Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kauli za rejareja zinatonesha kidonda cha Katiba Mpya

9503 Pic+kauli TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Madaraka hulevya na mtu akishalewa haoni haya kufanya lolote hadharani. Halafu ulevi ukimtoka, anaanza kujutia aliyokuwa akiyafanya.

Lakini ulevi una tatizo la uraibu, linalomfanya mtumiaji wa kilevi kuendelea kuhitaji ulevi hata kama anapata madhara.

Ndicho kilichowatokea baadhi ya wanasiasa ambao hutoa kauli za lejelaja bila kuzipima kutokana na ulevi wa madaraka na wanaposhtukiwa hujifanya wanazikanusha au kuzifuta wakati zimeshaleta madhara.

Sote tumesikia kauli ya Kheri James, mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wa CCM alipokuwa akihutubia mkutano wa katika kata ya Bagara wilayani Babati Mkoa wa Manyara hivi karibuni, akiwaonya wananchi kwamba wakichagua wapinzani, CCM inayotawala haitapeleka maendeleo.

Kwa maelezo yake ni kwamba kwa kuwa CCM ndiyo inayotawala yenyewe ndiyo inaamua ipeleke wapi maendeleo na wapi isipeleke na hakuna cha kuifanya.

Kauli hii imekuwa chungu miongoni mwa wananchi wakimkosoa kupitia mitandao ya jamii na vyombo vya habari. Hata viongozi wenzake ndani ya chama wamemkosoa, japo hawasemi watamchukulia hatua gani.

Binafsi siamini kama ni kauli ya bahati mbaya, hata kama Kheri ameomba radhi. Kwanza yeye siyo kwanza kutoa kauli kama hiyo. Ilishatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti mara kadhaa na hajachukuliwa hatua yoyote.

Kwa mfano, Februari 11, 2018, Mnyeti aliwataka madiwani wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM ili waweze kushirikiana naye kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama tawala.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Haydom wilayani Mbulu, Mnyeti alisema yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane, ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.

Pamoja kauli hizo, hatukuwahi kusikia viongozi wa chama wala Serikali wakimkemea. Kama ndivyo, bila shaka wanakubaliana naye.

Kauli hizo za lejaleja pamoja na nyingine zinazotolewa na viongozi wa CCM na Serikali zinaashiria kuwepo kwa janga kubwa la kuzorota kwa mifumo ya kitaasisi na kupuuzwa kwa utawala wa Katiba. Ni kauli zinazotonesha machungu ya Watanzania wanaoteseka kwa kushindwa kufaidika na matunda ya demokrasia wala fedha zao zilitumika kuitafuta katiba mpya bila mafanikio.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano kabla hata ya kubadilishwa, inaitambulisha Tanzania kama nchi inayofuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Ibara ya 8 inasema wananchi ndiyo msingi wa madaraka ya Serikali.

Maana yake ni kwamba wananchi ndiyo wanachagua viongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji, kata na majimbo na Rais.

Sasa kama wananchi wa mtaa au kijiji fulani wameamua kuchagua kiongozi wa upinzani, ndiyo waadhibiwe kwa kunyimwa maendeleo?

Leo kwa sababu Mkoa wa Dar es Salaam umechagua wabunge sita wa upinzani kati ya majimbo tisa na kuongoza halmashauri ya jiji, hii inakuwa sababu wananchi kuadhibiwa kwa kunyimwa maendeleo? Huu ni ubaguzi unaolenga kuligawa Taifa kinyume na Katiba yetu.

Tunasikia kampeni za CCM kuhamisha wabunge, madiwani na makada wengine kwenda kwenye chama chao. Hii nayo inaashiria kuwa bila kuhamia huko, maendeleo hakuna?

Inasikitisha kuona jinsi mfumo wa upinzani unavyodhalilishwa, vyama vimebanwa kiutendaji kama vile kufanya mikutano ya hadhara, maandamano, huku viongozi wake wakinyanyaswa, utafikiri ni kosa la jinai kuwa mpinzani.

Tumewasikia baadhi ya mawaziri wakiwaambia wananchi kwenye mikutano ya hadhara kwa kuwa mbunge au diwani wao kahamia CCM maendeleo yataharakishwa. Mara utasikia hata bungeni wabunge waliohamia CCM kutoka upinzani watapewa upendeleo wa kuchangia. Hii ni rushwa ya wazi na ni sumu ya demokrasia.

Tumeona baadhi ya waliokuwa makada wa vyama vya upinzani wakijiunga na CCM na muda si mrefu wameteuliwa kushika nafasi za ukuu wa wilaya, makatibu tawala huku na kule. Kwa nini vyeo vitumike kama peremende kwa wapinzani?

Wananchi wanafaidika nini?

Hapa ndipo tunapoona mahitaji makubwa ya nchi yetu kuwa na Katiba Mpya. Katiba itakayojenga taasisi imara siyo watu imara. Katiba itakayoweka kipaumbele cha maendeleo bila kubagua watu kwa vyama wala ukabila.

Katika mchakato wa Katiba uliokwama, wananchi wengi walitaka madaraka ya Rais yapunguzwe. Rais ana madaraka makubwa ikiwa pamoja na kuteua wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, wakuu mikoa, wilaya na idara mbalimbali za Serikali.

Rais anayo madaraka ya kuteua viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambao kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri ambao pia ni wateule wake husimamia chaguzi zote.

Sasa kama Rais pia mwenyekiti wa CCM, chama chake kitashindwaje uchaguzi? Ni utata usioeleweka katika jicho la demokrasia.

Hata tukiangalia nchi jirani kama Zimbabwe au Kenya, tume zao za uchaguzi haziko hivyo. Kabla hata ya kwenda huko, visiwani Zanzibar tu hapo, Tume ya Uchaguzi (ZEC) inahusisha wapinzani. Kwa nini NEC iwe ya upande mmoja?

Viongozi wa CCM wamekuwa wakijitetea kuwa chama chao kinakubalika zaidi kwa kutekeleza ahadi za maendeleo, ni sawa. Lakini kama ni hivyo kwa nini wasiweke uwanja sawa wa mapambano ili tuwaone hao wananchi wanaoikubali?

Tuwe na Katiba itakayopunguza madaraka ya Rais, ila hata teuzi anazofanya, ziridhiwe na Bunge. Halafu nafasi za uteuzi zimekuwa nyingi mno bila manufaa ya kitaifa. Wakuu wa mikoa na wilaya zimepitwa na wakati, ziangaliwe upya.

Utashangaa Serikali hiyohiyo inayojipambanua kwa kubana matumizi, lakini wateule ni wengi na wote wanalipwa mishahara na marupurupu.

Tuwe na Katiba itakayolipa nguvu Bunge liisimamie Serikali kwa kila inalofanya ikiwa pamoja na kuhoji matumizi ya fedha za umma. Hata kama ni maendeleo makubwa kiasi gani, lazima Bunge liridhie kwanza.

Wabunge wasijisikie wanyonge mbele ya Serikali wanayoisimamia. Kuletewa maendeleo majimboni kwao, siyo fadhila wala sadaka, ni wajibu wa Serikali. Hata kama mbunge wa upinzani ameipigia kura ya hapana Bajeti ya Serikali, bado Serikali inawajibika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Elias Msuya ni mwandishi wa Mwananchi. 0754 897 287

Columnist: mwananchi.co.tz