Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kikokotoo cha pensheni kilipita njia gani hadi kuanza kutumika nchini?

34500 Pic+maloto Mwananchi Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ijumaa iliyopita (Desemba 28, 2018), Rais John Magufuli, alifanya kikao cha wazi na viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi za Jamii (SSRA)

Lengo la mkutano lilikuwa kujadili masuala ya mafao ya wafanyakazi. Kwa upekee kabisa, agenda iliyochomoza ikawa kanuni ya upigaji hesabu (ukokotoaji) wa malipo wastaafu au kikokotoo.

Hoja yangu si namna kulivyokuwa na malumbano kabla ya Rais Magufuli kuitisha mkutano, bali namna Rais alivyofanya uamuzi wa kubatilisha kanuni ya kikokotoo kipya, iliyokuwa ikilalamikiwa.

Mshangao ulikuwa mkubwa, baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, jioni ya siku mkutano huo.

Maelekezo ya Rais Magufuli, alipokuwa akibatilisha kikokotoo kipya na kutaka kitumike cha awali kabla ya kanuni mpya, yalionyesha dhahiri kuwa hakubaliani na ukokotoaji uliofanywa na Serikali. Na hapa ndipo palipo na mshangao.

Masuala ya kikokotoo cha pensheni, yapo chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu, waziri wake ni Jenista Mhagama. Kwa mantiki hiyo, Jenista anaiongoza wizara hiyo chini Waziri Mkuu.

Ukokotoaji mpya wa mafao ya wastaafu kupitia kanuni mpya iliyozuiwa na Rais Magufuli kutumika, inaelekeza kuwa mstaafu atapata mafao ya mkupuo katika uwiano wa asilmia 25) kisha kuendelea kulipwa asilimia 75 kidogokidogo kila mwezi.

Kwa kumnukuu Rais Magufuli alisema: “Mtu anafanya kazi yake kwa muda wote, halafu anamaliza unamwambia apewe asilimia 25, haiingii akilini. Hata Waziri akimaliza ubunge wake ukimwambia utampa asilimia 25, kisha nyingine kidogokidogo hawezi kukubali.”

Hapa Rais Magufuli alitoa picha kuwa yeye mwenyewe utaratibu wa mafao haukubali. Kwamba hata Jenista ambaye ndiye msimamizi wa wizara inayoratibu kikokotoo hawezi kukubali.

Katika hotuba hiyo Rais Magufuli alikiri kufanya mkutano wa Baraza la Mawaziri na kukubaliana kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka mitano hadi miwili. NSSF kama mfuko wa sekta binafsi na isiyo rasmi, pia mifuko ya watumishi wa umma (LAPF, PPF, PSPF na GEPF kuwa PSSSF.

Lakini hakuna mahali Rais Magufuli anasema kanuni mpya ya kikokotoo ilipita kwake. Inawezekana kwamba naye alishtuka tu malumbano yanachukua nafasi. Huenda ni sahihi pia kusema kuwa kanuni haikupita Baraza la Mawaziri, maana Rais ndiye Mwenyekiti wa vikao hivyo.

Kwanini mshangao

Ibara ya 54 ya Katiba, ibara ndogo ya 1, 2 na 3, zinaeleza kuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri ni Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na Mawaziri kamili wa wizara. Inaelekeza Rais kuhudhuria vikao na kuviongoza. Rais asipokuwepo, vikao vitafanyika kwa Makamu wa Rais au Waziri Mkuu kuviongoza.

Ibara hiyo inaelekeza pia Baraza la Mawaziri ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba, na litamshauri Rais juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo.

Kumbe sasa jambo lolote linapowasilishwa ndani ya Baraza la Mawaziri, Rais lazima awe na taarifa kwa sababu Baraza linatakiwa limshauri.

Na ushauri unaweza kukubaliwa au kukataliwa. Kwa maana hiyo, Rais Magufuli angeshauriwa na Baraza la Mawaziri kuhusu kikokotoo kipya, bila shaka angekikataa kabla hakijatoka kwa umma.

Na wajibu mkuu wa Baraza la Mawaziri ni kuwa dira ya sera za Serikali na kufanya uamuzi kuhusu masuala ya kitaifa.

Baraza la Mawaziri linapokutana hutakiwa kujadiliana kuhusu matatizo ya nchi, hasa ya wakati unaokuwapo na kuyapatia ufumbuzi, vilevile hujadili miswada kabla haijapelekwa bungeni kuwa sheria.

Hata baada ya Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya kupinga akikokotoo hicho katika mikutano take na wanahabari, Spika Job Ndugai aliikana kanuni hiyo kuwa Bunge halitungi kanuni.

Hapo naopna mshangao, suala zito la mafao ya watumishi, liamuliwe nje ya Bunge na nje ya Baraza la Mawaziri.

Columnist: mwananchi.co.tz