Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kitabu cha Mengi kichochee uandishi na kutokata tamaa

11167 Mzee+pic.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uandishi wa vitabu ni taaluma ambayo inahitaji maarifa na weledi katika kufikisha ujumbe kwa hadhira. Waandishi wa vitabu popote duniani wanatumia simulizi za kubuni, simulizi zao wenyewe au za watu wengine.

Hata hivyo, simulizi za maisha ya mtu mwenyewe zinakuwa na uhalisia ndani yake kwa sababu anatoa somo juu ya jambo ambalo yeye mwenyewe amepitia. Mtu huyo anaweza kushauri au kufundisha jamii na akaeleweka kwa urahisi zaidi.

Suala la uandishi wa vitabu hapa nchini bado liko nyuma. Wapo wengi ambao wana simulizi kubwa za maisha yao lakini hawana mwamko wa kuandika vitabu, pengine hilo limesababishwa na utamaduni wa Watanzania wengi kutopenda kujisomea vitabu.

Kwa nchi nyingine duniani, utaona watu waliopata mafanikio ya kimaisha (wafanyabiashara), wanataaluma, viongozi wa kisiasa au viongozi wa dini wakiandika vitabu vinavyowahusu au juu ya jambo fulani ambalo wanalifahamu.

 

Kuna mifano michache ya viongozi hapa nchini ambao walitumia maarifa na uzoefu wao kuandika vitabu ili kurithisha historia za maisha waliyopitia kwa vizazi vijavyo. Vitabu walivyoviandika ni kumbukumbu ya kihistoria kwa sababu vimeakisi mabadiliko halisi ya maisha ya Watanzania.

Mwalimu Julius Nyerere ni mfano wa kuigwa kwa viongozi walioawahi kuandika vitabu. Aliandika vitabu mbalimbali kama vile Ujamaa: Essays on Socialism (1968), Uhuru na Ujamaa (1968) na Uhuru na Umoja (1966) na Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania (1993).

Mwingine ni aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Pius Msekwa ambaye ameandika vitabu mbalimbali vikiwemo The Transition to Multiparty Democracy (1995), Reflections On the First Multiparty Parliament (2000) na The Story of The Tanzanian Parliament (2013).

Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Edwin Mtei naye ameandika vitabu kadhaa akishirikiana na wenzake. Vitabu hivyo ni From Goatherd to Governor, Challenges of African Growth: Opportunities, Constraints and Strategic Directions (2007), The Political Economy of Economic Growth in Africa (2007) na Managing Tanzania’s Economy in Transition to Sustained Economy (1997). 

Ukifuatilia nchi zilizoendelea, watu wengi wamehamasika kuandika vitabu. Siyo wasanii, siyo viongozi, siyo wafanyabiashara, wote wamejitoa kuandika vitabu ili kuishirikisha jamii mafanikio yao na kuhamasisha.

Marais wengi wa Marekani wameandika vitabu kabla hata hawajapata mamlaka ya kuongoza nchi hiyo. Rais Donald Trump ameandika kitabu cha Trump: Think Like a Billionaire (2004) na Trump: The Art of the Deal (1987).

Barack Obama ameandika Dreams From My Father (1995) na Of Thee I Sing: A Letter to My Daughters (2010), Audacity of Hope wakati George W. Bush ameandika A Charge To Keep (1999) na Decision Points (2010).

Msanii Michael Jackson aliandika Moonwalk (1988) na Dancing The Dream (1992); Mfanyabiashara, Bill Gates ameandika The Road Ahead (1995); na Mhubiri wa kimataifa, Bill Graham ameandika vitabu kadhaa vikiwemo Just As I Am (1997) na Angels: God’s Secret Agents (1975).

Wiki iliyopita, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi alizindua kitabu chake kiitwacho “I Can, I Must, I Will: The Spirit of Success” ambacho kinazungumzia harakati zake mpaka kufikia mafanikio aliyonayo sasa.

Hatua ya Mengi kuandika kitabu hicho ni hamasa kwa wafanyabiashara na watu wenye mafanikio kama yeye. Amefanikiwa kuishirikisha jamii ya Watanzania njia alizopita na amekuwa chachu kwao kufanya kazi kwa bidii na kufikia mafanikio kama yake.

Kitabu hicho licha ya kuelezea maisha yake tangu akiwa mdogo, pia kimetoa mbinu mbalimbali za mafanikio. Dk Mengi, katika kitabu chake, anahamasisha vijana kutokata tamaa na kuamini kwamba wanaweza kufanya jambo lolote wakiamua kufanya hivyo.

Wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho iliyohudhuriwa na Rais John Magufuli, Mengi alisema alihamasishwa kuandika kitabu hicho na marehemu mwanaye, Rodney ambaye alimtaka siku moja aandike kitabu na kueleza harakati zake na mafanikio yake.

Dk Mengi alisema alimuahidi mwanaye kufanya hivyo ili kuwahamasisha vijana wengi kufikia mafanikio wanayoyaota. Alisema amefurahi kutimiza ahadi hiyo na kuwataka vijana kuthubutu kufanya jambo wanaloliamini.

“Ninafurahi leo nimetimiza ahadi yangu kwa mwanangu. Ahadi nyingine ni ya kwenda gym kila siku, kwa sasa ninakwenda mara tatu kwa wiki, nitaanza kwenda kila siku,” alisema Dk Mengi huku watu wakicheka.

Dk Mengi alisema ametoka kwenye familia masikini na familia yake ndiyo imemvutia kuwa mfanyabiashara mkubwa. Alisema alijifunza mambo mengi kutoka kwa mama na kaka zake ambao walikuwa wafanyabiashara wadogo.

 

JPM ahamasisha uandishi wa vitabu

Rais Magufuli aliwahamasisha wanataaluma na watu wengine kuiga mfano wa Dk Mengi kwa kuandika vitabu. Alisisitiza kwamba wazazi wahamasishe watoto wao kusoma vitabu kwa sababu kuna hazina kubwa ya maarifa kwenye vitabu.

Aliwataka Watanzania pia kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu. Alisema anaamini kitabu cha Mengi kitabadilisha maisha ya Watanzania wengi kwa kuwa na uthubutu na kushiriki katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda.

“Nimeona Profesa Mukandala (Rwekaza) alipokuwa anatoa summary ya kitabu hiki. Profesa Mukandala amefanya kazi katika Chuo Kikuu kama Vice Chancelor (makamu mkuu wa chuo), muda wake ukaisha akaongezewa, akaongezewa, amemaliza na amefanya kazi nzuri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.”

“Lakini sina uhakika kama ameandika kitabu, sina uhakika kwa sababu bado sijakiona kitabu alichoandika kwa ajili ya maisha yake tangu alipokuwa vice chancellor mpaka sasa ame-retire, pamoja na kwamba ametoa tafsiri nzuri ya kitabu cha Dk Mengi,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alimtaka Mengi aangalie uwezekano wa kukitafsiri kitabu chake ili Watanzania wengi waweze kuelewa alichokiandika. Alisisitiza kwamba akifanya hivyo atakuwa amewasaidia wananchi wengi ambao watafikiwa na kitabu hicho.

 

Maudhui ya kitabu

Akichambua maudhui ya kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, aliyekuwa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala anasema tafsiri rahisi ya kitabu hicho cha “I Can, I Must, I Will” ni “Ninaweza, Ninalazimika, Nitafanikiwa.”

Profesa Mukandala anasema kitabu hicho chenye kurasa 311 kinazungumzia maisha ya mtoto Reginald ambaye alikulia kwenye familia masikini ya Mzee Abraham Mengi pamoja na ndugu zake wengine.

Anasema sura tatu za mwanzo zinazungumzia familia yake, maisha yake akiwa mtoto na mafunzo aliyoyapata kutoka kwenye familia hiyo. Anasema kitabu kimebainisha kwamba Mengi alijifunza kuongeza thamani ya bidhaa kutoka kwa baba yake ambaye alikuwa akinunua mbuzi na kuwaosha vizuri, kisha kuwauza kwa bei ya juu.

“Mengi anaeleza kwenye kitabu chake kwamba baba yake alikuwa ananunua mbuzi mnadani, anawaosha na kuwa-brush vizuri, kisha anakwenda kuwauza kwa bei ya juu,” anasema Profesa Mukandala.

Anasema mama yake naye alikuwa mfanyabiashara ambaye alikuwa akinunua ulezi anakwenda kuusafisha nyumbani kisha anatia maji ili kuongeza uzito. Anasema akipeleka sokoni ulezi huo anauza kwa bei ya juu kwa sababu uzito unakuwa juu.

Profesa Mukandala anasema sura tano zinazofuata zinamtambulisha Mengi kama mhasibu, mmiliki wa vyombo vya habari, mjasiriamali, kiongozi wa umma na mtu anayependa familia yake. Mengi amesoma Tanzania na Scotland.

Anasema mwaka 1984, Mwalimu Nyerere alimteua kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu ya NBAA, nafasi ambayo ameitumikia kwa miaka 16. Anasema alijenga uhusiano mzuri kati ya Serikali na mashirika ya umma, jambo lililomfanya ateuliwe nafasi hiyo.

Mwanazuoni huyo anasema Mengi anasimulia kwenye kitabu chake kwamba alianza biashara kidogo kidogo kwa kuagiza kalamu nje ya nchi, na kuzitengeneza katika nyumba aliyokuwa amepanga katika Barabara ya Pugu, kisha kuziuza.

Baada ya muda mfupi, anasema alifanikiwa kupata Dola za Marekani milioni moja kupitia kampuni yake iliyoitwa Tanzania Kalamu Company Ltd. Baada ya miaka kadhaa, ilikua na kuwa makampuni ya IPP.

IPP inajumlisha makampuni mbalimbali ya utengenezaji wa vinywaji, uchimbaji madini, uuzaji gesi na mafuta na uzalishaji wa viwandani. Kwa upande wa vyombo vya habari, Mengi alianza na magazeti ambayo ni The Guardian na Nipashe, baadaye alianzisha televisheni ya ITV, EATV na Capital.

“Dk Mengi hajajifunga kwenye miradi yake na biasharaza zake pekee bali pia amekuwa tayari kuitumikaia jamii.

“Ni mwanzishi na mwanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), mwenyekiti wa Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC), mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC),” anasema Profesa Mukandala.

Dk Mengi amepata tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa kama vile Tuzo ya Kiongozi na Tuzo ya Azimio la Arusha, daraja la kwanza zilizotolewa na Serikali mwaka 1994 na Tuzo ya Martin Luther King Jr Drum Major for Justice ya Marekani (2008).

 

 

Columnist: mwananchi.co.tz