Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kukamata wapinzani kila mara kunatung’arisha zaidi - Haonga

38010 Pic+kamata Kukamata wapinzani kila mara kunatung’arisha zaidi - Haonga

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika maisha, kila mtu ana ndoto na maono yake ambayo anajiwekea na anakuwa na shauku kutaka kuyatimiza. Hivi ndivyo ilivyo kwa mwanasiasa kijana, mbunge wa Mbozi mkoani Songwe, Mwalimu Pascal Haonga.

Haonga anasema, “Nina ndoto, siku moja nitakuja kuwa Rais wa Serikali ya Tanzania”.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Haonga anazungumzia mambo mengi kuhusu maisha yake hadi kuingia kwenye harakati za kisiasa kupitia Chadema na kuwa mbunge wa Mbozi baada ya kumuangusha aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Godfrey Zambi wa CCM mwaka 2015.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya ubunge wake, anasema ameweka alama ambayo haiwezi kufutika kutokana na mambo aliyowafanyia wananchi wa jimbo hilo ikiwamo kuchimba visima vya maji, kuweka umeme wa sola kwenye vituo vya afya na zahanati na kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule.

Anasema kukubalika kwake kwa wananchi ni ishara tosha kwamba anatosha kuwa Rais wa Tanzania.

Anasema aliamua kuweka pembeni kazi ya ualimu na kuingia katika siasa na kugombea ubunge mwaka 2015 kwa sababu aliona viongozi waliopewa dhamana na wananchi hawaitendei haki nafasi ya ubunge, hivyo badala ya kuendelea kulalamika pembeni, akaona agombee ubunge ili kuwatumikia wananchi.

“Ninaamini kwamba unapokuwa mwalimu bado ualimu haufi kwani hata baba wa Taifa, Julius Nyerere alikuwa mwalimu lakini baadaye akaja kugombea urais na akawa Rais wa Tanzania.

Kwa hiyo mimi bado ni mwalimu, tofauti ni kwamba awali nilikuwa nafundisha darasani lakini sasa hivi ninafanya kazi ya uwakilishi wa wananchi bungeni, hivyo ninachokifanya sasa siingii darasani kufundisha bali nafanya kazi ya kuchukua matatizo ya wananchi na kuyapeleka bungeni ili yapatiwe majibu na ufumbuzi,” alisema.

Ndoto za kuwa Rais

Haonga anasema kila kiongozi lazima awe na malengo na maono katika maisha, hivyo na yeye ndoto zake si kuishia kwenye ubunge bali ni kuja kuwa Rais wa Tanzania.

Anasema kutokana na mambo aliyoyafanya kwa wananchi wake kwa muda wa miaka mitatu ameacha alama ambayo itakuwa ni kumbukumbu tosha kwa wakazi wa Mbozi.

Ndoto zake, anasema ni kuona anasimamia na kutekeleza kwa vitendo mambo yote muhimu aliyowaahidi wapigakura wa Mbozi.

Anasema Mungu amempigania katika kutekeleza ndoto zake kuwasaidia wananchi kutoka ualimu hadi kwenye ubunge na ndoto zake ni kwamba siku moja ataitwa Rais wa Tanzania.

“Mungu akinijalia huko mbeleni nina ndoto za kuja kuwa Rais wa nchi hii, kwa sababu kiongozi lazima uwe na malengo, lazima uwe na maono na unapoanza kwenye nafasi moja ni lazima upande juu. Sasa kama nimeanza na ualimu kufundisha darasani, nimekuwa mbunge na ndoto zangu huko mbeleni Mungu akinijalia ni kuwa Rais wa Tanzania tu.”

Anasema hakuna aliyejua kwamba Rais John Magufuli angekuwa Rais wa Tanzania kwani hata kwenye kura za maoni za CCM mwaka 2015 waliokuwa wanatajwa ni watu wengine kabisa na wote wakapigwa chini na aliyekuwa hana jina ndiye akawa Rais.

Anasema, “Sasa na mimi nina amini haya ninayofanya yote haya najua huko mbeleni sitakurupuka ni lazima nijipange nifanye kazi vizuri, kazi moja ninapoifanya lazima nitengeneze mazingira huko mbeleni. Na naamini siku moja nitakuja kuwa Rais wa nchi hii”.

Dhahabu kwenye moto

Haonga anasema katika utawala huu upinzani na viongozi wake wanapitia magumu mengi ikiwamo kukamatwa na kufunguliwa kesi katika mahakama mbalimbali nchini lakini hilo kwao ni fursa ya kujijenga kisiasa.

Anasema upinzani unazidi kuimarika zaidi huku wakiungwa mkono na wananchi wengi wapenda haki kwani wanaona yanayotendeka dhidi yao, hivyo anaamini hata kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi uchaguzi mkuu watashinda kwa kishindo.

Anasema yeye ni miongoni mwa viongozi na wabunge wa upinzani waliokumbana na misukosuko ya kukamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani kwa kile anachoamini ni kuwatetea wananchi wake.

Anasema, “Mimi nimekamatwa na kuwekwa mahabusu. Nimefunguliwa kesi, awali nilikamatwa na kuwekwa ndani kwa amri ya mkuu wa mkoa aliyepita (Chiku Galawa) kwa sababu nilikuwa wanatetea wananchi wangu. Mara ya pili nilifunguliwa kesi ya kufanya fujo kwenye uchaguzi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mlowo-Mbozi.

“Lakini nashukuru Mola wananchi tulisimama kidete hadi tuliposhinda mwaka jana, sasa yote hii wasidhani ni njia ya kunidhoofisha bali inanijenga zaidi.”



Columnist: mwananchi.co.tz