Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAKALA YA MALOTO: Kuna uongozi wa wananchi na uongozi wa kujifurahisha

38007 Liquman MAKALA YA MALOTO: Kuna uongozi wa wananchi na uongozi wa kujifurahisha

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwaka 2015 nilisoma andiko kwenye mtandao wa Forbes, lililoandikwa na Dan Pontefract, likiwa na kichwa “If You Act Like A Leader You Will Think Like A Leader”, kwamba “Kama unatenda kama kiongozi utafikiri kama kiongozi”.

Andiko hilo lilikuwa na shabaha ya kuweka mkazo kitabu cha mwandishi Herminia Ibarra, chenye jina “Act Like A Leader, Think Like A Leader”, yaani tenda kama kiongozi, fikiri kama kiongozi. Kitabu hicho kilitoka mwaka 2015 katika mfululizo wa Mapitio ya Biashara, Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani.

Mawazo yaliyounda kitabu yapo sahihi, maana uliguswa uongozi wa kibiashara. Uongozi wa kikazi ofisini. Kwamba wakati wote kiongozi lazima ajipambanue kiuongozi, namna anavyofikiri na jinsi anavyotenda. Wasaidizi wake wawe na mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake.

Inatakiwa ifahamike kuwa kuna tofauti mbili za uongozi. Kuna uongozi wa huduma na uongozi wa usimamizi. Hapa sigusii ile mitindo sita ya uongozi ambayo hufundishwa kwenye siasa na biashara.

Uongozi wa usimamizi ni kama meneja ofisini na watu wa chini yake, anawasimamia ili kuleta matokeo yenye kukusudiwa. Uongozi wa usimamizi pia ni kama Rais anavyoliongoza Baraza la Mawaziri. Waziri anavyoiongoza timu yake ya wizara na kadhalika.

Uongozi wa huduma, ni ule wa kuhudumia watu. Katika mitindo ya uongozi, unaweza kuufananisha na Servant Leadership, yaani uongozi wa kiutumishi. Uongozi wa huduma una matawi mawili.

Tawi la kwanza ni huduma ya timu. Kiongozi lazima avae viatu vya wasaidizi wake. Azingatie masilahi yao na mtindo wake wa uongozi uwe wenye kujiuliza, je, jinsi anavyowaongoza wasaidizi wake, ingekuwa yeye ndiye anaongozwa hivyo angeridhika?

Tawi la pili ni uongozi wa umma, yaani uongozi wa wananchi. Sura yake ni moja tu; kutimiza matarajio ya wananchi. Aina ya uongozi huu ni wa Serikali, Bunge na Serikali za Mitaa. Siku zote lazima wahusika wajipambanue kuwa wapo kwa ajili ya umma.

Sasa basi, falsafa ya Tenda Kama Kiongozi, Fikiri Kama Kiongozi, ina mantiki sana katika uongozi wa usimamizi. Unaowasimamia wanatakiwa kukuona wewe ni kiongozi. Hata kama unatoa uhuru wa wasaidizi wako kuamua na kutenda ndani ya mipaka yao ya kazi (free reign), lazima namna yako ya kufanya kazi na kufikiri ikupambanue kuwa wewe ndiye kiongozi.

Katika uongozi wa huduma, falsafa inayotakiwa ni “kufikiri kama mwananchi wa kawaida, tenda kama kiongozi”. Mawazo ya viongozi watumishi, sharti yafanane na ya wananchi wa kawaida. Namna viongozi wanavyotenda, itoe picha yenye tafsiri ya kuzitatua changamoto za wananchi.

Rais afikiri sawa na wananchi waliompigia kura. Mbunge awe na mawazo sawa na wapigakura wake, vivyo hivyo diwani kwa wakazi wa kata yake. Tofauti iliyopo ni kwamba mwananchi wa kawaida hatakuwa na uwezo wa kutenda, ila atafikiri jinsi ambavyo angependa ahudumiwe. Kiongozi sharti azitafsiri na kuzichakata hizo fikra za mpigakura.

Inapotokea matendo ya kiongozi hayashabihiani na namna mwananchi anavyofikiri, maana yake matarajio ya watu hayatatimizwa. Na huo unakuwa siyo uongozi wa wananchi, bali ni uongozi wa matakwa binafsi, ambao pia unaweza kuuita uongozi wa kujifurahisha.

Dhuluma ya uongozi

Ifahamike kuwa uongozi wa kujifurahisha ni dhuluma kwa wananchi. Mbunge akiwa bungeni, badala ya kuwakilisha sauti za watu waliomtuma, anakwenda kuongea tofauti au anaunga mkono ambayo wapigakura wake wanayakataa, au anayapinga yale yenye kutakiwa na anaowawakilisha, hiyo ni dhuluma.

Uongozi usioendana na hali halisi za watu, husababisha wanaoongozwa wajione mayatima. Hujiona hawana chao kwenye uongozi. Wakati moja ya nguzo za utawala bora ni kumfanya kila mwananchi ajione ana hisa sawa na wengine wote kwenye nchi.

Kwa kuliweka hili vizuri ni kwamba viongozi wengi hudhani wana leseni ya kufikiri kwa niaba ya wananchi. Watakachokiamua ndicho wapigakura watapenda jambo ambalo si sahihi.



Columnist: mwananchi.co.tz