Sat, 25 Aug 2018
Chanzo: mwananchi.co.tz
Ni kwa sababu ni makosa kisheria na itakuwa kumuumiza Bobi Wine kuwa na kesi moja katika mahakama mbili tofauti kwa hoja zilezile
Kampala, Uganda. Mahakama Kuu ya Kijeshi, katika hali ya mshangao Alhamisi ilimfutia shtaka la umiliki wa silaha Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine, lakini baadaye ilionekana kutekeleza maagizo kutoka mamlaka nyingine serikalini.Majira ya saa 4:30 asubuhi Mahakama Kuu ya Kijeshi ilifanya kikao chake makao makuu ya Divisheni ya 4 mjini Gulu kusikiliza kesi ya Bobi Wine anayeshtakiwa kwa kosa la umiliki haramu wa silaha na risasi.
Hata hivyo, wakati mwenyekiti wa mahakama Luteni Jenerali Andrew Gutti, akiwa tayari kwa ajili ya mchakato wa kesi hiyo, mwendesha mashtaka wa kijeshi Meja Raphael Mugisha alidondosha bomu. Alisema kwamba Jamhuri imemwondolea mashtaka ya umiliki haramu wa silaha na risasi Bobi Wine.
“Nimepokea maagizo kwamba mchakato unaoendelea mbele ya mahakama hii, chini ya Kanuni ya 65 ya Mwenendo katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), usitishwe na mshtakiwa (Bobi Wine) akabidhiwe polisi,” alisema Meja Mugisha.
Alikuwa akiwasilisha maelekezo kutoka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Jaji Mike Chibita.
Katika maagizo hayo, Chibita aliiambia mahakama ya kijeshi kwamba ilikuwa busara kuondoa shtaka la umiliki wa silaha dhidi ya Bobi Wine kwa sababu atakuwa anakabiliwa na shtaka la uhaini katika mahakama nyingine lakini ikiwa na maelezo kama hayo. Chibita alisema itakuwa kumuumiza Bobi Wine kumshtaki sehemu tofauti katika mahakama ya kijeshi na mahakama ya kiraia kwa mashtaka yenye hoja hiyo hiyo.
“...Tafadhali fikiria kumwachia Mheshimiwa Ssentamu ili akabiliwe na kesi katika Mahakama Kuu badala ya Mahakama Kuu ya Kijeshi,” Jaji Chibita alisema katika barua yake kwenda jeshini.
Hata hivyo, mwanasheria wa Bobi Wine, Medard Sseggona alipinga pendekezo la kumkabidhi polisi kwa shtaka la uhaini.
“Mara tu mtu anapoondolewa mashtaka yanayomkabili, anakuwa huru. Bwana yule aliyekaa mbele yenu alikamatwa na jeshi, akapigwa na haki zake zikakiukwa. Mwendesha mashtaka anataka kutumia jukwaa hili kusafisha ukiukwaji wa haki nyingine kwa kukuomba wewe umkabidhi kwa polisi. Hakuna rekodi katika mahakama hii kwamba Mheshimiwa Kyagulanyi anahitajika polisi,” alisema Sseggona.
Aliongeza: “Ombi letu ni kutaka kumwona Mheshimiwa Kyagulanyi akitangazwa kuwa mtu huru na tumpeleke kupata matibabu. Mheshimiwa Kyagulanyi ni Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, si mkimbizi na ana anwani maalumu anakopatikana.
Hata hivyo, polisi walimng’ang’ania wakaondoka naye na atafikishwa kortini Agosti 30.
Columnist: mwananchi.co.tz