Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuingiliana katika madaraka kunaweza kuzusha vurugu

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Binadamu amejaliwa mafunzo makubwa juu ya mgawanyo wa kazi na madaraka hata kabla ya kuja duniani.

Mafunzo yapo mwilini mwake tokea akiwa ndani ya tumbo la mama na hutakiwa kuheshimu mgawanyiko wa hayo mamlaka na madaraka ya viungo na sehemu mbali bali za mwili katika maisha yake yote.

Mgawanyo huu wa madaraka unatokana na mwili wa Bin Adam (mtoto wa Adam) kugawika katika idara na vitengo mbalimbali ambavyo kila kimoja huwa na kazi maalumu ya kumsaidia mtu katika maisha yake.

Ni mara chake utaona baadhi ya viungo vinakaimu nafasi za viungo vingine pale kiungo halisi kinapokuwa “likizo” au kinashindwa kufanya kazi au kutokuwepo kabisa.

Katika mgawanyiko huu mikono hufanya kazi kama ya kula, kulima, kuwinda, kushona, kuendesha chombo, kuandika na kadhalika wakati kazi ya miguu ni kwenda na kwa vijana wengi ni kulisakata kabumbu.

Kazi ya meno ni kutafuna, mdomo kusema, masikio kusikia na macho kuona. Mishipa inasaidia kusafirisha damu, mapafu kupumua, akili kupima jambo na kutoa wazo, uamuzi na kadhalika.

Panapotokea tatizo, furaha au huzuni utaona mtu anajieleza kwa ishara kama ya mikono, kicheko, kilio au kutikisa kichwa.

Inapotokezea hana au amepoteza nguvu za miguu huenda kwa kutumia mikono, kigari au msaada wa fimbo (mkongojo).

Wapo watu wenye ulemavu wanaoandika au kufanya shughuli mbalimbali kwa miguu kutokana na kutokuwa na mikono.

Mafunzo yanayoyapatikana katika mwili tangu mtu anapoumbwa na kutambua matumizi yake akiwa mdogo hutarajiwa kumsaidia katika maisha ya kila siku na kuheshimu mgawanyo wa mamlaka katika maisha.

Mgawanyo katika maisha

Kwa bahati mbaya kuheshimu mgawanyo wa mamlaka na madaraka katika maisha kama ilivyo katika maumbo yetu, silioni kwa baadhi yetu (nadhani na mimi nimo katika kundi hili).

Mwingiliano ya mgawanyo wa majukumu husababisha misuguano na migongano isiyo ya lazima inayoleta maafa, kama ilivyo kwa msuguano wa waya mbili za umeme ambao huzusha mlipuko.

Mara nyingi hapa nchini, Bara na Visiwani nimesikitishwa kuona baadhi ya viongozi wa Serikali wakitumia vibaya madaraka yao kwa kuingilia mamlaka ya mgawanyo wa kazi.

Viongozi hawa hujifanya mabingwa na wataalamu wa kila fani – afya, elimu, uhasibu, sheria, habari, michezo na kadhalika badala ya kuhakikisha kila mtu anawajibika kwa mamlaka aliyonayo.

Hali hii imezidi miongoni mwa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao wamekuwa chanzo cha migongano na vurugu.

Wapo ambao namna wanavyoongoza mikoa na wilaya haitofautiani na sawa na amri ambayo hakuna mwenye haki ya kuhoji au kuuliza, kama inavyokuwa kwenye gwaride la kijeshi.

Viongozi hao hutoa amri za kila aina, zikiwemo zinazokiuka sheria au maadili ya suala wanalotaka kujifanya wana utaalamu nao.

Mwenendo huu unazusha mfarakano katika baadhi ya sehemu na watu kujiuliza kama wanachokiona ndio utawala bora.

Kwa mfano, hivi karibuni nilishtuka kumsikia kiongozi mmoja wilaya ya Kusini Unguja, akiahidi kumchukulia hatua kali dereva wa gari lililopata ajali katika Kijiji cha Muyuni na kusababisha vifo vya watu sita.

Hapa tujiulize huyu kiongozi wa serikali anayo haki gani ya kumuadhibu dereva wa gari, kapata wapi mamlaka hayo na nani amempa.

Hili suala lilikuwa linachunguzwa na Jeshi la Polisi na kutokana na vielelezo vinavyopatikana na kwa idhini ya ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, ndio polisi hupeleka mashitaka mahakamani ili kutolewa uamuzi wa kisheria.

Alichofanya huyu kiongozi wa wilaya na kupewa nafasi kubwa ya kusikika katika vyombo vya habari vya Serikali ya Zanzibar ni kuigilia

mkondo wa sheria usifanye kazi yake na kutoheshimu mgawanyo wa madaraka ya kazi.

Masuala ya utawala na sheria za usalama barabarani ni maneno mawili tafauti na kila eneo lina watu waliopewa mamlaka na madaraka ya kusimamia.

Huu mtindo wa viongozi wanaohusika na utawala kujiingiza kila pahala, kama mafuta, chumvi au sukari katika chakula, unadhoofisha utawala bora na unatoa taswira mbaya.

Yapo mambo, kama ya mkuu wa wilaya na mkoa kuchukua hatua anapoona sheria ziliopo wazi zinakiukwa hayana mjadala.

Kwa mfano, kitendo cha karibuni cha mkuu wa mkoa wa mjini magharibi, kufanya ukaguzi wa baa na kuzifungia zile zinazouza chakula mchana au pombe mwezi wa Ramadhani kinaeleweka.

Hii ni kwa sababu sheria na kanuni za leseni ya biashara ya kuuza pombe Zanzibar ipo wazi juu ya saa za kufanya kazi na kuzuia biashara ya pombe wakati huo.

Kwa maana hiyo ni wazi yeyote ambaye hayupo tayari kutouza pombe wakati wa Ramadhani atafute biashara nyingine ya kufanya.

Kama mkuu wa mkoa baada ya kuzifunga baa angejifanya hakimu na kuwapeleka gerezani wenye baa kutumikia vifungo angekuwa anajipa madaraka asiyokuwa nayo.

Hata huu mtindo wa kuwaweka watu kizuizini kama adhabu hauna sura wala harufu nzuri ya utawala bora. Sheria zipo na anayekosa zimtie adabu na sio kauli ya mkubwa kuwa ndio adabu. Hii sheria ya kuwekana kizuizini ni chafu na ilifurahisha kuona kwamba aliyeileta Tanzania, kuisimamia na kuitetea ipitishwe na Bunge ndiye wa kwanza kumbana.

Columnist: mwananchi.co.tz