Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kipi bora kutengwa au kuvumilia ndoa ya mateso?

Kutengwa Pic Kipi bora kutengwa au kuvumilia ndoa ya mateso?

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Licha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kuanza mwaka 1908 baada ya wafanyakazi wa kiwanda cha nguo New York Marekani kugoma kutokana na mazingira mabaya yaliyowakabili, vitendo vya ukatili na unyanyasaji vimeendelea katika mataifa mbalimbali.

Kwa Tanzania vitendo hivyo, hasa kwa wanawake waliopo kwenye ndoa vimeendelea kuwa tishio na kugharimu maisha yao.

Miaka ya karibuni kumekuwa na matukio ya mauaji dhidi ya wenza, hata hivyo mara nyingi matukio ya aina hii hayatokei ghafla, bali huanza taratibu.

Rose Njiro ni mfano wa waliopitia ukatili kabla ya kuamua kutafuta njia yake ya kujinasua.

Mama huyu kutoka jamii ya Kimasai alikumbana na utamaduni wa kuozeshwa akiwa na umri mdogo.

Katika utamaduni huo, Mmasai mwanawake anapopata ujauzito, hujitokeza mwanamume kuonyesha utayari wa kumuoa mtoto atakayezaliwa endapo atakuwa wa kike.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Rose, akiwa tumboni tayari alishachumbiwa na alipozaliwa alikuwa mchumba wa mtu anayesubiri kwenda kwa mumewe bila kujali anayemuoa amemzidi umri kiasi gani.

Elimu pekee aliyoipata ni ya darasa la saba na hata alipofaulu kujiunga na kidato cha kwanza hakupata fursa hiyo kwa kuwa alitakiwa kuolewa.

Akiwa na miaka 12 akaanza maisha mapya ya ndoa kama mke wa tatu kwa mzee wa miaka 59.

“Niliteseka sana kwenye ndoa hii, kwanza wazazi wangu hawakuwa tayari niolewe, lakini baba yangu mkubwa alikuwa na nguvu kwenye familia na ndiye aliyeshikilia msimamo wa mimi kuolewa kwenye ile nyumba na akaniozesha. Nilikaa kwenye ndoa nikapata watoto wanne nikiendelea kunyanyasika.”

Rose anasema aligundua kuwa anapitia katika ukatili na taratibu akaanza kushiriki kwenye harakati za kujikwamua na kufikia mwaka 2011 alifanikiwa kutoroka kwenye familia aliyoolewa na kuanza maisha mapya.

Hatua hiyo ilimfanya kukutana na changamoto nyingine kwa kuwa, katika mila za Kimasai ni aibu kwa mwanamke kutoka kwa mume kwa maana ya ndoa yake kuvunjika.

“Watu walikuwa wananishangaa na kunitenga kwamba nimetoka kwa mwanamume, kitu ambacho ni kibaya sana kwenye jamii ya Kimasai, pili nikaanza kujitokeza hadharani kupigania haki za wanawake na watoto.

“Vikwazo vingi nilivyopitia vilinifanya kuanzisha Shirika la Mimute Women Organization linalopambana na mila kandamizi katika jamii ya Kimasai, ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji na nyingine zinazofifisha ustawi wa wanawake wa Kimasai,” anasema Rose.

“Katika jamii za Kimasai, wanawake na watoto wanapitia majanga makubwa lakini hawana sauti, ndiyo maana nimeamua kujitoa kupita huku na kule kuzungumza kuhusu matatizo tunayopitia ili tupate msaada, watoto wa kike wanaozeshwa wakiwa wadogo mno.”

Rose ni mfano wa wanawake wachache ambao wamethubutu kuacha ndoa zao kutokana na vitendo vya ukatili ambavyo wamekuwa wakikutana navyo kutoka kwa wenza wao.

Wengi wanashindwa kufanya uamuzi kwa kuhofia jamii itakavyowatazama, ikiaminika kuwa mwanamke anayetoka kwenye ndoa ameshindikana, hivyo wanaishia kuvumilia manyanyaso na vitendo vya ukatili hadi kufikia kupoteza maisha au kupata ulemavu.

Novemba 16 mwaka huu mwanamitindo Flaviana Matata alitumia ukurasa wake wa Instagram kuelezea hali aliyopitia baada ya ndoa yake kuvunjika na jamii ilivyomchukulia.

“Jamii yetu inatakiwa kuacha kuwalaumu wanawake pale ndoa inapovunjika na kwa nini wanawake walaumiwe. Hatumsaidii mtu kwa kumdhihaki pale ndoa yake inapofikia mwisho,” ameandika Flaviana.

“Hii ndiyo sababu wapo wanaoendelea kuwepo kwenye ndoa zenye machungu, ukatili na maumivu. Kabla ya kumdhihaki mtu kwa ndoa yake kuvunjika tafadhali jaribu kumhurumia. Hakuna anayefunga ndoa ili baadaye ikavunjike.”

Kuhusu saikolojia

Mwanasaikolojia Saldeen Kimangale anasema mwanamke atatakiwa kuchagua kati ya lawama na fedheha kutoka kwa jamii au manyanyaso na ukatili kutoka kwa mume yanayoweza kuhatarisha maisha yake.

“Lililo la busara ni kutoka kwenye kifungo cha ndoa na uhusiano hata kama utabebeshwa lawama na fedheha, kwa kuwa jamii inachojua kuhusu hadhi na ubora wa uhusiano wako ni karibu na sifuri, kwa hivyo hakuna haja ya kuwahakikishia au kuwathibitishia kwamba uko sahihi,” anasema mwanasaikolojia Kimangale.

“Kuamua kufanya hivyo ni kuhatarisha afya yako hasa ya akili, rasilimali isiyo na mbadala. Ni muhimu kwa mwanamke kutambua kuwa iwapo atajizingatia yeye zaidi kama wafanyavyo wanaume basi nguvu na msukumo wa watu na jamii haitawasumbua.”

Mkurugenzi wa Taasisi ya Family Vibes inayotoa huduma za ushauri, Dk Mayrose Majinge anasema ndoa inapaswa kujengwa kwa upendo na masikilizano baina ya wanandoa na inapotokea mambo yanakwenda tofauti kiasi cha uhai wa mmoja kuwa hatarini ni vyema kuchukua hatua mapema.

“Hatupendi ndoa zivunjike kwa kuwa ikitokea hivyo wanaothirika ni watoto, lakini kama unaona umejaribu njia mbalimbali za kujinusuru wakati uhai wako upo hatarini, kama unaona dalili za maisha yako kuwa hatarini usisubiri hadi ufike huko au kumdhuru mwenzio, ni heri utoke,” anasema Dk Mayrose ambaye pia ni mtaalamu wa maendeleo ya watu.

Anasema kuna haja ya jamii kutambua kuwa kuishi kwenye unyanyasaji na ukatili ni hatari zaidi ya mwanamke kutoka kwenye ndoa au mahusiano yanayomuumiza.

“Pamoja na dhana potofu ambazo zimekuwepo kwenye jamii, sasa hivi kuna wimbi baya la watu kufurahia matatizo ya wenzao, yaani mtu anafurahia kabisa kumuona mwenzie ana shida na anamzungumzia vibaya bila kujali ataumia kiasi gani,” anasema Dk Mayrose.

“Kwanza tunatakiwa kuikataa hii tabia, upendo ni kitu kikubwa na chenye thamani, tujifunze kupendana, kuhurumiana na kuelewa changamoto anazopitia mwenzio, kama upo kwenye nafasi ya kumsaidia kutatua au kupata ufumbuzi msaidie, sio kumsema au kumtolea maneno ya kukatisha tamaa, wewe mwenye tatizo, hususan la kupitia ukatili kwenye uhusiano usisubiri hadi upate ulemavu au ugharimu maisha yako.”

Hata hivyo, kupitia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, baadhi ya wanawake wametambua thamani yao katika jamii na familia kwa jumla kutokana na kupata elimu wanapohudhuria sherehe hizo.

Wananchi wanasemaje?

Farida Bakari anasema baadhi ya watu huwa wanaogopa kuachwa pindi vipigo vinapozidi kwa kuhofia jamii itawachukulia tofauti, hivyo huona bora wavumilie mateso.

“Kuna watu wanapigwa sana na waume zao na hawasikilizwi, lakini hawasemi, wanaogapa mama fulani ataenda kuwaambia wana kikundi katika Vicoba, matokeo yake wanaishi kwa hofu,” anasema.

Akizungumzia unyanyasaji ndani ya ndoa, baba Brenda anasema wanaofanyiwa ukatili huo hasa wanawake wanapaswa kutokaa kimya.

“Ukiona mtu amejeruhiwa na mumewe basi tatizo hilo sio la siku moja, limeanza tararibu hadi limeota mizizi,” anasema.

Ripoti ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu (UNODC) ya mwaka 2018, inasema nyumbani ni mahali hatari zaidi kwa wanawake, hasa kwa mauaji na ukatili. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanawake 87,000 waliuawa duniani mwaka 2017, huku 50,000 kati yao wakisababishiwa matatizo hayo na wenzi wao na watu wa familia.

Columnist: www.mwananchi.co.tz