Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lini tutaacha kuwapa dada zetu sifa wasizostahili?

Why To Celebrate Women Day Lini tutaacha kuwapa dada zetu sifa wasizostahili?

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Siku ya Wanawake Duniani ilikuwa juzi tu Machi 8. Majina mengi sana ya kuonyesha umuhimu na uimara wa mwanamke yalitajwa. Wapo walioitwa Super Woman, Malkia wa Nguvu na Mwanamke wa Shoka.

Baada ya hapo namuona Mwanamke wa Kitanzania anarudi kulekule kwa zamani, anaanza kuomba vocha, pesa ya kwenda saluni, kulipiwa nauli lakini hakuna kitu kizuri kama kuwa na uhuru wa kiuchumi.

Kinadada wanaojimudu huwa hawanyanyaswi na mtu, Inasikitisha kuona baadhi ya kinadada wakiendelea kujilegeza, inasikitisha kuona baadhi yao bado wanaendelea kulipiwa bili kila siku.

Unaweza kuwa sehemu unaburudika siku za wikendi na ukatamani kumuita rafiki yako wa kike aje Unajua nini kitakuboa? Ni kujilegeza kwake kulikopitiliza. Utaanza kumlipia usafiri, kinywaji.

Ipo haja kubwa ya dada zetu kuanza kubadilika ili kuepuka fedheha wakati mwingine.

Ukiitwa mahali kwenda kupata chakula cha usiku beba hata pesa kidogo kwenye mkoba wako. Tabia ya kutegemea mwanaume atalipa kila kitu kuna siku itakuponza. Kuna siku tu itakula kwako. Imewahi kutokea mwenzako kaitwa mchana akapate chakula, kufika hotelini hajamkuta mtu. Umeenda na usafiri wa kukodi. Umeenda huna hata senti tano mfukoni.

Kuna siku watu watakutia aibu mbele za watu. Kuna siku watu watakudharau. Jitahidi walau uweze hata kumudu maisha yako tu ya kawaida. Jitahidi walau kuwa na akiba kidogo tu kwenye pochi. Mwanaume wakati mwingine anapenda mwanamke anayeweza kujitegemea. Anapenda mtu anayeweza kujifanyia walau vitu vidogo vidogo.

Siku ya Wanawake Duniani ilikuwa juzi tu. Majina mengi sana ya kuonyesha nguvu ya mwanamke tuliyasikia. Ni siku ambayo Sauti ya Mwanamke wa Shoka ilisikika. Ni siku ambayo Super Woman alitamba kila kona ya duniani. Ni siku ambayo Malkia wa Nguvu alikuwa jasiri sana. Nguvu ya Mwanamke haipaswi kuishia tu Machi 8. Inapawa kuwa na mwendelezo. Tabia ya kutembea bila hata akiba kidogo kwenye pochi itakuja kuwapa aibu kubwa dada zangu.

Ukiitwa sehemu kwenye kupata kinywaji Jumapili kama hii usiende mikono mitupu. Beba akiba yako kidogo kwenye pochi. Inasaidia kukuweka huru. Inasaidia kukupa heshima. Unaweza kuitwa sehemu na watu wakakukimbia. Unarudije nyumbani? Usinipe jibu. Unaweza kuitwa sehemu na ukakuta watu wamebadilisha kijiwe. Unafanyaje na hujatembea hata na senti tano mfukoni? Dada zangu huu ni wakati wenu wa kubadilika na kupunguza kujilegeza. Inasaidia sana nyie kuheshimika. Inawajengea heshima kwa jamii. Usitoke tu nyumbani mikono mitupu.

Usitoke tu nyumbani bila hata kubeba nauli kidogo mkononi.

Nimewahi kumshuhudia dada ameitwa mahali na rafiki yake, lakini baada ya muda kidogo wakakosana. Kila mtu anatakiwa kuondoka kivyake. Unajua nini kilimtokea dada? Ni Aibu tupu. Kupendeza sana wakati pochi haina hata Sh1,000 ya kulipia bodaboda ni tatizo kubwa. Kupendeza sana wakati huna hata elfu 10 ya akiba, kuna siku utaaibika.

Kinadada wengi wamezuiwa pochi zao kwa kutegemea kulipiwa na mtu mwingine. Kinadada wengi wamenyang’anywa simu kwenye baa kwa sababu hizohizo za kupenda mteremko. Beba walau pesa kidogo kuna siku utanishukuru. Usipende kujilegeza sana. Kuna siku utaaibika.

Uhuru wa kiuchumi ni muhimu sana dada zangu. Mwanamke anayejitegemea kiuchumi huwa anaheshimika sana. Mwanamke anayejitegemea kimaisha huwa anajiamini sana. Ni muda sasa wa kupinga utegemezi. Ni muda sasa wa kuongeza thamani ya mwanamke. Usikubali kuja kuaibishwa mbele ya jamii kwa sababu tu ya kushindwa kujilipia chakula. Usikubali kuja kupata aibu kwa kutokuwa hata na pesa kidogo ya nauli.

Ukialikwa mahali Jumapili kama ya leo, nenda ukiwa na akiba. Kuendelea kujilegeza kuna siku kutakugharimu. Utaitwa sehemu na usiwakute waliokuita, utaaibika.

Ile nguvu iliyokuwepo Machi 8 inabidi iwepo siku zote. Ule morali uliokuwepo Siku ya Wanawake Duniani inabidi uwepo siku zote. Kuna muda unapata aibu kwa sababu tu ya kushindwa kujisimamia. Kuna muda mwanamke thamani inashuka kwa kujilegeza tu kwenye vitu vidogovidogo. Ni wakati wa kuongeza thamani ya mwanamke.

Hongereni sana kinadada wachapa kazi. Hongereni sana kinadada wapiganaji. Wapo kinadada wengi tu ambao wanajiendesha kiuchumi wenyewe.

Wapo kinadada wengi tu ambao moto wa Siku ya Wanawake Duniani wanaishi nao kila siku. Hawa ndiyo watu wa mfano. Hawa ndiyo watu wanaopaswa kuigwa na kinadada wengine wote waomba nauli. Hakuna kitu kizuri kwenye maisha kama kuwa na uhuru wa kiuchumi. Hakuna mtu yeyote atakayekunyanyasa. Hakuna mahali popote utakapopata aibu.

Kama umejifunza chochote kutoka hapa, usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Columnist: www.mwananchi.co.tz