Ndege ya Serikali, inayotumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imerejea Tanzania kwa amri ya Mahakama, baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa, Afrika Kusini.
Ndege imerejea na ujumbe wa aibu kuwa Watanzania si wamoja. Wapo waliodhihirisha shangwe kwa ndege hiyo, Airbus 200-300 kushikiliwa, wengine walikasirika mpaka wakaandamana katika ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania.
Mambo ya kimahakama watu wakaandamana hadi ubalozi wa Afrika Kusini, eti kushinikiza nchi hiyo iiachie ndege yao. Hakika, Airbus ya ATCL imewaumbua Watanzania na kuwatangaza katika sura mbaya.
Airbus ya ATCL imewaumbua Watanzania katika maeneo mawili; kwanza ni kuwa Watanzania hawajui kutofautisha masuala ya kisiasa na mahakama. Ndege ilishikiliwa kwa amri ya mahakama na iliachiwa kwa uamuzi wa mahakama. Yale maandamano ya ubalozi wa Afrika Kusini, yaliitangaza vibaya nchi yetu.
Pili ni kuwa Watanzania hawajui kutofautisha mitazamo ya kisiasa, itikadi zao na mali za nchi. Wapo tayari mali zao zipotee kwa sababu za kisiasa. Kuna waliochekelea ndege ilipokamatwa, na hakika wameumia ilipoachiwa. Shangaa kwamba ndege hiyo ni mali yao na ilinunuliwa kwa kodi zao. Wapo tayari kuona jasho lao linapotea bure ili kufurahia maslahi ya kisiasa.
Walioumia ndege kushikiliwa si hoja nzito, maana ndivyo ilipaswa kuwa. Ni ndege yao, iwe ilishikiliwa kwa makosa au halali, inatakiwa kuwauma.
Pia Soma
- Ekari 150,000 mto Rufiji kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji
- Wizara ya Afya yataja sababu gharama vipimo Muhimbili kuwa juu
- Mbunge ataka sheria kudhibiti wanaochafua hewa kwenye ndege
Wakati wa goli la kuongoza (ndege iliposhikiliwa) watu wa timu moja walishangilia kwa namna ya kuwabeza wenzao ambao walikuwa upande wa Serikali, wakitaka ndege iachiwe. Ndege ilipoachiwa, ilikuwa mithili ya lugha za watu wa michezo, kwamba timu B “ilipindua meza kibabe”. Yaani iligeuza matokeo. Wakaanza kuwananga walioshambulia awali. Nchi haikufurahi pamoja ndege ilipoachiwa, haikulia pamoja iliposhikiliwa. Ni ujumbe mbaya sana.
Mbaya zaidi ndege ilishikiliwa si kwa makosa au matokeo ya siasa za sasa, bali kwa sababu ya utekelezaji wa sera ya utaifishaji mali za watu binafsi kuwa za umma, wakati wa awamu ya kwanza.
Raia wa Afrika Kusini, Hermanus Steyn, anatajwa kuwa alikuwa anamiliki ardhi kubwa, mifugo na mali nyingi, zikataifishwa na Serikali ya Tanzania miaka ya 1980.
Kwamba Steyn anaidai Tanzania dola 4.1 milioni (takriban Sh9 bilioni kwa sarafu ya sasa). Vilevile kuna riba imekuwa ikiongezeka. Ombi la Steyn kwa mahakama kuamuru Airbus ya ATCL izuiwe ni kutaka Serikali ya Tanzania ione ulazima wa kulipa deni haraka.
Unajiuliza sasa, waliokuwa wanasherehekea waliguswa na kipi? Tena vijana wengi waliokuwa wakipaza sauti kusherehekea na kuzodoana mitandaoni, hawakuwa wamezaliwa wakati sakata la Steyn lilipoanza.
Tukio la Airbus ya ATCL kuzuiwa Afrika Kusini, limetoa ujumbe kuwa Tanzania imerudi nyuma karibu muongo mmoja. Kabla ya mwaka 2010, Zanzibar ndivyo ilivyokuwa. Siasa zilisababisha uadui wa kijamii, ndugu wakafarakana, majirani wakahasimiana, hawakuchangia sherehe wala misiba.
Rais wa sita wa Zanzibar, Aman Karume, katika muhula wake wa kwanza (mwaka 2000-2005), aliona anaongoza nchi ambayo baadhi ya watu hawakumwona kama Rais wao, waliishi kwenye nchi kwa kufuata sheria lakini hawakuwa radhi naye. Kundi la pili lilimtambua kuwa ni kiongozi halali.
Lile kundi ambalo halikumwona ni kiongozi halali, liliishi kama ambavyo watu waliishi nyakati za ukoloni. Walitii mamlaka, lakini hawakuridhia uhalali wa kuongoza naye. Mtaa wa kwanza ni wananchi; kuheshimu mamlaka, kupenda mema ya nchi yao. Kushirikiana na mamlaka kujenga na kulinda taifa.