Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kiswahili na nguvu ya utambulisho ughaibuni

10652 Erasto+Duwe TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lugha ina dhima nyingi. Miongoni mwake ni dhima kubwa ya kutambulisha watu wasiofahamiana.

Dhima hii si rahisi kujibainisha katika mazingira asilia ya uzungumzaji wa lugha husika au mazingira ambayo lugha hiyo hutumiwa na watu wengi, bali inadhihirika zaidi katika mazingira ya ugenini ambako mmoja ajuaye lugha fulani anaweza kumsikia mtu au watu wengine wakitumia lugha ambayo yeye anaifahamu.

Katika mazingira ya namna hiyo, watumiaji wa lugha hiyo wanaweza kujitambulisha kila mmoja kwa mwenziwe na kujisikia wamoja kwa sababu ya lugha inayowaunganisha.

Christine Torome raia wa kutoka nchini Kenya ambaye amekuwapo nchini Ujerumani kwa miezi kadhaa, amekutana na Mbalamwezi ya Kiswahili na kueleza namna lugha ya Kiswahili ilivyo na nguvu ya kukutanisha, kuunganisha na kutambulisha.

Anaeleza kuwa siku ya kwanza akiwa ‘super market’ na Mkenya mwenziwe wakitafuta mahitaji yao huku wakifanya mawasiliano yao kwa Kiswahili, walitokea watu watatu weusi ambao walionekana kufuatilia maongezi yao.

Kati ya watu hao watatu, mmoja wao aliingilia kati maongezi yao akiuliza: “Samahani, nyinyi watoto wa Kenyatta au Magufuli?” Christine na mwenziwe wakiwa bado hawajajibu, mtu huyo aliyejitambulisha kwao kuwa ni Mtanzania aliwaambia kuwa aliwasikia wakizungumza Kiswahili akahisi kwamba ni watu wanaotokea Afrika ya Mashariki. Kuanzia hapo maongezi yakaanza. Wakafahamiana, wakajenga urafiki na kutembeleana.

Katika tukio jingine, Christine anaeleza kuwa akiwa na Wakenya na Watanzania wenziwe katika kituo cha gari moshi, wakimsubiri mwenyeji wao Mjerumani, ghafla alitokea mama wa Kijerumani . Mama huyo alisimama na kuwasalimia kwa Kiswahili. Walipomhoji mintarafu kukijua kwake Kiswahili, aliwaeleza kuwa miaka kadhaa iliyopita aliwahi kuishi Tanga, nchini Tanzania akitoa huduma katika kanisa. Alifafanua kuwa akiwa Tanga alilazimika kujifunza Kiswahili kwa jitihada zote ili kuweza kuwahudumia vizuri watu wake.

Hata hivyo, alieleza kuwa aliporudi Ujerumani hakuwapata watu wengi ambao angeweza kuendelea kuzungumza nao Kiswahili. Alisema kuwa kuna rafiki yake, Mtanzania, ambaye anafanya kazi huko Ujerumani sehemu inayokaribiana na yeye anapofanyia kazi. Alieleza kuwa huonana na Mtanzania huyo daima.

Alisisitiza; “Napenda kuonana naye daima na kila tunapoonana tunatumia Kiswahili katika mawasiliano yetu licha ya kwamba yeye anajua Kijerumani pia.” Alieleza kuwa matumizi ya Kiswahili, yanamjengea taswira nzuri ya safari yake nchini Tanzania, huduma aliyokuwa akiitoa na ukarimu wa watumiaji wa Kiswahili huko Tanga. Christine alieleza kuwa, mama huyo alionekana kuongea Kiswahili vizuri kama Mswahili aongeavyo Kiswahili bila ya kugugumiza au kutafutiza maneno. Hata hivyo, Christine anaeleza kuwa baadhi ya Wajerumani waliopata kutembelea Afrika ambao wanakijua Kiswahili, wanapowaona watu weusi hupenda kuwasalimu kwa Kiswahili wanapohisi kuwa wanatokea Afrika Mashariki. Salamu wanazotumia ni kama vile: ‘Jambo’, ‘habari’, ‘Mambo’. Kiswahili nchini Ujerumani licha ya watu wachache kukifahamu, kinafundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali.

Ni lugha inayochangamkiwa na watu wengi katika idara za lugha za kigeni ambamo Kiswahili hufundishwa kama lugha na kama fasihi ya Kiswahili. Baadhi ya vyuo maarufu vifundishavyo Kiswahili nchini Ujerumani ni Humboldt Berlin, Leipzig na Bayreuth.

Columnist: mwananchi.co.tz