Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kinachowakwaza walemavu kwenye fursa za mikopo

10236 Walemav+pic TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hivi karibuni Serikali ilitambua kuhusu umuhimu wa kundi la walemavu katika kupata mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Mikopo hiyo ambayo ni asilimia 10 ya mapato yote ya halmashauri, awali asilimia tano ilikuwa ikienda kwa wanawake na asilimia tano nyingine kwa vijana.

Hata hivyo baada ya Serikali kutambua kundi la walemavu kuachwa nyuma katika hilo ukizingatia kuwa nao ni watu wanaojishughulisha na uzalishaji mali ikiwemo biashara, waliwaingiza katika utaratibu huo.

Mabadiliko hayo sasa yamefanya asilimia nne kwenda kwa vijana, asilimia nne nyingine kwa wanawake na asilimia mbili kwa walemavu.

Pamoja na nia njema hiyo ya Serikali imebainika kuwa zipo changamoto lukuki zinazolisibu kundi hilo kutoifikia mikopo hiyo.

Fredrick Msigala ambaye ni meneja ushauri na utetezi wa programu ya Kuwezesha Vijana Kiuchumi (YEE), anasema kwamba pamoja na mafunzo hayo kuwa na mtazamo chanya katika suala la kumuwezesha mlemavu kujikwamua kiuchumi bado kundi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuzifikia fursa ikiwemo mikopo.

YEE ni mradi uliokuwa ukisimamiwa na Shirika la Plan International kwa kushirikiana na wadau wengine na umetekelezwa katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

Msigala ambaye pia ni mtumishi wa CCBRT anasema fursa hii haipo kwa waliopata mafunzo ya YEE, bali kwa kundi kubwa la walemavu.

“Siku za karibuni kumekuwa na uhamasishaji mkubwa wa walemavu kupelekwa shule, lakini ukweli huko nyuma watu hawa walifichwa tu nyumbani na kuonekana hawawezi kufanya chochote ikiwemo kusoma.

“Ni kutokana na hali kama hii hata taarifa za masuala ya kukopa kwao zimekuwa ngeni na moja ya matatizo ya kufikia fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi za fedha ikiwemo zile za Serikali,” anasema Msigala.

Ili kuondokana na hili, anasema ipo haja ya shule, vyuo na taasisi za elimu kuwaekewa idadi maalum ya kuchukua walemavu ili nao wapate elimu. Anasisitiza elimu hiyo isiwe ya kuwatenga wasome wenyewe bali kuwachanganya na watu walio kamili na kuongeza kuwa kinachotakiwa ni kuwajengea mazingira wezeshi ikiwemo vifaa na majengo yanayofikika kirahisi.

Sababu nyingine ya kushindwa kufikia fursa hiyo, Msigala anasema ni walemavu kujinyanyapaa wenyewe kwa kuona hawawezi kufanya lolote na njia kwamba nyepesi kwao ni kuwa ombaomba.

Msigala anasema tabia hii ilijikita kwenye jamii kwa muda mrefu, jambo ambalo hata leo akionekana mlemavu kafanya jambo kubwa la kiubunifu, watu wanamuuliza mara mbilimbili ni wewe kweli umefanya kazi hii?

Anasema ipo haja ya walemavu wenyewe kujikubali kwamba wanaweza, kwani hawezi kukubaliwa na watu wengine kabla ya wao wenyewe kujikubali.

Pia masharti magumu ya ukopaji, nalo Msigala anasema limekuwa kikwazo ukizingatia wengi wa walemavu wanatoka familia duni, lakini ukija kwenye mikopo unatakiwa uwe na mali isiyohamishika na wengi hawana.

Anashauri hata mikakati ya Serikali kuhusu Tanzania ya Viwanda inapaswa isiwaache nyuma walemavu, kwani ili kufikia huko lazima kuwepo ujumuishi wa kundi hilo.

Msigala pia anasema ili kuwawezesha walemavu kukopa, jamii inapaswa kuwaunga mkono kwa kununua bidhaa zao, kwani huwezi kuendelea kuzalisha kama huna walaji na ili uweze kurudisha mikopo vizuri lazima biashara iwe inafanyika.

Walemavu katika YEE

Akizungumzia ushiriki wa walemavu katika mradi wa YEE, Msigala anasema wamejifunza mengi ambayo kama si mradi huo huenda wasingepata elimu hiyo.

Anasema mpaka mradi unafikia ukingoni mwishoni mwa Juni mwaka huu, walemavu 220 kati ya 900 waliolengwa wamepata mafunzo yafani mbalimbali ikiwemo mapishi na kupamba, ufundi cherehani na ufundi wa kutengeneza simu.

Katika mafunzo hayo ambayo yalifanyika kwa miezi sita, mitatu darasani na mitatu kwa vitendo, yaliwafikia hadi walemavu ambao hawawezi kutoka eneo moja kwenda jingine akiwemo Dismas Komba (38) mkazi wa Ifakara, Morogoro ambaye kwa sasa ni fundi simu anayefuatwa na wateja nyumbani.

Hata hivyo Msigala anasema yapo mambo mbalimbali waliyojifunza wakati wa utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitatu ambao ulianza mwaka 2015.

Mojawapo ni kuhitajika bajeti ya kutosha linapokuja suala la kutoa mafunzo kwa walemavu, ambao hawa wanahitaji muda mwingi wa kufundishwa ukiwalinganisha na watu waliokamilika.

“Kuna baadhi ya maeneo ambayo walimu walifika majumbani kwa walemavu, lakini kuna maeneo mengine kutokana na mazingira ikiwemo Dar es Salaam ilishindikana kuwafikia kutokana na gharama za kuwa na walimu.

“Lakini nina imani kama mbele ya safari utakuja mradi wa aina hii na fedha ikatengwa nyingi kwa kundi hili, kila mmoja atakayekuwa amelengwa atafikiwa ipasavyo ikiwemo kuwa na walimu wengi,” anasema Msigala.

Jingine walilogundua ni kuwa walemavu wakiwezeshwa wanaweza kwani wana uwezo na upeo mkubwa wa kufanya mambo na kinachowatofautisha na watu wengine ni hali zao za kimaumbile.

Pia anasema ili kufikia walemavu wengi zaidi ni vyema vyama vya watu hao vikashirikishwa kwa karibu kwani wao ndio wanawatambua zaidi hali zao na mahali walipo.

Nini mikakati ya serikali

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe ambaye mradi wa YEE umepita mkoani kwake, anasema mikakati yao ni kuhakikisha walemavu wanakuwa na maeneo ya kuendesha shughuli zao.

Kebwe anasema elimu waliyoipata kundi hilo hawawezi kuiacha ikapotea na kuahidi kwa mkoa wao watakuwa wanafuatilia maendeleo yao mara kwa mara.

Kwa upande wa mikopo anasema wachangamkie fursa ya asilimia mbili iliyowekwa kwa ajili yao na kuwataka watoe taarifa pale wanapowekewa vikwazo vyovyote katika kuipata mikopo hiyo badala ya kulalamikia pembeni.

Wilayani Kibaha mkoa wa Pwani, kupitia ofisa maendeleo ya vijana halmashauri ya Kibaha, Pudensian Domel, amewataka walemavu kuchangamkia fedha zilizotengwa kwa ajili yao.

Pudensia anasema kasi ya walemavu kuomba mikopo kwa wilaya hiyo ni ndogo, kati ya Sh37 milioni zilizotengwa ni Sh2 milioni tu ndio zimetumika hadi sasa.

Kwa Dar es Salaam wilaya ya Temeke, Anna Malika, ofisa vijana wa wilaya hiyo, anasema kilichosababisha kutotoa mikopo hadi sasa kwa baadhi ya vikundi vya walemavu waliopata mafunzo ni kutokana na vikundi vingi kutokamilisha usajili.

Mmoja wa walemavu aliyefaidika na YEE, Immaculata Lusajo, mkazi wa kijiji cha Nyangao, mkoani Lindi, ambaye ni fundi cherehani, anasema kupata moyo kwake kuingia katika mradi huo kumechangiwa na familia yake ambayo imekuwa naye muda wote.

Immaculata ambaye hushona nguo akiwa amesimama anasema kabla ya hapo familia yake ilimnunulia cherehani moja na alikuwa akishona nguo ndogo ndogo.

Baada ya kushiriki mafunzo aliongezea ujuzi wa kudarizi na sasa hata kipato chake kimeongezekea na kuomba miradi ya namna hiyo kuwafikia walemavu wengine zaidi.

Mlemavu mwingine Fatma Mabrouk, amesema awali kabla ya YEE kumpa mafunzo alikuwa akitegemea kila kitu kutoka kwa mama yake, na kukiri kuwa mradi huo umemtoa gizani, kwani awali alikuwa akijua yeye ataishia kuwa tegemezi.

Columnist: mwananchi.co.tz