Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lowassa alikuwa mpita njia Chadema, CCM ni kwao

Lowassa alikuwa mpita njia Chadema, CCM ni kwao

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kabla Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hajahamia Chadema mwaka 2015, chama hicho kilimchukulia kama mhalifu, mtuhumiwa wa ufisadi na hata kwenye orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi (list of shame) jina hilo halikukosekana.

Lowassa aliyejizolea umaarufu mkubwa tangu miaka ya 1995 alipojitokeza kugombea urais na wenzake akiwemo Jakaya Kikwete (Rais mstaafu wa awamu ya nne), aliendelea na ndoto yake hiyo ambayo haijawahi kutimia.

Waliendeleza ushirikiano wa kundi lao na Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005 alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu, lakini hata hivyo cheo hicho hakikudumu kwani mwaka 2007 alikumbwa na kashfa ya mradi tata wa ufuaji umeme wa Richmond.

Lowassa aliyekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuwa Rais alijikuta kwenye majanga mwaka 2007 baada ya kukumbwa na kashfa ya mradi tata wa umeme wa Richmond na kusababisha kupoteza Uwaziri mkuu.

Licha ya kuchafuliwa na kashfa hiyo, Lowassa hakukata tamaa ya kuupata urais na ilidhaniwa kuwa angepitishwa baada ya utawala wa awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete kumaliza miaka 10.

Lakini, ghafla akatoswa na chama hicho na badala yake akapitishwa Rais John Magufuli.

Pengine ni kutokana na kiu ya urais, Lowassa akatimkia Chadema ile ile iliyokuwa ikimbeza na wao kwa tamaa yao ya kuongeza kura wakampokea.

Lakini cha ajabu, CCM waliomtosa Lowassa wakashikwa na gere na kuanza kumbeza. Sasa ikawa zamu ya chama hicho kuisakama Chadema kwa kumpokea ‘fisadi’ na kwamba wameanza kumsafisha.

Ilileta shida kwa baadhi ya makada wa chama hicho akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden aliyeamua kujitoa.

Baada ya kuukosa urais alioufuata Chadema mwaka 2015, Lowassa ameona hana la kufanya tena kwenye chama, ila kujirudia tu CCM.

Sasa kibao kimegeuka, Lowassa siyo mhalifu tena kwa CCM bali ni mtu mwema kwa kuwa ameridhishwa na utendaji wa kazi za Rais Magufuli na kwamba maendeleo hayana chama.

Hii inamaanisha kuwa vyama vya siasa ama havina itikadi au haviwezi kuzisimamia itikadi na miiko yao. Kwa mfano CCM wanasema wanasimamia Sera ya Ujamaa na Kujitegemea, lakini ukifuatilia utendaji wao usishangae kuuona ukifanana na uliberali. Zamani makada wa CCM walipewa mafunzo na kuapishwa kuwa wanachama. Leo CCM imebaki kugombea wanachama na vyama vya upinzani bila kujali uadilifu wala itikadi ya chama.

Siasa zimegeuka kuwa biashara na hapo ndipo utasikia mbunge au diwani amejivua nyadhifa zake zote kwenye chama A, halafu kesho yake anagombea tena ubunge au udiwani kwa chama B.

Tena utashangaa chama B kinampa upendeleo kuliko wale wafia chama aliowakuta na wala mchakato wa kura za maoni haufanyiki. Tumeshuhudia wabunge wengi wa upinzani wakihamia CCM kwa mtindo huu wa fasta fasta.

Kwa wapinzani nako kuna shida, kwani licha ya kuhubiri uadilifu, wako tayari kupokea mtu yoyote agombee hata urais bila kujali wasifu wa mtu huyo. Kwa hili Chadema wanastahili lawama kwani hawakuzingatia wanachokihubiri.



Columnist: mwananchi.co.tz