Uamuzi wa Rais John Magufuli kurejesha utaratibu wa zamani wa utoaji wa mafao kwa wastaafu wa serikalini yaani kutoa asilimia 50 ya mafao kwa mkupuo umepokelewa kwa shangwe si tu kwa wafanyakazi, bali hata wale waliokuwa wakitetea makato hayo.
Rais Magufuli alitoa suluhisho hilo Desemba 28, 2018 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), mifuko ya hifadhi za jamii ya PSSSF na NSSF na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Hapa ndipo wale waliokuwa wakipendekeza kutetea makato ya asilimia 75 wameumbuka.
Lakini licha ya uamuzi wa Rais Magufuli kupokelewa kwa shangwe, bado kuna maswali mengi yamebaki nyuma yake. Kwa mfano, mfumo huo bado unatumika kwa wafanyakazi wa sekta binafsi wanaosimamiwa na NSSF ambao pia unapaswa kuboreshwa.
Rais Magufuli alisema mfumo wa zamani wa kukokotoa mafao utatumika katika kipindi cha mpito kitakachoishia mwaka 2023 ambako wafanyakazi 58,000 watastaafu na Serikali haitashindwa kuwalipa. Swali ni je, hii itakuwa furaha ya muda tu halafu maumivu yanarudi palepale?
Pamoja na furaha hiyo ambayo wafanyakazi wa umma wameipata, japo hadi 2023, bado kuna kero nyingi za wafanyakazi nchini. Iwe wa umma au wa sekta binafsi.
Kero kubwa ni kutopandishwa kwa mishahara ya watumishi wa umma.
Pamoja na kuwapo kauli ya Rais ya Mei Mosi 2018 alipoeleza sababu za kutopandisha mishahara aliposema, bado naamini anaweza kubadili msimamo na kuwafurahisha zaidi.
Hii ni pamoja na kuwapo miradi mingi mikubwa ambayo Rais alisema, “Kwangu mimi naona ukijenga reli ‘Standard gauge’ utabeba mizigo mingi hasa kwenye nchi ambazo ni ‘land locked countries’ kama Rwanda, Burundi, DRC nk. Ukibeba mizigo mingi utatengeneza pesa nyingi ambazo utazitumia hata kama ni kujiongezea mishahara.”
Pamoja na hiyo pia kuna kauli nyingine kwamba makusanyo ni makubwa na mapato yameongezeka. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitangaza ongezeko la mapato tangu utawala wa awamu ya Tano ulipoingia madarakani.
Basi tungetarajia ongezeko hilo liakisi maisha ya wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla.
Vilevile si rahisi wafanyakazi kusubiri mpaka hiyo miradi ikamilike ndipo wapate nyongeza.
Kama suala ni miradi ya maendeleo, Serikali inaweza kuchagua miradi michache ya mkakati ili kuepusha kuelekeza rasilimali fedha zote kwenye chungu kimoja na kuyaacha maeneo mengine yanalia?
Ni kweli kuwa miradi ya maendeleo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi, lakini pia ni lazima ustawi wa wafanyakazi nao uangaliwe mara kwa mara
Haya ni masuala ambayo naamini yanaweza kufanyiwa kazi na kuongeza furaha ya wafanyakazi huku pia miradi mikubwa ikiendelea kufanyiwa kazi.