Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa hiyo Cecafa ndio mmemaliza mambo yenu!

17756 Ibra+Bakari TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Makocha wa timu za taifa za mataifa mbalimbali hasa Afrika Magharibi huwa hawana kazi sana ya kuhangaika na wachezaji wa timu za taifa.

Mfano, makocha wa Senegal, Ivory Coast, Nigeria, Ghana, Mali, Algeria, Morocco unadhani hawa wana kazi ya kusaka wachezaji? Jibu rahisi, hakuna.

Cecafa haioni fahari kwa timu zake!

Baraza la vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Cecafa ni chombo cha juu cha kusimamia soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lakini haionyeshi kama kweli ina dhamira ya kuendeleza mchezo huo, kikanda.

Cecafa ninaweza kusema ni kama imejifia kwani wakimaliza eneo moja, basi miguu juu wanasubiri mwakani.

Niliwahi kuandika kuwa Cecafa haina mipango endelevu katika soka, haina mkakati wowote kusaidia mataifa yake wala kuyapa mbinu.

Inachojua Cecafa ni kuandaa mashindano ya Chalenji kwa timu za wakubwa, michuano ya vijana na ile ya wanawake na baada ya hapo inakuwa kazi imemalizika.

Pamoja na kazi nzuri iliyofanya ya kuendesha mashindano ya vijana, Cecafa kwa kipindi kirefu haikuwahi kuwatafutia wanachama wake kozi za juu ama hata za chini, hakuna kwa makocha, wakurugenzi wa maendeleo ya soka, madaktari wa michezo, viongozi wa vyama na mashirikisho wala waamuzi.

Hakuna huo mkakati, na inafika hatua Cecafa haina hata uhakika wa mashindano yake pindi mashindano ya kwanza yanapomalizika.

Kinachoshangaza ni kwamba, inafika hatua Cecafa haijui nani anafuata kuwa mwenyeji na pia haijui hata fedha za kuendesha mashindano yanayofuata na inachofanya ni kuishia kuahirisha mashindano kila mara.

Pamoja na matatizo ya kiuchumi kwa mataifa husika, lakini ikiamua mbona mashindano yanafanyika japokuwa kimkandamkanda? Basi mambo yaende hivyo.

Kikubwa ninachotaka kuzungumzia hapa ni Cecafa kuandaa utaratibu mpya wa mashindano kwamba kuwepo na mchanganyiko wa klabu mfano timu zake za Ligi ya Mabingwa na zile za Kombe la Shirikisho zikapambanishwa pamoja ili kuzipa mazoezi kabla ya michuano hiyo.

Kwa sasa kila mahali mfumo wa uendeshaji mashindano umebadilika, UEFA, Asia, CAF na ukiangalia Cosafa lakini angalia Cecafa, mambo ni yaleyale. Cecafa inafanya mambo yake kwa mazoea, hawana hata ubunifu, hawaangalii kinachotakiwa kufanyika walau kuinua soka Afrika Mashariki na Kati na kwa wakati gani.

Cecafa ingeandaa kongamano ambalo lingekutanisha na makocha, manahodha, mameneja kwa klabu zote zilizofuzu na kutengeneza mkakati maalum kwa ajili ya ukanda wa Cecafa.

Kuwapa morari, kuwapa hadidu rejea kwanini Cecafa imewaita na hata kuahidi zawadi nono kwa timu itakayofika mbali kama ilivyo sasa kwa Rayon Sport, lakini Cecafa imebakia kusubiri Chalenji na Kombe la Kagame na michuano ya vijana, basi.

Ilitakiwa Cecafa kuzishika mkono timu zake kwa njia moja ama nyingine, lakini hakuna hicho kitu.

Ni mpango mkakati wa ubunifu pekee ndio utakaosaidia timu kusonga mbele.

Kingine ninachoweza kusema ni kama tatizo lingine kwa Cecafa kwamba haina Kamati ya Masoko, haina Kamati ya Mipango na Uchumi na kama wangekuwepo hayo yote yangefanyika na kuleta msisimko katika ukanda wa Cecafa na timu zake za Afrika.

Columnist: mwananchi.co.tz