Tuanze kwa misahafu. Wale kaka zake Yusuf, kwa wivu tu, waliona wamtumbukize kisimani ili kumuua. Waliona anapendwa na baba yao kuliko wao.
Nduguze Yusuf waliporejea nyumbani walijitahidi kujifanya wanaomboleza. Ni kwa sababu wangefanya lolote kuonyesha kufurahia yaliyompata Yusuf, wangenyooshewa vidole kwamba wao ndio walihusika.
Hata wangetokea watu na kumsema vibaya Yusuf au kufanya sherehe kwa yaliyompata, hakuna ambaye angeacha kuhisi wamehusika na hapo kaka zake Yusuf, wangepata kisingizio.
Waliompiga risasi Tundu Lissu, mwanasheria mkuu wa Chadema Septemba 7, 2017, walikusudia kumuua. Na bado hawajulikani. Hapo ndipo inahitaji tahadhari kubwa kumzungumzia.
Kama dunia ilivyoundwa kwa milima, mabonde na tambarare, zipo nyakati za kupanda, kuteremka na kutembea kwenye ardhi iliyonyooka. Maisha yana mirindimo yake; sherehe, huzuni na mapito ya kawaida. Jirani akiwa na msiba, wewe ukafanya sherehe, jicho la kijamii halitakutaza vizuri.
Mitandaoni na katika makundi mbalimbali, kuna watu wenye uthubutu wa kumzungumzia vibaya Lissu. Ni angalizo kwao kuwa waliotaka kumuua hawajajulikana, hivyo matamshi yao, yanaweza kuibua jicho baya dhidi yao.
Pia Soma
- Ajali ya ndege ilivyokatisha ndoto za marubani wenye majina yanayofanana
- KESI YA KINA KITILYA:Mchumi aeleza jinsi mkopo wa dola 550 milioni ulivyopitishwa na Waziri wa Fedha
- Shida wanazopata mashahidi zimulikwe kwa tochi
Maisha ya binadamu yana makundi – wapo ndugu, marafiki na maadui. Ni kawaida kuwa na ndugu wengi kuliko maadui.
Na katika uhusiano wa kijamii. Ubaya huwa hautangazwi. Maana linaweza kumpata jambo uliyemtangazia vita, na kila mmoja akajua ni wewe. Utapata taabu kujinasua kwenye tuhuma.
Angalizo la pili la uhusiano wa kijamii ni ulinzi dhidi ya ulimi. Namna ulimi wako unavyochakata maneno inaweza kukuingiza kwenye tuhuma. Walimwengu waliotangulia kuishi katika jamii ya Kiswahili, walinena kuwa “ulimi uliponza kichwa”.
Katika ulimwengu wa sasa wa mitandao ya kijamii, wakati mwingine ulimi hauhusiki, bali vidole na fikra. Mtu anaandika mtandaoni kuonyesha jinsi alivyochukizwa Lissu kubaki hai, au kuna yule aliyeita waandishi wa habari na kunadi kuwa mbunge huyo “alitakiwa auawe kwa usaliti”. Unajiuliza, Je, yeye ni shabiki wa waliompiga risasi? Kijamii si ajabu kuna ambao wanahisi na huyo ni miongoni mwa wahusika.
Kiburi au chochote kile ambacho mtu anaweza kujivunia katika kutoa matamko au kauli hasi, ni kuzingatia jamii anayoishi.
Watu wana akili timamu, wameshajenga fikra za namna ya kuhusika na mapito ya nyakati. Wanajua kwamba Lissu alitendewa unyama na hapaswi kuwepo wa kukenua. Anayekenua, anavuna chuki ya jamii.
Katika angalizo la maisha, kuna hekima ya wakati wa kuonyesha uadui. Unaweza kushangilia adui yako akigombana na mwenza wake wa ndoa au wanasiasa wanaweza kufanya tafrija, pale chama hasimu kinapopitia migogoro. Kisiasa si kitu cha kushangaza.
Itaibua kila tafsiri hasi, ikitokea wanasiasa wakisherehekea kushambuliwa au kukaribia kuuawa kwa mpinzani wao.
Hapo ndipo kwenye elimu kuwa japo chuki ni kubwa kiasi gani, inatakiwa uwe makini wakati wa kudhihirisha uadui.
Maana jamii ina namna yake ya kuhukumu. Inaweza isikufunge jela, lakini hukumu yake ni hasira dhidi yako.
Lissu kapona au amekaribia kupona. Bado anachechemea, lakini ni nafuu kubwa kutoka kulala kitandani, kutegemea magongo na sasa anainua miguu mwenyewe. Mungu mkubwa!
Unaweza usiite miujiza kama ya Yusuf kuokolewa kwa ndoo na mchota maji kisimani, au Ibrahim alivyobaki salama katikati ya moto, ila hili haliwezi kupingwa kuwa ni mkono wa Mungu – yaani, risasi 16 kupenya mwilini kati ya 38 zilishambulia gari lake lisilo na kinga ya risasi.
Kijamii, inategemewa watu wafurahie kupona kwake, maana Mungu ameshinda na udhalimu wa uporaji nafsi umeshindwa.
Mazingira ya jumla ya Lissu kupona muweke Mungu. itakuhukumu. Kuna msemo maendeleo hayana vyama, tuongeze pia unyama hauna vyama.