Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kusahaulika vipaumbele muhimu vya bajeti kijinsia

18809 Tumaini+msowoya TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapotaja neno ‘jinsia’ watu wengi huwa wanadhani ni suala la wanawake. Hata pale wanaharakati au wanasiasa wanapopiga kelele kuhusu upangaji wa bajeti yenye mtizamo wa kijinsia, bado fikra za watu wengi huwa zinawapeleka kwa ‘wanawake’.

Wachambuzi wa masuala ya kijinsia wanasema hakuna maendeleo yanayoweza kufikiwa kama upangaji wa bajeti hautaweza kuzingatia mlengo wa kijinsia, lakini hawamaanishi ‘mtazamo wa wanawake’.

“Hapa tunazungumzia makundi yote muhimu, yaani wanawake, wanaume, watoto, wenye ulemavu, wazee na vijana. Si wanawake peke yao,” anasema Mkuu wa Idara ya Maarifa, tafiti na uchambuzi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Happy Maruchu.

Mwanaharakati huyo wa masuala ya jinsia, anasema: “Ukipanga bajeti bila kujua mahitaji halisi ya makundi hayo, yaani kwa kuzingatia, tofauti za kimajukumu na kimahusiano ya makundi hayo, huwezi fikisha lengo.”

Uelewa mdogo kuhusu bajeti yenye mtazamo wa kijinsia ndiyo unaoilazimisha TGNP kuwakutanisha madiwani wa halmashauri mbalimbali za wilaya, manispaa na majiji nchini ili kuwanoa.

Baada ya kupata ujuzi huo, baadhi ya madiwani wanakiri kuwa walikuwa wanakosa uelewa mzuri kuhusu namna gani bajeti inaweza kuandalia kijinsia.

Wanasema dhana kwamba ‘bajeti inalenga wanawake peke yao’, ndiyo iliyokuwa inaleta ukakasi na kuwafanya wengi wasielewe.

Lakini, wale wanaoelewa kuhusu upangaji wa bajeti kwa mtizamo wa tofauti za makundi kimajukumu wanakiri kuwa imesaidia kuleta maendeleo chanya kwenye wilaya zao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga anasema mipango ya maendeleo kwa nchi nyingi hasa zinazoendelea zinafuata mfumo dume ambao umekuwa ukitumiwa kuweka vipaumbele bila kufuata makundi maalumu, yakiwamo ya watu wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Diwani wa viti maalumu katika Manispaa ya Ilala, Sada Mandwanga anasema ‘bajeti yenye mtizamo wa kijinsia’ ni suala geni kwake, hivyo anahitaji kujifunza zaidi.

“Binafsi ndio najifunza sasa kuhusu hili jambo, zamani nilijua ukisema jinsia basi ni wanawake na wasichana peke yao,” anasema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mwalingo Kisemba baada ya kuanza kuzingatia usawa kijinsia katika uandaaji bajeti, wameweza kutafiti na kujua mahitaji ya msingi ya makundi maalumu na hivyo kuyapa kipaumbele.

“Kwetu shida ilikuwa wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule za sekondari, tukagundua wanaoathirika zaidi ni wasichana. Wakati tunapanga bajeti, tulichukua jambo hilo kwa kipaumbele na tayari, tumejenga mabweni tisa katika shule tisa kati ya 28 zilizopo,” anasema Kisemba.

Maruchu anasema wameamua kuwanoa madiwani ili kuondoa dhana kwamba jinsia ni jambo linalohusu wanawake peke yao, pili, kuona wanao wajibu kushiriki kikamilifu kutafiti, kujua vipaumbele, kupanga na kupitisha bajeti zikiwa na mtizamo kijinsia.

“Bajeti yoyote lazima ianzie ngazi ya chini, tumewaita nyie madiwani kwa sababu mnatoka kwenye kata na mnaweza kufikia mitaa na vijiji. Kaanzieni kule kuandaa bajeti mkitizama haya makundi,” anasema.

Sababu za bajeti kijinsia

Maruchu anasema sababu za kuzingatia jinsia wakati wa kupanga bajeti za serikali ni pamoja na kuyapa makundi maalum fursa ya kupata huduma za afya, elimu na maji.

Ofisa huyo wa TGNP anasema kiuhalisia ni rahisi kupata maendeleo na kufikia uchumi ikiwa bajeti inayotengwa itazingatia makundi hayo.

“Kwa hiyo bajeti yoyote inayopangwa ni lazima iwe na mtizamo wa kijinsia, ianzie ngazi ya chini na nyie madiwani ndio viungo muhimu katika upangaji huo, hata hivyo hatua ambayo Tanzania tumefikia kwa sasa sio mbaya, tumeweza kuanza,” anasema.

Mchambuzi wa masuala ya bajeti, Geofrey Chambua anasema bajeti hiyo ndiyo inayolazimisha waandaaji kufanya tafiti ili kujua mahitaji ya jamii husika kabla ya kupanga vipaumbele.

“Tunapotaja waandaaji madiwani ni watu muhimu, ndio wanaopitisha bajeti kwenye halmashauri na ndio wanajua wananchi wao kwenye kata wana shida gani,” anasisitiza Chambua.

Anasema bajeti yenye mlengo wa kijinsia ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yoyote ile kama wapangaji wataweza kujikita katika hiyo.

“Bajeti hii ndiyo inayotazama maeneo muhimu na namna ya kupanga vipaumbele, madiwani lazima wajue hali halisi ya makundi kwenye kata na ni nini hasa mahitaji yao ya msingi ili waweze kupanga bajeti.

Kuandaa bajeti kijinsia

Chambua anasema hatua ya kwanza ya kuandaa bajeti hiyo ni kwa waandaaji kujua mahitaji ya makundi maalumu yaliyo kwenye maeneo yao. “Ukishajua makundi na mahitaji yao utaangalia nini kipaumbele katika yote uliyojua,” anasema.

Anasema wakati vipaumbele vinapoangaliwa, ni muhimu kuoanisha na bajeti ya kipindi cha nyuma kujua utekelezaji wake hasa kwenye vipaumbele vilivyoibuka ulikuwaje.

“Ni jambo moja kutenga bajeti ya ujenzi wa bweni, lakini ni jambo la pili kujua bweni hilo limesaidia nini? Limepunguza tatizo lililokuwapo? Bajeti inayofuata iweje? Haya ni mambo muhimu mno,” anafafanua.

Wilaya zilizoweza

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo anasema katika utafiti wao walibaini kundi la vijana linahitaji upekee zaidi katika upangaji wa bajeti kutokana wengi kukosa ajira.

“Kwa hiyo tukakubaliana kuhakikisha sio tu kwamba wanapewa mikopo, bajeti watakayotengewa isaidie kuwaandalia mazingira mazuri ya kujikwamua kiuchumi,” anasema.

Anasema kwa kutumia asilimia nne inayotengwa na halmashauri kwa ajili ya vijana, walifanikiwa kutenga bajeti iliyoanza kuzaa matunda.

“Tumekwishatoa mikopo ya Sh160 milioni kwa makundi maalum wakiwemo vijana, tuna uhakika vijana wakiweza kuzalisha uchumi wao watainua maendeleo ya wilaya yetu,” anasema.

Halmashauri ya Morogoro haitofautiani na ile ya Mbeya ambako wanasema baada ya utafiti walibaini wanaweza kumaliza tatizo la mimba shuleni ikiwa yatajenga mabweni kwa ajili ya watoto wa kike.

Anasema walibaini pia wengi wanakatisha masomo kwa kutokana na umbali kutoka nyumbani hadi shule, waliamua kuandaa bajeti ya elimu kuzingatia jinsia.

Nini kifanyike

Akitoa mapendekezo ya nini kifanyike, Dk Sanga anasema jambo la msingi ni kuwajengea uelewa viongozi wa kuchaguliwa kwa sababu ndio wanaopewa rungu la kuongoza vikao vya bajeti.

“Kijijini anayesimama kuongoza kikao ni mwenyekiti wa kijiji, kata ni diwani na halmashauri ni mwanasiasa yuleyule wa kuchaguliwa ndiye kiongozi, bila wao kuelewa bajeti inayotengwa haiwezi kunufaisha makundi yote muhimu,” anasema.

Anasema mafunzo hayo lazima yafanyike kwenye mabaraza ya madiwani na kata ili kila mmoja wao ajue wapi anaweza kuanzia.

“Ukisema jinsia unaweza kupuuzia, lakini ikitokea mama akatumia saa nne kuchota maji kwa sababu ya umbali, sio tu umemuathiri yeye bali maendeleo ya kijiji, kata, wilaya na taifa,” anasisitiza.

Diwani Wa kata ya Kivule, Wilson Mollel anasema kama viongozi wa siasa watakuwa wanajengewa uelewa baada ya kuchagulia na kuanza kuingia vikao vya bajeti wataweza kufikia malengo ya mtizamo huo.

Columnist: mwananchi.co.tz