Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kutoka hofu ya kukwama hadi bajeti kupita kwa kishindo

10464 BAJETI+PIC TanzaniaWeb

Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki hii wabunge wamepitisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 kwa kishindo. Kura 266 kati ya 348 zilizopigwa (asilimia 76) zilikubali bajeti hiyo ya Sh32.45 trilioni ipite, na kuacha mjadala mzito.

Maswali mengi yameibuka katika suala hilo kutokana hofu iliyokuwapo kuhusu uwezekano wa bajeti kukwamishwa, ambayo ilijengwa juu ya hoja zilizoibuka wakati wa mjadala.

Wabunge wengi walikuwa wakali kama pilipili wakati wa mjadala. Waliibua hoja nzito zilizosababisha mgawanyiko mkubwa baina yao, lakini mwisho wa siku kwa pamoja walipitisha bila kikwazo.

Hoja zilizoibuka

Wabunge hao walisimama kidete katika hoja kadhaa, kubwa ikiwa ni mabilioni ya wakulima yanayotokana na asilimia 65 za ushuru wa mauzo ya nje ya korosho na mabadiliko ya sheria kuhusu ushuru huo.

Kutokana na mjadala mkali kuhusu suala hilo, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM aliwaonya wabunge wa chama hicho kutokana na msimamo wao ndani ya Bunge.

Pengine hilo lilikuwa dogo, kabla hata ya bajeti hiyo kupigiwa kura, Spika Job Ndugai aliwatahadharisha wabunge endapo wangeipigia kura ya hapana, akisema Rais angelivunja Bunge haraka warudi kwenye uchaguzi.

Kwa mujibu wa Ndugai, wakirudi kwenye uchaguzi baadhi yao hawatarudi bungeni.

Pengine tahadhari hiyo, licha ya kwamba ni utaratibu wa kikatiba, ndiyo ilichangia wabunge hao licha ya kutoa kasoro nyingi bado waliipitisha kwa kishindo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mfumo uliopo kikatiba ndiyo hasa chanzo cha wabunge hao kushindwa kusimamia kile wanachokiamini kwa kuhofia kupoteza ubunge wao.

Wakati Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Dk Gibson Sanga akisema kuwa mambo mengi yanayopelekwa bungeni kwa kiasi kikubwa yanakuwa yameshaamuliwa, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema wanasiasa wanakosa msimamo katika masuala ya msingi.

Wasomi, wanaharakati wazungumza

Akizungumzia ni jinsi gani tunavyoweza kutoka katika mfumo wa sasa, Henga anasema ni lazima ifike mahali wanasiasa wawe na msimamo.

“Ifike mahali wanasiasa waache unafiki, wajadili maendeleo yetu bila kuangalia maslahi yao. Sasa siasa imekuwa kubwa kiasi kwamba mwakilishi anaogopa chama chake na anahakikisha analinda maslahi yake badala ya kutetea wananchi waliomchagua,” anasisitiza Henga.

Henga ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Hellen Kijo-Bisimba aliyestaafu, anasema anasikitishwa na mfumo uliopo ambao hautoi fursa kwa mbunge kusimamia hoja anayoiamini.

“Mfano issue (suala) ya korosho, wote tumeshuhudia jinsi wabunge akiwamo Nape Nnauye, Hawa Ghasia na wengine walivyojaribu kuleta hoja za msingi, lakini cha kushangaza baada ya kuzungumzia mapungufu yote mwisho wa siku wanaunga mkono hoja kwa asilimia 100, huu ni unafiki uliopitiliza,” anasisitiza Henga.

“Kwanini sasa wanakosoa kisha mwisho wa hoja wanaunga mkono? Hii ni sawa na kumwambia mtu nguo yako haijakukaa vizuri lakini umependeza,” anaongeza.

Kutokana na hali hiyo, mwanaharakati huyo anawataka wawakilishi hao kuzungumzia zaidi masuala ya maendeleo kwa mujibu wa kazi waliyotumwa na kuachana na tofauti zao za kiitikadi.

Kwa upande wake, Sanga anasema anachokiona yeye ni jinsi Serikali inavyoamua kupitisha jambo wakati ilishaliamua yenyewe

“Tusidanganyane, hizi bajeti zinaandaliwa na Serikali na zinapoletwa bungeni tayari nusu na robo ya maamuzi yake yanakuwa yameshaamuliwa, hivyo wanakamilisha tu taratibu,” anasisitiza.

Sanga anasema jambo lingine linalosababisha hali hiyo kuendelea ni wingi wa wabunge kutoka upande wa chama tawala, unaotoa faida kwa kuwezesha kupitisha chochote hata kama hakina manufaa kwa wananchi.

“Kuna hatari sana Serikali inapaswa kuwa makini na kufanyia kazi hoja zinazotolewa, wasitumie wingi huo na kudharau hoja zinazokinzana nao,” anaongeza mhadhiri huyo.

Mhadhiri huyo anasema kinachopaswa kufanyika sasa ni kuondoa mfumo uliopo hasa wa upigaji wa kura, kwani hauna manufaa tena.

“Katika ulimwengu tulionao sasa, huu mfumo wa kupiga kura za ama za ndiyo au hapana hauko angavu tena, umepitwa na wakati.

“Lakini, pia ni wakati wa Serikali kujishusha na kupokea ukosoaji wowote kabla ya utekelezaji chanya, kwa kuwa mwisho wa siku atakayepata sifa au fedheha ni yenyewe na si mtu mmojammoja,” anasisitiza

Kwa upende wake, waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya nne Njelu Kasaka anasema kinachosababisha hayo yote ni mfumo uliopo kwani licha ya kuwa katika vyama vingi, ukweli ni kwamba bado Bunge halina tofauti na mfumo wa chama kimoja.

“Sasa hivi wabunge wa chama tawala ni wengi, hivyo hakuna tofauti na mfumo wa vyama vingi kwani hata wapinzani wote wakipiga kura ya hapana haisaidii kitu. Tumeshuhudia juzi wapinzani licha ya kupinga bajeti bado ilipita kutokana na wingi wa wabunge wa chama tawala,” anasisitiza.

Anasema hilo linaweza kubadilika tu iwapo wananchi wataamua kutambua umuhimu wa mfumo imara wa vyama vingi, yaani kutoa fursa wa wabunge nusu kwa nusu kutoka kila upande.

“Endapo tutaendelea na mfumo huu wa chama kimoja tusitegemee kubadilika chochote kwa lugha nyingine chama kinapokuwa na wabunge wengi endapo wamepatikana kihalali, basi hiyo ni sauti ya wananchi lakini tatizo katika nchi zetu chaguzi hazitendi kwa haki,” anaongeza.

“Kama wataendelea kuchagua hivi wasilalamike, maana watakuwa wamechagua kuwa na mfumo huu. Wao ndio wana nguvu ya kubadili mfumo huu uliopo na si vinginevyo,” anasisitiza.

Kasaka anasema jambo jingine linalofanya mfumo huo uote mizizi ni suala zima la chama kuwa na nguvu dhidi ya wanachama wake.

“Baadhi ya nchi hawafukuzi mwanachama kwa sababu tu ametofautiana mawazo na msimamo wa chama; hapa kwetu hali ni tofauti chama kina mdhibiti mwanachama wake mpaka katika maisha yake ya kawaida unategemea hapo kutakuwa na kupingana mawazo kweli?” alihoji Kasaka.

Kasaka anasema kutokana na hali hiyo wabunge wamekuwa waoga na kuhofia kufukuzwa pindi watakapoonyesha msimamo wao.

Vilevile, mwanasiasa huyo mkongwe anasema hata nguvu ya kisheria aliyopewa Rais kuvunja Bunge inawafanya wabunge wengi wahofie kurudi tena katika uchaguzi kutokana na uwezekano wa kupoteza majimbo yao.

Anasema ili kukabiliana na hilo Tanzania haina budi kukubaliana na mfumo wa kuwa na mgombea binafsi ambaye ataweza kujinadi bila kupitia katika chama.

“Sasa wanaogopa kuonyesha msimamo wao katika hoja za msingi kwa kuhofia Bunge kuvunjwa na chama kinaweza kisikupe hata nafasi ya kujinadi tena kwa wananchi na ukaishia kukatwa katika hatua za awali.”

Jinsi ilivyokuwa

Wakichangia mjadala wa bajeti wabunge wa CCM, baadhi ya wabunge, wakiwamo Nape Nnauye (Mtama) na Ghasia (Mtwara Vijijini) walisema kinachofanywa na Serikali kinakwenda kukiua chama hicho katika mikoa ya kusini.

Wabunge hao waliowahi kuwa mawaziri walisema wako tayari kudhalilishwa na wabunge wenzao waliopangwa kuitetea Serikali katika sakata la korosho.

Nape alisema korosho kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani na mingine 17 iliyoongezeka kulima zao hilo ni maisha ya wananchi.

Alisema kama wakulima wa pamba wakizungumzia zao hilo wanazungumza maisha, wao hawana mifugo wala almasi.

“Wanaosema si hela zetu, hiki kiatu hamvai ninyi, tunakivaa siye,” alisema Nape.

Ghasia anasema: “Mimi utafiti wangu wa shahada ya kwanza na ya pili unahusu korosho. Leo mtu anakuja humu anaijua korosho na ninasema kila mtu atetee lake na wananchi mjiandae kuwasikia.

“Tudhalilisheni, tuchambeni ila bado tutaisema korosho. Mimi nilikaa upande wa kutetea gesi lakini nilichomewa moto nyumba, mikorosho ya baba yangu ilikatwa, mabomba ya maji yaling’olewa na katika hili nilimpoteza baba yangu, siko tayari kuchomewa moto, siko tayari.

“Wale wenye nia njema waendelee kuwa na nia njema na wale wenye nia ovu wadhihirishe hapahapa duniani.”

Upinzani wakataa bajeti

Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ukiacha kundi la CUF linalomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, walipiga kura za hapana. Kambi hiyo imeeleza kilichosababisha kuikataa bajeti hiyo kuwa ni mwenendo wa Serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.

Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde aliyeambatana na Abdallah Mtolea, ambaye ni kaimu kiongozi wa Upinzani Bungeni walisema wamepiga kura ya hapana kwa sababu Serikali haisikilizi wabunge wake.

Wanatolewa mfano fedha za kisheria kama za korosho serikali inakwenda kuzifuta. Sheria ya fedha inakwenda kufuta Tume ya Mipango na kulifanya Taifa lisilo na Tume ya Mipango.

“Hii ni sawa na basi linalotembea mwendo kasi bila breki, mwisho litakwenda kuanguka. Sasa fikiria hatuwezi kupigia kura bajeti inayokwenda kufuta mipango ya nchi na kuanzisha mipango ambayo haipo katika bajeti.”

“Miradi ya maendeleo ya wananchi hakuna, fedha zilizotolewa katika afya na shule. Halmashauri zinahangaika,” alisema.

Mbunge huyo anasema wanataka wananchi waelewe uamuzi wao haumaanishi kuwa upinzani hautaki maendeleo ya wananchi, bali unataka bajeti itakayokuwa shirikishi kwa wakulima na wavuvi.

Columnist: mwananchi.co.tz