Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lowassa, Maalim Seif ‘maisha yanakwenda kasi’

49749 Pic+lowassa

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar. Kuna msemo wa siku hizi kwamba ‘maisha yanakwenda kasi sana.’ Miezi 40 iliyopita, kuna watu wawili walitikisa uchaguzi Mkuu kutoka vyama vya upinzani. Hawa walikuwa Edward Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad.

Lowassa aliyekuwa akiwania urais kupitia Chadema anaweza kuwa ndio chanzo cha matumizi ya neno mafuriko.

Umati mkubwa uliokuwa unajitokeza katika mikutano yake ya kampeni ilitosha kumfanya apende kutumia neno mafuriko, na haikuwa ajabu kusikia jeuri yake kuwa mafuriko hayawezi kuzuiwa kwa mikono.

Chadema ilionekana kuimarika kutokana na ujio wa Lowassa na wafuasi wake kutoka CCM.

Umati mkubwa wa watu katika mikutano ya Lowassa iliwafanya baadhi ya wanasiasa kudhani picha hizo zilikuwa zikitengenezwa.

Haikuwa ajabu kuona waziri mkuu huyo wa zamani akipata zaidi ya kura milioni sita ambazo ni nyingi kuliko za mgombea mwingine yeyote wa upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyila mwaka 1995.

Baada ya kushika nafasi ya pili nyuma ya Dk John Magufuli, wengi walitarajia ushawishi wa Lowassa ungeibuka tena katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.

Kutokana na kura alizopata na ushawishi wake mkubwa, hakuna aliyedhani mbunge huyo wa zamani wa Monduli angerejea CCM.

Ukiangalia upande wa pili wa nchi, Maalim Seif alikuwa na nguvu kubwa katika kuwania urais wa Zanzibar.

Ingawa nguvu yake hiyo imejidhihirisha katika chaguzi zote, lakini mwaka 2015 ilikuwa ya aina yake kwa sababu alikuwa makamu wa kwanza wa rais hivyo kuwa na kitu za ziada tofauti na miaka ya nyuma aliposhiriki akiwa kiongozi wa CUF pekee.

Kwa ujumla, CUF ilionekana chama chenye ushindani mkubwa kwa CCM na ushawishi wa Maalim Seif ulikuwa tishio.

Miezi 40 baadaye unaposikia Lowassa amerudi CCM na Maalim Seif amejiunga na ACT Wazalendo inayoongozwa na Zitto Kabwe, unapaswa kukumbuka kuwa muda unakwenda haraka sana.

Siasa ndani ya miaka mitatu imebadilika kabisa na miaka miwili iliyobaki, mambo yanaweza kuwa tofauti kabisa.

Kwa jinsi mambo yalivyobadilika ndani ya kipindi hicho na hasa majina hayo makubwa kubadili vyama, kila kitu kimebadlika. Kama Chadema ilikuwa na mpango wa kumsimamisha tena Lowassa sasa haiwezekani tena na CUF hasa Zanzibar inapita katika wakati mgumu wa kupambana na mwasisi wake ambaye tangu alipotangaza kuhamia ACT chama hicho kipya kimekuwa kikitangaza kusomba wanachama wapya kila kukicha.

Wasemavyo wasomi

Alipotakiwa kutoa maoni yake, mhadhiri mwandamizi wa idara ya siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema inaashiria kuwa watu wanapata haki zao za kisiasa na kiraia nchini.

“Mwanasiasa yeyote anatafuta jukwaa la kumfanya atimize azma yake ya kisiasa. Kwa wanasiasa wazee wanapambana waache kumbukumbu katika maisha yao ya siasa ndiyo maana wao hupambana zaidi,” alisema Dk Bana.

Alisema Lowassa alihamia Chadema iliyokuwa imara ili kutimiza malengo yake ya kisiasa na Maalim Seif amefanya hivyo baada ya mgogoro ambao kama angebaki CUF ungemmaliza.

“Maalim bado ana ndoto ya kuwa Rais wa Zanzibar baada ya mgogoro ule ndani ya chama chake hakuwa na budi kuhama,” alisema.

Alisema uchaguzi ujao utakuwa tofauti na pengine mwaka 2025 kusiwe na tofauti.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema hatua hiyo inaashiria uhuru wa wanasiasa jambo ambalo ni zuri kwa mustakabali wa siasa nchini.

“Wote walikuwa muhimu katika vyama vyao, Lowassa alihama na watu wengi, kura za urais za Chadema na idadi ya majimbo na kata viliongezeka. Kinachoendelea Zanzibar ni ishara kuwa Maalim Seif naye amehama na watu wengi hivyo huenda ACT kikawa chama kikubwa cha upinzani visiwani kama ilivyokuwa CUF ambayo huenda ikakosa nguvu,” alisema.



Columnist: mwananchi.co.tz