Uchaguzi wa mwaka 2015 uliomalizika miaka mitatu iliyopita, uliacha historia kwa chama kikuu cha upinzani Chadema kupata idadi ya kura nyingi ambazo hakijawahi kuzipata tangu uchaguzi wa vyama vingi uanze mwaka 1995.
Katika uchaguzi huo, vyama vinane kati ya 11 vilishiriki kinyang’anyoro cha urais. Dk John Magufuli wa CCM aliibuka kidedea kwa kupata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47, akifuatiwa na Edward Lowassa (Chadema) aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97.
Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani alijiunga na chama hicho akitokea CCM kwa madai ya hujuma za kukatwa jina lake katika kikao cha Kamati ya Maadili huku yeye akipinga kwamba hakikutenda haki.
Hata hivyo, Machi Mosi mwaka huu Lowassa akiwa katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM alitangaza kurejea ndani ya chama hicho. Siku chache baadaye Lowassa amesikika akiwa katika mapokezi nyumbani kwake Monduli, akiwataka Watanzania wote waliompigia kura milioni sita kwenye uchaguzi uliopita wazitoe kwa Rais Magufuli kupitia uchaguzi mkuu ujao 2020.
Swali la kujiuliza ni kweli wapiga kura hao watakuwa tayari kukubaliana na ombi la Lowassa? Kuna hatua tatu zinazoweza kuthibitisha mazingira ya mwelekeo wa kura hizo kwa kutumia makundi matatu.
Kura hizo milioni sita, zina kundi la wanachama waliokuwa tayari kumpigia kura mgombea yeyote yule ambaye angepitishwa na Chadema mwaka 2015, hata kama asingekuwa Lowassa.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, makadirio ya wanachama hadi kufikia robo ya mwaka jana ilikuwa ni zaidi ya milioni nne. Kwa ngazi ya chini, chama hicho kimeshafikia asilimia 68 ya vitongoji (misingi) vyote nchini. Kwa hiyo itakuwa ni vigumu sana kwa Lowassa kunasa kura za kundi hili.
Kundi la pili ni wana mabadiliko. Kundi hili halikutengenezwa na Chadema. Chadema ilitumia fursa ya kunasa kundi hili kutokana na kukosekana kwa mbadala. Ni kundi la vijana waliokuwa na hasira dhidi ya Serikali na mfumo uliokuwa ukilalamikiwa kwa miaka mingi. Kundi hili nalitazama katika picha za mafuriko yaliyokuwa yakiandamana na Lowassa kuchukua fomu ya kugombea urais.
Kundi hili litakuwa tayari kumfuata Lowassa aendapo litakuwa limepata majibu sahihi ya maswali yaliyoibuliwa katika kipindi cha uchaguzi mwaka 2015. Madai ya msingi yaliyohusu mabadiliko ya kimfumo wa serikali. Kama Serikali iliyopo madarakani itakuwa imeyajibu basi Lowassa atakapokuwa CCM ajiandae kuwapokea kwa mafuriko.
Kundi la tatu ni lile lisilokuwa na upande wowote. Lililokuwa linaamua kwa kutumia ushawishi na mvuto wa mgombea kwa wakati huo. Kundi hili linaloathiriwa na ushawishi, mkumbo bado halijafikiria hadi sasa litapiga kura upande gani. Mvutano mkali utajitokeza wa kuchukua kundi hili endapo Tundu Lissu (Chadema) atasimamishwa kugombea urais.
Pamoja na picha halisi ya makundi hayo katika kura milioni sita za Lowassa, bado tunahitaji kujiridhisha na nguvu ya Lowassa katika kampeni na matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao mwakani. Je, Lowassa ni mchezaji nyota atakayeongeza thamani katika chaguzi hizo?