Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa nini wanafunzi washangilie mwalimu asipofika darasani?

10651 Kwanini+pic TanzaniaWeb

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uhusiano ya mwalimu na mwanafunzi ni jambo la msingi katika mchakato wa kufundisha na kujifunza. Panapokosekana uhusiano mzuri, tendo la ujifunzaji huwa katika hatihati.

Wanafunzi wanapaswa kuwaheshimu walimu wakati wote na walimu pia hawapaswi kuwavunjia heshima wanafunzi wao katika mazingira yoyote yale; hupaswa kutunza utu wao, hata kama watakuwa wamekosewa.

Mara kadhaa wanafunzi shuleni hutokea kushangilia na kuwa na furaha na amani pale wanaposikia kipindi kinachofuata ni cha mwalimu fulani wanayemkubali.

Wakati huo huo pia imetokea wanafunzi kuchukia na kutamani kuondoka katika kipindi cha mwalimu mwingine. Hata hivyo, wakati mwingine wanafunzi hufurahi zaidi pale wanaposikia mwalimu wa somo fulani hatofika darasani.

Hili ni jambo la kushangaza lakini linatulazimsha kujihoji ni kwa nini wanafunzi hao wafikie hatua hiyo? Sababu zipo nyingi, baadhi ni hizi zifuatazo:

Ualimu ni zaidi ya kusimama mbele

Mwalimu ni zaidi ya kusimama mbele na kufundisha. Walimu wamekuwa wakitekeleza majukumu mengi wakiwa shuleni na darasani.

Mathalani, walimu wamekuwa wakifundisha na kuna wakati huvaa kofia ya kazi ya mzazi au mlezi, hakimu au mwanasheria, mshauri na mnasihi, mtu wa mfano (kioo cha jamii) kwa anayosema na kutenda, askari, mtafiti, msanii, mbunifu, mtu asiyekata tamaa na nafasi nyingine nyingi.

Mfano kutoka chekechea

Watoto wadogo hujifunza mambo mengi kwa vitendo. Kucheza ni kazi ya watoto na walimu wanapotumia mbinu za ufundishaji zinazoruhusu vitendo vingi, wanafunzi hufurahia somo, shule na kumpenda mwalimu wao.

Vitendo hivyo vya ujifunzaji hupaswa kuzingatia umri na uwepo wa makundi maalum darasani. Hivyo, shughuli za kujifunza kupitia michezo zinapaswa kuwa jumuishi.

Mwalimu anayependa kazi yake huheshimiwa na kupendwa na wanafunzi, kwa sababu amekuwapo wa ajili yao. Kinyume na hapo wanafunzi watachukia somo na mwalimu pia.

Mfano kutoka shule ya msingi na sekondari

Mabadiliko ya ukuaji wa kimwili, kiakili na kitabia kwa wanafunzi hutokea kwa kiwango kikubwa katika hatua za elimu ya msingi na sekondari.

Hivyo ni wajibu wa walimu kukumbuka hilo na hivyo kuwasaidia wanafunzi kisaikolojia kukabiliana nayo.

Mfano kutoka vyuoni

Wapo wakufunzi na wahadhiri wa kariba tofauti; wengine, hupenda kuchochea, kukuza staha na moyo wa kujiamini wa wanafunzi wao.

Pia, wapo wengine ambao hupenda mara zote kutengeneza hofu kwa wanafunzi wao kwa “kuwadogesha” yaani, kuwaondolea wanafunzi wao staha na moyo wa kujiamini.

Walimu ambao mara zote huwajengea hofu wanafunzi wao ni nadra sana kupendwa na wanafunzi. Siyo rahisi, wanafunzi kumpenda mwalimu ambaye kila anapoingia anatoa vitisho ikiwamo kauli za kuwafelisha.

Kwa mfano, ni jambo la kawaida kwa wanafunzi wa elimu ya juu kupewa kazi binafsi au za kundi za kutafuta suluhu ya maswali. Wakati mwingine hutakiwa majibu yao kuyawasilisha mbele ya darasa ama mmoja mmoja au kama kikundi.

Wapo walimu ambao huwakatisha tamaa wanafunzi wao kwa maneno ya dharau na yanayowadhihaki na kuwashusha wanafunzi kujiamini.

Ni kweli wakati mwingine wanafunzi wanaudhi, lakini wakati mwingine walicholishwa katika ngazi za elimu walizopita huweza kuonekana katika ngazi hii ya juu.

Wanafunzi katika ngazi hii ya elimu ya juu wamepita katika mikono ya walimu wengi kabla. Wapo ambao waliharibiwa na walimu, mazingira na mifumo ya elimu ya sehemu walizotoka.

Pia, wapo ambao walinufaika na walimu wao wa zamani na mifumo ya mazingira na elimu. Makundi hayo ya wanafunzi hukutana vyuoni, hivyo kusababisha changamoto kubwa na umakini katika kuyahudumia ambayo kimsingi huwa hayafanani kati ya mwaka na mwaka.

Wapo walimu katika ngazi hii, ambao hukosa kuona jema lolote kwa wanafunzi wao licha ya kupaswa kukumbuka kuwa wanapowafelisha kwa sababu mbalimbali, nao pia hufeli hata kama wengine husema kuwa mishahara yao haibadiliki wanafunzi wakifeli.

Wapo walimu ambao hutumia njia ya maswali binafsi au ya makundi kila wanapofika darasani. Walimu wa aina hii wengi huchukiwa na wanafunzi.

Hupendwa pale tu wanafunzi hao wanapovuka kiunzi cha darasa hilo husika na kugundua umuhimu wa walimu hao katika kuwajenga uwezo wa kujitafutia maarifa.

Umahiri wa mwalimu katika somo

Umahiri wa mwalimu katika kufundisha somo ni chachu ya uhusiano bora. Hata hivyo, uelewa mdogo wa wanafunzi wa kwa nini wanajifunza, huweza kusababisha mgongano katika ushirikiano.

Hivyo ni wajibu wa mwalimu kufanya tathmini binafsi awapo darasani au shuleni ili kugundua kama ana upungufu wa kiutendaji anaopaswa kuuboresha ili wanafunzi wasifurahie anapokosekana darasani.

Pia, wasimamizi wa udhibiti ubora wa elimu katika ngazi ya shule, vyuo, kata, wilaya, mkoa na hata taifa, hawana budi kuwa na mfumo wa kupata mrejesho wa nini kinaendelea darasani kuhusu ufundishaji na ujifunzaji.

Wazazi na walezi nao watimize majukumu yao kwa taifa kwa kuwa karibu na watoto na vijana ili kuwatia moyo, kushauri na kuwasaidia kukabiliana na changamoto na misongo ya mchakamchaka wa shule.

Columnist: mwananchi.co.tz