuwa viongozi wa kijamii, watambue kuwa hulka zao watakazozionesha au wanazozionesha, ndizo zitaamua tafsiri ya maoni ya watu siku wakiondoka au kuondolewa.

Mambo ya kujiuliza ni haya; je wananchi wanamkejeli kwa sababu aliingia kwa mbwembwe? Mfano, alivyomshusha cheo aliyekuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Leopold Fungu akimwondolea hadi daraja la kijeshi kutoka kuwa mrakibu wa polisi hadi mrakibu msaidizi, ikiwa ni siku nne baada ya Kangi kuapishwa uwaziri.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kangi alimshusha pia cheo Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Kagera, George Mrutu. Uamuzi huo aliufanya kwa kumpa maagizo aliyekuwa katibu mkuu wa wizara, Meja Jenerali Jacob Kingu. Kangi alisema, alipanga kuwafukuza kazi Fungu na Mrutu, ila bahati yao siku hiyo alikuwa anasherehekea kuzaliwa kwake.

Julai 6, 2018, alimtimua kwenye kikao aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk Juma Malewa, kisa alichelewa kuingia kwenye ukumbi wa mkutano kwa dakika moja. Ikia imepita dakika moja Dk Malewa aliingia ukumbini, Kangi akafoka: “Huyo ni nani anafunguliwa mlango wakati nimeagiza mlango ufungwe. Hakuna kuingia kwenye kikao changu.” Dk Malewa akaomba radhi, Kangi akaongeza: “Hakuna msamaha hapa, rudi nje.”

Hilo ni tukio mbele ya vyombo vya habari. Taarifa za baadaye zilieleza Dk Malewa alifika eneo la mkutano kuanzia saa 3:00 asubuhi lakini kikao kiliahirishwa mpaka saa 4:00 asubuhi. Kikaahirishwa tena mpaka saa 5:00 asubuhi.

Ilielezwa kwamba baada ya kikao kuahirishwa saa 4:00 asubuhi, Dk Malewa alikwenda kwenye ofisi nyingine zilizopo ndani ya jengo hilohilo la Wizara ya Mambo ya Ndani, ndipo alichelewa kwa dakika moja. Hivyo, Kangi kama angevuta subira, angetambua kwamba Dk Malewa hakuchelewa.

Julai 13, 2018, taarifa ya Ikulu, ilieleza kuhusu uteuzi wa Kamishna Jenerali mpya wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike, aliyechukua nafasi ya Dk Malewa ambaye alistaafu.

Pamoja na wito wa subira, kitu muhimu ni staha. Unapokuwa kiongozi haimaanishi wale wa chini yako ni watoto na unaweza kuamua chochote dhidi yao. Kuheshimiana ni jambo muhimu mno.

Hata kama Dk Malewa angechelewa dakika 10, alipaswa kutumia hekima kuliko kumtoa nje mbele ya kamera na vinasa sauti vya vyombo vya habari.

Alipofanya kikao cha kwanza na wakuu wa majeshi chini ya wizara yake, alimtaka kila mmoja aonyeshe ilani ya CCM ya 2015. Alisema walipaswa kwenda kwenye mkutano na ilani ya CCM.

Aprili mwaka jana, Kangi alisema CAG Profesa Mussa Assad ni muongo na alipotosha kuhusu kashfa ya ufisadi wa sare hewa za jeshi la polisi zenye thamani ya Sh16 bilioni. Kangi akaahidi kuvua nguo.

Agosti mwaka juzi, aliwatimua kwenye mkutano maofisa wa Jeshi la Zimamoto. Kisa walijitambulisha ni maofisa wa Jeshi la Zimamoto, badala ya kusema “Zimamoto na Uokoaji”.

Kangi alipoingia ofisini, waandishi wa habari wakaona mtu si ndiye yeye, wakapata matumaini ya kuulizia kuhusu kutoweka kwa mwandishi mwenzao, Azory Gwanda.

Kangi akasema “sisi hatutafuti watu waliojipoteza kwa sababu zao za kimaisha.”

Kangi afanye mapitio ya vitendo vyake na viongizi wengine wajao nao wafanye hivyo, wataelewa ni kwa nini huyu amekejeliwa baada ya kuondolewa.

Columnist: mwananchi.co.tz