Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kila swali ni lazima liwe na jibu

49521 Gaston+Nunduma

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna kila sababu ya kukubali kuwa masikilizano ya kifamilia huzaa tija kwa jamii nzima. Kila mmoja akitimiza majukumu yake ndani ya familia ndivyo anavyoweza kufanya kazi kwa nafasi na ufanisi, kusoma kwa bidii na kudumisha uhusiano mwema kwa wale wanaomzunguka.

Ustawi wa jamii huanzia kwenye familia. Kama huwezi kumudu kuiongoza vyema familia yako, asilani huwezi kuwa kiongozi wa mtaa, kijiji, wilaya, mkoa, nchi au bara lako. Uungwana huanzia nyumbani hivyo litakuwa jambo geni kwa mtu asiyejali familia kuujali mtaa mzima.

Katika dunia nzima wake za wafalme hubeba hadhi ya umalkia. Hali kadhalika wake za marais huitwa “first ladies” wanapobeba dhamana ya ukuu miongoni mwa wanawake wote katika nchi zao. Hii inamaanisha kumtunza kiongozi ni kutunza umati wa watu.

Mama wa familia huwa na kazi ngumu sana kama kiongozi. Yeye ndiye anayetoa utetezi na kurekebisha mwenendo mzima wa mumewe pale anapoteleza. Inaeleweka kuwa baba ni lazima asimamie maamuzi yake, lakini yanapomkwaza mtu inabidi mama asaidie. Baba naye kwa kushauriwa na mama anaweza kulegeza baadhi ya misimamo ili mambo yasonge.

Familia za kifalme huonyesha umakini wa hali ya juu kutokea kwenye hatua za awali. Mtoto anayetarajiwa kuwa mfalme au malkia anawekewa uangalizi wa hali ya juu. Usemi wa “mke wa Kaisari hapaswi kubeba waa (doa)” huenda ndio uliomgharimu Princess Diana mwaka 1997.

Diana alikuwa maarufu kabla hajaingia kwenye familia ya kifalme. Lakini hali ilianza kubadilika mwaka 1993 baada ya picha za Diana zilizomwonyesha akiwa katika ‘kivazi cha hasara’ zilipozagaa na kuuzwa kwa fujo ndani na nje ya Uingereza. Mamlaka zilipiga marufuku biashara hiyo na Diana kuanza kulaumiwa.

Inasemekana kampuni ya MGN ambayo ndiyo ilimiliki picha hizo ilimlipa Diana kiasi cha Paundi milioni moja za Uingereza na kuchangia Paundi laki mbili kwenye taasisi zake za misaada ya jamii. Diana aliyakiri hayo na kusababisha mzozo kwenye familia na sintofahamu kwa Waingereza.

Mwaka 1996 Diana alitalikiwa na mwenza wake Prince Charles na kupoteza sifa ya kuwa mrithi wa kiti cha kifalme. Kuanzia hapo Diana alikuwa na uhusiano na daktari wa upasuaji wa moyo, Hasnat Khan mpaka alipokuja kugundulika kuzama kwenye mapenzi mazito ya Dodi Fayed, mtoto wa bilionea wa Kimisri aliyekufa naye kwenye ajali ya gari.

Tunaona jinsi Diana alivyoandaliwa lakini hakuweza kwenda sawa na familia ya kifalme. Kwa upande mwingine tunaiona familia ikikosa amani kutokana na yule waliyemwandaa kutaka kuishi kama Diana na si kama malkia mtarajiwa.

Kwenye familia zetu huku mtaani ipo shida kubwa ya masikilizano. Kwa kawaida mtu aliye sawasawa ana uwezo wa kusema maneno 125 mpaka 180 kwa dakika moja. Na anao uwezo wa kusikiliza kati ya maneno 400 mpaka 500 kwa dakika. Mara nyingi msikilizaji anao uwezo zaidi ya msemaji kwa sababu anayo hiari ya kuzingatia au kutozingatia yale ayasikiayo. Ndiyo maana mtu anaweza kuendelea na mapishi huku akisikiliza vipindi vya redio. Jiulize swali moja, unampa nafasi msemaji mkiwa kwenye majibishano?

Watu wenye busara huonyesha utulivu hata kama hawasikilizi ili kumpa moyo msemaji. Ugumu unaingia pale msikilizaji anapoamua kujibu kabla msemaji hajamaliza hoja yake. Hapa ndipo tunapoona kutoelewana kati ya mke na mume, na kosa hilo linaambukiza familia na makundi yaliyo jirani na familia hiyo.

Kuna wakati familia inafikia hatua ya kutosikilizana. Hatua hii huanzia kwenye kutoaminiana na huenda ikafikia hata kuzuia majadiliano muhimu. Kama hali imefikia hapo ni lazima kuwepo na upande wa tatu utakaoweza kusikiliza hoja za kila upande.

Katika mazungumzo juu ya jambo makini hasa kwenye familia, kila mmoja anapaswa kuzingatia nafasi. Kwa mfano kunapotokea malalamiko ya mke dhidi ya mume - mume anapaswa kuyasikiliza na kuyaelewa kabla hajafikia uamuzi wa kutoa maelezo yake.

Na mume anaporuhusiwa kutoa maelezo, mke ayasikilize kwa makini kabla hakijaanza kipindi cha maswali na majibu. Mabishano huweza kutokea iwapo mmoja wao hataruhusiwa kumaliza anachosema. Wasikilizane kwa umakini mkubwa kabla hawajaanza kuulizana maswali.

Swali moja baada ya lingine. Kwa kuwa mlalamikaji huwa na hoja na maswali mengi anaweza kuwa na jazba. Anajikuta akiyamwaga bila mpangilio na bila kuzingatia uzito wake. Anashauriwa kuuliza swali moja fupi na kusikiliza jibu kabla hajauliza lingine.

Swali halijibiwi kwa swali. Kuna hali ya kukwepa kujibu maswali ya msingi kwa kupandikiza swali juu ya swali. Mtu aweza kujibu “Sasa ulitaka mimi nifanyeje?” au “mbona wewe ulifanya hivyo”. Kimsingi maneno kama hayo hayatakiwi kupata nafasi hata kidogo kwenye mazungumzo.

Mwisho wa yote ni lazima kuwepo na maridhiano. Sisemi kuwa utatuzi wa migogoro ni lazima ufanyike katika siku moja, lakini makubaliano aidha ya kusuluhisha au hata ya kuahirisha ni lazima yafikiwe na pande zote.



Columnist: mwananchi.co.tz