Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwanini Spika Ndugai alisema Rais Magufuli anaweza kulivunja bunge

10156 Spika+pic TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni sheria iliyo dhahiri kuwa iwapo Bunge linagomea kupitisha bajeti na masuala mengine, Rais anayo mamlaka ya kulivunja na kuitisha uchaguzi mpya.

Si kitu cha kumkumbusha mbunge kwa kuwa anakijua na ni lazima akijue.

Lakini, kabla ya Bunge kupitisha bajeti ya mwaka 2018/19, Spika Job Ndugai alisema kitu kilicho dhahiri.

“Endapo mlio wengi mtaikataa bajeti ya Serikali, Bunge hili Rais atalivunja haraka. Na baadhi yenu, mkirudishwa majimboni hamrudi kwa hiyo akili za kuambiwa changanya na zako,” alisema Spika Ndugai juzi Jumanne.

Spika Ndugai alitoa kauli hiyo kabla ya wabunge kuipitisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 ya Sh32.45 trilioni. Bajeti hiyo ilipita kwa kura 266 kati ya 348 zilizopigwa, hiyo ikiwa sawa na asilimia 76.

Kauli ya Ndugai ilitokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 90(2) kifungu kidogo cha (b) kinachompa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano kulivunja Bunge, “kama

limekataa kupitisha bajeti iliyopendekezwa na Serikali”.

Majukumu makuu ya Bunge kwenye mchakato wa bajeti ni kuchambua bajeti kupitia kamati zake za kudumu; kukubali ama kukataa bajeti; kusimamia utekelezaji wa bajeti na utendaji wa wizara, idara na wakala wa Serikali na kusimamia matumizi ya fedha za umma.

Soma zaidi

Ndugai awaambia wabunge wakiikataa bajeti, Rais atavunja Bunge

·Wabunge wapitisha bajeti, Ndugai akionya

Nchini Tanzania, Bunge huwa halina mamlaka ya kurekebisha bajeti wala kuhamisha fedha kutoka sehemu moja hadi nyingine. Japokuwa Bunge linaweza kukataa kupitisha bajeti iliyowasilishwa na Serikali. Lakini matokeo ya uamuzi kama huo ni mazito kwa kuwa Rais anayo madaraka ya kikatiba ya kulivunja Bunge katika hali kama hiyo.

Baraza la Mawaziri ambalo mwenyekiti wake ni Rais, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ndilo huwajibika kupeleka bajeti mbele ya Bunge kwa ajili ya kupitishwa. Mawaziri wengine pia huwajibika kupeleka bajeti za wizara, idara na wakala wa Serikali kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge. Baraza la mawaziri linawajibika kuitetea bajeti na kuhakikisha kuwa inapitishwa na Bunge.

Bajeti ni mpango ama mkataba wa namna Serikali itakavyokusanya na kutumia pesa za wananchi. Unaelezea namna fedha zitakavyokusanywa kutoka kwa wananchi na namna zitakavyogawanywa katika ngazi mbalimbali na idara za Serikali na kwa kuzingatia vipaumbele mbalimbali.

Nchini Tanzania, mwaka wa fedha huanza Julai mosi hadi 30 Juni ya mwaka unaofuatia. Mwaka huu hutajwa kwa kuanzia mwaka ulipoanzia na mwaka ulipoishia. Kwa mfano, mwaka wa fedha ulioanza Julai 1, 2017 na kuisha Juni 30, 2018 hutajwa kama “Mwaka wa Fedha 2017/18.”

Mchakato wa bajeti unasimamiwa na sheria kadhaa, ikiwa ni pamoja katiba, Sheria ya Fedha za Umma, 2001 (kama ilivyo rekebishwa), Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, 1982 (kama ilivyo rekebishwa), na sheria nyingine kadhaa za kodi.

Ikumbukwe kuwa bajeti ya safari hii ilitawaliwa na kilio kikubwa kuhusu mabadiliko ya sheria ambayo yanataka ushuru wote wa mauzo ya korosha nje ya nchi, uingizwe kwenye mfuko mkuu wa Serikali ambayo ndiyo itakayopanga matumizi ya fedha hizo.

Kilio hicho kutoka wabunge wa CCM na upinzani kilitishia kukwamishwa kwa bajeti kutokana na wabunge kuhofia kuwa matumizi ya fedha hizo hayatafanywa kama ilivyokusudiwa, hasa baada ya kuona Serikali imeshindwa kutoa zaidi ya Sh70 bilioni kwa mwaka unaoisha.

Wasiwasi huo wa wabunge, ndio uliotaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango awape majibu ya kuwatoa wasiwasi kuhusu jinsi walivyoweka utaratibu mzuri utakaowezesha fedha hizo kurudi kusaidia maendeleo ya zao la korosho.

Lakini kukosekana kwa majibu hayo kunaweza ndio kulifanya hali ya wasiwasi kuwa wabunge wasingepitisha bajeti hiyo, izidi na hivyo Spika kulazimika kutoa angalizo au onyo kwa wabunge kuwa waangalie vizuri upigaji kura wao.

Swali kubwa ambalo limeanza kuzua mijadala ni kauli ya Spika Ndugai kusema kitu kilicho dhahiri kwamba alilenga kukumbusha wabunge athari za kutopitisha bajeti au alitaka kuwaambia ni lazima waipitishe au aliwatisha?

Na kama ilikuwa ni kuwakumbusha, alilazimika pia kusema kuwa baadhi ya wabunge wanaweza wasirudi bungeni iwapo Bunge litavunjwa? Pengine kauli hizi mbili za Ndugai zinafikirisha kuwa kuna kitu hakiko sawa katika Katiba na hivyo inabidi kifanyiwe kazi.

Mtangazaji mmoja wa redio maarufu, alisema leo asubuhi kuwa “hayo ndiyo mambo ambayo yalifaa kuangaliwa katika marekebisho ya Katiba”.

 

 

Columnist: mwananchi.co.tz