Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lugha ya mazungumzo katika uandishi rasmi

15587 Erasto+Duwe TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika toleo lililopita la gazeti hili tuliandika kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili baadhi ya waandishi.

Miongoni mwa changamoto hizo moja ni matumizi ya lugha ya mazungumzo katika uandishi rasmi.

Wasomaji wa safu hii walipiga simu na kutuma ujumbe wakiomba tutoe ufafanuzi zaidi kuhusu matumizi ya lugha hiyo ya mazungumzo katika uandishi.

Kwa kuwa lengo la Mbalamwezi ya Kiswahili ni kuelimisha kuhusu lugha ya Kiswahili na fasihi yake, ni wajibu wetu kutoa ufafanuzi huo. Awali ya yote ifahamike kwamba kuna tofauti kubwa kati ya lugha ya maandishi na lugha ya mazungumzo. Uandishi ulio rasmi aghalabu hutumia lugha rasmi pia.

Hata hivyo, mara chache lugha ya mazungumzo inaweza kutumiwa katika uandishi rasmi katika muktadha maalumu wa kutoa ufafanuzi, mifano, nukuu ili kuthibitisha kauli fulani na mengineyo.

Katika uandishi mathalani wa barua rasmi, hotuba, risala, dokezo, tasnifu, insha na ripoti mbalimbali, taratibu zinatuongoza kutumia lugha ya kimaandishi na kuepuka kuandika kama vile tunafanya maongezi.

Baadhi ya tofauti za lugha ya maandishi na ile ya maongezi ni kwamba, katika lugha ya maandishi, mwandishi hufungwa na kanuni maridhawa za uandishi ilhali katika lugha ya mazungumzo mwandishi yu huru kutumia lugha vile aonavyo kulingana na mawasiliano afanyayo.

Pia, katika lugha rasmi lengo la kuandika huzingatiwa zaidi na kupewa kipaumbele, kwa hivyo, hata msamiati na istilahi zinazotumiwa katika uandishi huo zinaendana na madhumuni ya uandishi husika. kumbe katika mazungumzo, mzungumzaji huwa huru kutumia msamiati vile apendavyo.

Kwa ujumla, uandishi umejikita katika matumizi ya lugha rasmi tofauti na lugha ya mazungumzo ambayo humpa uhuru mzungumzaji.

Kama tulivyosisitiza katika toleo lililopita, uandishi wa nyaraka rasmi hauna budi kuzingatia lugha rasmi ya maandishi.

Hata hivyo, baadhi ya waandishi wameshindwa kutofautisha aina hizo za uandishi. Badala ya kutumia lugha ya uandishi, wamekuwa wakitumia lugha ya maongezi katika uandishi wa kazi rasmi za uandishi.

Tuangalie mifano ifuatayo:

1.Nilipokwenda mwenye ofisi yake nilimkuta hayupo (nilipokwenda ofisini kwake sikumkuta)

2.Hata hivyo, sikuona naniliu niliyokuwa nimepanga kumwomba (hata hivyo, sikuona nilichokuwa nimekusudia kumwomba)

3.Alikatwa na mapanga utadhani nyama inavyokatwa buchani (alikatwa kwa mapanga kama vile nyama ikatwavyo buchani)

4.Penye pale alisema penginepo asingefika (alisema pengine/huenda asingefika)

5.Mi napendaga sana vibua (huwa napenda sana vibua).

Ukichunguza mifano iliyotolewa, utabaini kuwa takribani kila tungo ina kasoro zake. Kasoro hizo kwa namna moja au nyingine zinatokana na athari za lugha ya mazungumzo.

Kutokana na kuathiriwa na lugha hiyo, baadhi ya waandishi huandika kama wanavyoongea.

Mpendwa msomaji, kuna athari nyingi za mtu kuandika kama anaongea. Kazi iliyoandikwa kwa namna hiyo hukosa urasmi, hadhi na mvuto, huwa na uradidi mwingi na pengine hukosa kueleweka. Msingi wa uandishi bora, huanza kujengwa katika ngazi za awali mtoto anapofundishwa kuandika. Walimu katika viwango vya shule za msingi na sekondari, wana wajibu mkubwa wa kuwafundisha wanafunzi misingi ya uandishi bora.

Wanafunzi wasipofundishwa uandishi bora katika ngazi hizo za elimu, wengi huingia katika vyuo vikuu wakiwa na kasoro kubwa katika uandishi. Hata hivyo, ni wajibu wa mtu binafsi kuchukua hatua za kuboresha uandishi wake.

Columnist: mwananchi.co.tz