Freedom House ni taasisi ya kimataifa isiyo ya kiserikali inayomulika uhuru na demokrasia. Makao yake makuu yapo Washington DC, Marekani. Katika ripoti yake ya Uhuru Duniani 2019 iliyotoka Januari mwaka huu, inaitaja Tanzania kuwa na uhuru kwa kiasi kidogo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Freedom House, Tanzania ni bora zaidi ya Uganda, Rwanda, Afrika ya Kati, Sudan na nchi nyingine ambazo hazina uhuru kabisa. Lakini hii si alama njema kuonesha kuwa ukuaji wa uhuru na demokrasia unatetereka. Ukiipenda nchi yako lazima ulichukie hili.
Taasisi ya Mo Ibrahim, kupitia ripoti yake kuhusu utawala wa sheria, demokrasia na ustawi wa watu Afrika, inaeleza kuwa ukuaji wa demokrasia Afrika ni wa kusuasua kulinganisha na matarajio ya watu. Waafrika wanataka demokrasia, lakini hali inakuwa mbaya kila mwaka.
Ripoti za namna hiyo zinapotoka zinatakiwa kujenga tafakuri na kujitathmini. Katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alipata kusema kuwa utafiti hujibiwa kwa utafiti. Kujitathmini ndiyo kujitafiti. Je, hali ya Tanzania ipoje? Freedom House ni wakweli au waongo?
Wakati wa kujitathmini, vema pia kukumbuka maoni mengine. Desemba mwaka jana, Bunge la Umoja wa Ulaya lilitoa maazimio kuhusu Tanzania na kwa sehemu kubwa liliinyooshea kidole kuhusu haki za binadamu, utawala bora, demokrasia, haki ya vyama vya siasa na kadhalika.
Hata mwaka 2016 ilikosolewa na mashirika mbalimbali kutokana na uchaguzi Zanzibar wa Oktoba 25, 2015 kufutwa na kuitishwa upya Machi 20, 2016.
Hivyo basi, namna ambavyo Tanzania inaweza kutajwa kwa watu wake kuwa na uhuru kidogo au kuminywa uhuru wa kisiasa, huwezi kuacha kumzungumzia Seif. Ni kama ambavyo hutaacha kuwataja viongozi wa Chadema na mapito yao ya kukaa mahabusu kuwa yanatengeneza sura mbaya ya nchi kuhusu demokrasia na uhuru wa kufanya siasa.
Wakati Seif akiwa kwenye harakati za kudai alichoona ni haki yake ya kuwa Rais wa Zanzibar, mara kilichokuwa chama chake, CUF kikaingia kwenye mgogoro wa uongozi. Profesa Ibrahim Lipumba, aliyejiuzulu uenyekiti Agosti 2015, alirejea mwaka 2016 na kudai bado ni mwenyekiti halali. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikamuidhinisha kuwa mwenyekiti halali.
Mgogoro ukasababisha Seif ajikite kwenye kutafuta ufumbuzi wa ndani ya chama na kuacha kile alichokuwa amekianza cha kusaka huruma kimataifa juu ya hatma ya urais Zanzibar. Kesi zikaenda mahakamani, hoja ya Seif na timu yake ikawa Msajili ndiye anapandikiza mgogoro CUF.
Ruzuku ya chama ikawa imezuiwa kungoja mgogoro umalizike, lakini upande wa Seif ukaeleza kuwa kambi ya Lipumba iliingiziwa ruzuku.
Hivi karibuni Mahakama Kuu iliridhia Lipumba ni mwenyekiti halali CUF, hivyo Seif na timu yake wametimkia ACT-Wazalendo. Na tayari mvutano kati ya ACT na Msajili umeanza. Siku zinahesabika tangu Msajili alipowaandikia ACT barua ya kujieleza ndani ya siku 14 ni kwa nini chama chao kisifutiwe usajili.
Kati ya hoja zilizotajwa na Msajili ni pamoja na kuhoji hesabu za mwaka wa fedha 2013-2014. Huu ni mwaka wa fedha 2018-2019. Yaani ni mwaka wa tano wa fedha kutokea mwaka huo ambao Msajili anahoji hesabu zake, lakini Seif alipohamia tu, ndani ya wiki tayari ameandika barua ya kusudio la kuifuta ACT.
Pamoja na hoja nyingine zilizoambatanishwa kwenye kusudio la Msajili, vilevile majibu ya Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe, watu wanaweza kujiuliza, hapa tatizo ni ACT au Seif na timu yake?
Na ni mwezi tangu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipopokelewa kwa shamrashamra baada ya kurejea CCM kutokea Chadema.
Vipi CCM waruhusiwe, wapinzani iwe marufuku? Lazima kutumia maarifa, haya matukio ndiyo yanaipaka matope nchi.