Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kawawa aeleza jinsi walivyoishi na wapigania uhuru

70774 Kawawa+pic

Sat, 10 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Baadhi ya mataifa yanaendelea kuikumbuka Tanzania kwa mambo mengi, kubwa ni mchango walioupata wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa nchi zao.

Miongoni mwa mataifa ambayo yanaendelea kuikumbuka Tanzania katika mchango wake ni Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe.

Baadhi ya wapigania uhuru hao waliishi katika maeneo ya Kongwa, (Dodoma), Mazimbu (Morogoro) na Magomeni (Dar es Salaam) na wapo watu walioishi nao ambao hadi leo wanakumbuka maisha hayo.

Miongoni mwao ni Vita Kawawa ambaye aliishi na baadhi ya wapigania uhuru wa nchi hizo akidokeza kwamba licha ya kujaa upendo, furaha na amani, maisha yao yalitawaliwa na usiri mkubwa.

Kawawa ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa pili wa Tanzania, hayati Rashidi Kawawa (Simba wa Vita) anakumbuka namna walivyoishi na watu kadhaa lakini anamkumbuka zaidi Rais wa kwanza wa Namibia, Sam Nujoma (1990 – 2005) ambaye anasema alikuwa ni zaidi ya ndugu.

Anasema hakuna jirani aliyejua kuwa viongozi hao walikuwa ni wapigania uhuru katika nchi zao na badala yake waliwaona kama wakimbizi wa kutoka nchi zenye vita.

Pia Soma

“Wengi nawakumbuka lakini wawili tuliishi nao vizuri sana hasa Samora Machel wa Msumbiji, lakini naomba nimuelezee huyu ambaye alikuwa ni kama baba yetu naye ni Sam Nujoma. Kweli yeye na baba walikuwa zaidi ya marafiki.”

Kawawa anasema nyumba aliyokuwa akiishi Nujoma na nyumba walipoishi familia ya Kawawa katikati kulikuwa na nyumba nyingine tatu ambazo nazo zilikuwa na baadhi ya watu walioitwa wakimbizi.

“Kwanza alikuwa ni mtu wa kujichanganya, kwenye misiba alikuwepo na kwenye sherehe alionekana japo mara chache sana na kingine ambacho tulikuja kuona baadaye kuwa alikuwa ni mpigania uhuru, ni namna alivyokuwa makini kwa kila jambo,” anasimulia Kawawa.

Anasema kiongozi huyo alikuwa na usaidizi wa vijana kadhaa ambao walionekana kila wakati alipokuwepo na kila alipokuwa anaondoka nao walipotea, lakini walikuwa wamejichanganya na Watanzania wengine hata katika michezo.

Hata hivyo, anakumbuka namna kiongozi huyo alivyokuwa akitumia muda mwingi kukaa na Mzee Kawawa (baba) na kujadiliana mambo mengi, lakini yeye (Vita) na wenzake hawakujua kilichokuwa kikifanyika.

Msaada wa silaha

Vita Kawawa anasema kuna wakati Nujoma alikwama kuchukua silaha zilizokuwa zimezuiwa bandarini, lakini baba yake alishauriana na Rais Julius Nyerere wakamruhusu silaha zake zichukuliwe bila vikwazo.

“Hata hivyo, alikwama kuzichukua pamoja na agizo la Mwalimu ndipo baba alipokwenda bandarini na Mkuu wa Majeshi wa wakati huyo, Jenerali Mirisho Sarakikya akaamuru silaha zote zilizokuwa zimeingia nchini zikitakiwa kwenda Namibia ziruhusiwe na ilifanyika hivyohivyo,” alisema Kawawa.

Anasema kitendo hicho kilikuwa kimetanguliwa baadhi ya silaha ambazo Mwalimu Nyerere alikuwa amezitoa kwenda Namibia wakisubiri za kwao ziingie kwanza jambo lililomjengea imani kubwa Nujoma.

Anasema katika maisha ya wapigania uhuru hao, Serikali ya Tanzania ilikuwa inajua kilichokuwa kikiendelea kwani wakati mwingi walikuwa wakizungumza nao, lakini katika faragha zaidi ambayo majirani hawakujua huku ulinzi mkali lakini wa siri ukiendelea kuimarishwa katika majengo walimokuwa wakiishi.

Nujoma awa Rais

Baada ya Namibia kuwa huru, zikasikika taarifa kuwa Nujoma amekuwa Rais wa nchi hiyo na hapo ndipo watu wa Magomeni walipoanza kujua kuwa hakuwa mkimbizi, bali alikuwa ni mpigania uhuru aliyeishi kwa kujipanga zaidi.

Simulizi ya Kawawa inasema alipoondoka katika eneo hilo hakujulikana kama alikuwa amekwenda Kongwa au Mazimbu lakini wakasikia Sam Nujoma ni Rais wa Namibia, jambo lililowaacha wengi midomo wazi na mshangao kuwa waliishi na mtu mkubwa.

Anasimulia kuwa iliwachukua muda kuamini kwamba ni Nujoma yule waliyeishi naye Magomeni na si mwingine. Waliamini zaidi pale aliporudi akiwa Rais na akawasalimia kwa kuzungumza Kiswahili fasaha.

Kawawa aachiwa Ikulu Namibia

Moja ya matukio ambayo Vita anayakumbuka zaidi ni mwaliko ambao Nujoma aliutoa kwa baba yake kwenda Namibia akimtaka aende na familia yake naye akiwa miongoni mwao.

Anakumbuka namna ambavyo Nujoma aliwaachia Ikulu ya Namibia akaenda kukaa Ikulu ndogo ambayo anaikumbuka ilikuwa karibu na eneo la bahari na akamwambia Kawawa sababu za kumuachia Ikulu.

“Mimi alikuwa ananikumbuka na aliita kwa jina langu, lakini walipokaa na kuzungumza na baba alimwambia sababu za kumuachia aishi kwa siku kadhaa Ikulu akisema ni kutokana na mchango mkubwa waliopewa walipokuwa Tanzania, hivyo akasema hana shaka hata tungekaa Ikulu hapo,” alisema.

Moja ya kitu anachokumbuka ni namna ambavyo kila wakati mazungumzo ya wawili hao yalivyokuwa yametawaliwa na Kiswahili. Kwa mtu mgeni, angeweza kudhani kuwa wawili hao walikuwa ni watu waliotoka eneo moja.

Vita ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Namtumbo, alipoulizwa kuhusu kambi hizo alisema ile ya Namibia ilikuwa na usiri mkubwa kuliko nchi zingine kwani watu wa wengi hawakujua chochotekuhusu harakati za taifa hilo.

Kawawa anatamani kuona siku moja majengo waliyoishi viongozi hao yakienziwa na kuweka sehemu ya kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Columnist: mwananchi.co.tz