Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kusajili jina la biashara kwa mujibu wa sheria

9797 Justine+Kaleb TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Usajili wa jina la biashara unafanyika chini ya Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, sura namba 213 ya mwaka 2002.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kila mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 18 ambaye ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au mtu yeyote ambaye anaishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali, ana haki ya kusajili jina la biashara ili kumuwezesha kufanya biashara yake kwa ufanisi zaidi na ambayo itakuwa inatambulika kisheria. Kimsingi, biashara isiyosajiliwa haitambuliki na haina uwezo wa kujisimamia kisheria.

Kuna aina mbili za usajili wa majina ya biashara. Aina ya kwanza ni usajili wa biashara ya ubia (partnership/firm). Hii ni aina ya biashara inayojumuisha watu, kikundi au taasisi zaidi ya moja zenye malengo ya kibiashara yanayofanana kwa ajili ya kufanya biashara walioikusudia. Aina ya pili ni usajili wa biashara binafsi (sole proprietor). Hii ni biashara inayohusisha mtu mmoja pekee, kama muhusika mkuu katika biashara hiyo. Atahusika na kila kitu kinachohusiana na uwajibikaji katika biashara hiyo ikiwamo utaratibu wa kibenki. Mchakato wa usajili wa jina la biashara unaanza na muhusika au wahusika kwanza kufahamu mambo ya msingi na kama wanataka biashara yao itambulike kwa jina gani. Kumbuka kwamba jina ambalo litasajiliwa ni lile ambalo halifanani na jina lingine lililokwisha sajiliwa na halipaswi kuwa miongoni mwa majina yasiyoruhusiwa kusajiliwa. Majina yasiyoruhusiwa kusajiliwa ni pamoja na ya taasisi za serikali, ya watu binafsi, ya mahali nk. Jambo la msingi katika jina ni kuwa mbunifu kama sifa ya mjasiriamali ilivyo. Hupaswi kuiga kila kitu. Kaa chini ubuni jina la kipekee lenye mvuto na litakalokutofautisha na watu wengine. Kumbuka kwamba ni muhimu kuwa na majina mbadala angalau matatu ili kama jina ulilolipendekeza halitakubaliwa, uweze kutumia majina mengine mbadala ya kuendeleza mchakato wa usajili. Pamoja na jina, ni muhimu mkafahamu fika kwamba biashara yenu mnataka ifanye nini, mnataka kujishughulisha na nini, mtatoa huduma gani au mtauza bidhaa gani.

Taarifa nyingine zitakazohitajika katika mchakato wa usajili wa jina la biashara ni pamoja na anwani ya posta ya biashara, barua pepe, namba ya simu, anwani ya makazi ya biashara na biashara yenyewe. Taarifa za wahusika zitakazohitajika ni pamoja na majina matatu, namba za simu, tarehe za kuzaliwa, namba za nyumba, namba ya kitambulisho cha uraia, barua pepe na taarifa nyinginezo.

Kumbuka kwamba usajili wa jina la biashara unafanyika kwa njia ya mtandao, mhusika utapaswa kuingia katika mtandao wa Brela na kuanza mchakato wa usajili baada ya kujisajili wewe mwenyewe na kisha kuruhusiwa kuanza kusajili jina la biashara. Unaweza kuomba ushauri wa kisheria kwa wanasheria ili wakusaidie kufanikisha mchakato huo pasipo vikwazo vyovyote. Hatua ya kwanza ikishakamilika, fomu itatumwa mtandaoni mtakayopaswa kuichapisha, kuisaini na kuituma tena kwenye mtandao.

Baada ya hapo Kisha mtapaswa kulipia mchakato wa usajili kwa njia ya simu au benki. Ikiwa kutakuwa na marekebisho mtapaswa kufanya marekebisho ili usajili uendelee. Ikiwa usajili utakataliwa mtatarifiwa na ikiwa usajili utakubaliwa mtatumiwa nakala ya cheti halisi cha usajili mtandaoni. Cheti cha usajili huwa ni nakala mbili ambazo ni cheti cha usajili (Certificate of incorporation) pamoja na taarifa za rejista (extract from register).

Cheti cha usajili kinakuwa na jina la biashara, uthibitisho wa usajili, tarehe ya usajili, namba ya usajili, saini ya msajili wa Majina ya Biashara na nembo ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Cheti cha taarifa za rejista huwa na jina la biashara, tarehe ya usajili, namba ya usajili, saini ya msajili wa majina ya biashara, majina ya wahusika wa biashara, majina ya wahusika wa akaunti ya biashara, uthibitisho wa malipo ya usajili, namba ya risiti ya serikali iliyolipwa, anwani ya biashara na nembo ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jina la biashara likishasajiliwa linakuwa na nguvu ya kisheria ya kitaasisi. Lina uwezo wa kununua na kuuza, kushitaki na kushitakiwa, kumiliki na kumilikisha mali.

Ikumbukwe kwamba biashara inapowajibika kijinai watakaowajibishwa ni wahusika au washirika wa biashara hiyo au mmiliki na si vinginevyo.

Baada ya usajili ili biashara ianze rasmi ni muhimu kutimiza vigezo vyote vya kukuwezesha kuanza biashara kisheria ikiwamo kuhakikisha kuwa umepata namba ya mlipa kodi (TIN), inayosoma jina la biashara pamoja na cheti cha uthibitisho wa mlipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Nyaraka hizi zitakusaidia kupata leseni ya biashara kutoka halmashauri au wizarani. Kwa biashara ya ubia, ni muhimu kumuona wakili ili awaandalie mkataba wa ubia ambao utaeeza namna mtakavyoshirikiana kibiashara, mtaji, mgawanyo wa faida na hasara pamoja na haki na wajibu wa kila upande.

Hivi vyote vitawasaidia pale mtakapohitaji kufungua akaunti ya biashara. Akaunti ya biashara ni muhimu ikawa na jina lililopo kwenye cheti cha usajili au linalofanana na hilo ili wateja wasiwe na kigugumizi wanapohitaji kufanya malipo.

Kumbuka wateja hawapendi kumlipa mtu binafsi kwa hiyo kuwa na akaunti ya biashara huifanya miamala yenu ya kifedha kuwa salama.

Hata mbuyu ulianza kama mchicha, safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja. Wanaoacha hawajawahi kushinda na washindi huwa hawaachi hata siku moja.

Mjasiriamali wa kweli huwa haogopi gharama wala changamoto, bali hutumia changamoto kama fursa za kumfanya afike mbali zaidi. Faida za kusajili na kuirasimisha biashara yako ni kubwa zaidi kuliko changamoto na gharama utakazolipa. Siku moja biashara yako itakuwa ni miongoni mwa biashara kubwa sana nchini na nje ya nchi. Kama wengine wameweza wewe unashindwaje? Na unasubiri nini kuanza? Sajili leo biashara yako. Chukua hatua inawezekana!

Columnist: mwananchi.co.tz