Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Klabu inayofanya usajili mbovu, mafanikio ni ndoto

10370 Goshashi+allan TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kipindi cha usajili kimemalizika. Zilianza tetesi za usajili, tukasikia mchezaji fulani anatakiwa na klabu fulani, mchezaji fulani anaachwa na klabu fulani, wachezaji fulani mikataba yao imekwisha yaani kilikuwa ni kipindi cha wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya wachezaji na pia ni kipindi kizuri kwa baadhi ya wachezaji.

Kipindi cha usajili ni kipindi cha mshtuko kwa wachezaji na mashabiki, kwani wachezaji huachwa kweli, wengine huachwa kiholela kwa chuki, hila, fitina na siyo kuangalia umuhimu wa mchezaji au kiwango chake na mara nyingi uamuzi huo haufanywi na kocha ila viongozi wa klabu.

Kwa mujibu wa kanuni ya 61 ya Kanuni za Ligi Kuu ya Tanzania kipengele cha tano, kocha wa timu ndiye mkuu wa shughuli zote za timu kuanzia usajili wa wachezaji, uandaaji wa timu, usimamiaji wa timu katika mashindano na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Hata hivyo hapa nchini huwa ni kinyume chake kwa sababu viongozi huamua kuacha wachezaji na hutafuta wachezaji wa kusajili bila kumshirikisha kocha.

Pia, katika kipindi hiki cha masuala ya usajili, wapo wachezaji ambao hupelekwa kwa mkopo katika klabu nyingine bila mchezaji kushirikishwa huku klabu zikidai mchezaji hana uwezo wa kuhoji endapo atatakiwa kuhamishwa kwa mkopo kwenda klabu nyingine.

Kikimalizika kipindi cha usajili yaani wachezaji kuhamishwa kinakuja kipindi cha kupitia majina na kutangaza pingamizi, hapa ndipo huibuka suala la mchezaji fulani kasajiliwa mara mbili kwa sababu viongozi wa klabu zetu bado wamekuwa wakizuia maendeleo ya wachezaji badala ya kuwauza kwa klabu zinazowataka. Na baada ya hapo hufuata kipindi cha kuthibitisha usajili.

Kwa mtazamo wangu, kama kuna wakati muhimu klabu hazipaswi kufanya makosa kuelekea kucheza mashindano yoyote yale ni kipindi cha usajili wa wachezaji.

Umuhimu wa kipindi hiki uko wazi, kwani ndiyo wakati klabu hutumia fedha nyingi kununua wachezaji au kuingia nao mikataba mipya kuliko wakati mwingine wowote.

Ni kipindi cha hekaheka ya wachezaji kuzivuna klabu mamilioni ya fedha kutokana na ada za usajili na kwa upande mwingine ni kipindi cha klabu kuvuna wachezaji wazuri watakaoiletea mafanikio katika Ligi Kuu.

Ni wazi kuwa, klabu iliyowekeza fedha nyingi kwenye kusajili wachezaji wazuri na kuwa na kocha mzuri na uongozi mzuri ndiyo yenye kujenga mwelekeo jirani kupata mafanikio, kuliko klabu iliyokwenda kinyume chake.

Au, kwa maneno mengine, mafanikio ya timu kwenye mashindano yoyote hutegemea zaidi na jinsi ilivyoandaliwa, kwa maana maandalizi mazuri ndiyo kiini cha mafanikio kuliko badala yake.

Hata hivyo, jambo la kushangaza hapa nchini ni kwamba timu zimezoea kusajili kwa mazoea, zimejikuta zikisajili hata wachezaji wasio na viwango, tena wengine ni wachezaji wa kigeni!. Hii ni kwa sababu tu zimemezwa na utumwa wa mazoea ya kusajili. Hilo linatokea kwa sababu viongozi wa klabu wanasajili wachezaji bila kuzingatia mapendekezo ya kocha ambaye ndiye mwenye jukumu kubwa la kufundisha wachezaji hao.

Viongozi wanalazimisha kusajiliwa wachezaji wanaowataka kutokana na mapenzi binafsi, ukaribu, undugu, urafiki au kwa misingi ya rushwa badala ya kumuachia kocha kufanya usajili unaostahili kwa kutumia wang’amuzi wa wachezaji.

Klabu yoyote inayofanya usajili mbovu, mafanikio kwao huwa ni ndoto zisizo na tamati. Kila siku zitaota kufanikiwa bila kufanikiwa. Tusubiri Ligi Kuu ianze tuone kama usajili uliofanyika ulikuwa na faida.

Columnist: mwananchi.co.tz