Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM ya kutahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko ikiwa haki na usawa havitazingatiwa imekuja kwa wakati wake.
Kauli hiyo aliyoitoa hivi karibuni wakati akihutubia katika kongamano la kumbukumbu ya Waziri mkuu wa zamani, marehemu Edward Sokoine mjini Morogoro, inamulika uhalisia katika suala la haki na usawa wa binadamu hapa nchini.
Dk Bashiru Ally ambaye ni mwanataaluma wa sayansi ya siasa ni kama vile aliweka pembeni cheo chake cha ukatibu mkuu wa chama na kuzungumzia hali hiyo huku akieleza ugumu wa kuwaaminisha wananchi kile ambacho CCM inakihubiri.
Kwa mfano, anaeleza jinsi madereva wa bodaboda wanavyonyanyaswa na polisi, jinsi wakulima na wazalishaji wadogo wanavyokandamizwa na mamlaka za Serikali, huku akirejea misimamo wa Sokoine katika kusimamia usawa wa binadamu.
Hata hivyo, pamoja na hisia hizo, bado nachelea kusema Dk Bashiru ana kazi kubwa ya kuyasogeza mawazo hayo kwa viongozi wenzake wa CCM hadi wamwelewe.
Sina uhakika kama viongozi wa juu wa CCM wanakubaliana naye kuhusu ukandamizwaji wa haki za wanyonge.
Related Content
- BARAZA LA SALIM: Ufufuaji viwanda Zanzibar una changamoto nyingi
- Warioba asimulia ugumu wa kumpata Nyalali kwa uteuzi wa jaji Mkuu 1977
- Binti wa Trump kutoa fursa kwa wanawake Afrika
Katiba pia inatoa haki na uhuru wa watu kujiunga na vyama, kujumuika na kutoa maoni yao hadharani. Lakini vyama vya upinzani na wafuasi wao wanapata taabu kufanya siasa utafikiri ni kosa la jinai.
Siku hizi imekuwa kawaida kwa viongozi wa vyama vya upinzani kunyimwa haki ya kufanya mikutano ya hadhara kwa visingizio vya kuvunjika kwa amani wakati CCM haipati kikwazo hicho.
Tumeona watu wakiandamana kwa ajili ya kupongeza utendaji wa ngazi fulani za serikali, lakini wale wanaoandamana kuikosoa Serikali hawaruhusiwi.
Siku hizi imekuwa kawaida kusikia kauli za viongozi wa Polisi kama vile, ‘watapata taabu sana’ watapigwa mpaka wachakae’ wakati si Katiba wala sheria zinazoruhusu watu kuhukumiwa wala kuadhibiwa na vyombo vya dola badala ya mahakama.
Iko wapi haki ya kufanya siasa hapo? Uko wapi uhuru wa maoni unaotolewa na Katiba? Je, huku siyo kupandikiza chuki kwa wananchi?
Kwa sababu kama ingekuwa ni tishio la amani, basi katazo hilo livihusu vyama vyote, lakini kwa nini inteljensia ya Polisi ikandamize upande mmoja tu wa wapinzani?
Yalianza matamko ya kukataza mikutano ya hadhara na maandamano ambayo hata hayaeleweki yalitolewa kwa misingi ya Katiba na sheria zipi, lakini sasa inakwenda hadi kwenye mikutano ya ndani nako inavunjwa. Kauli ya Dk Bashiru inapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee na haikutakiwa ipotee hivi hivi, bali itupeleke kwenye kudai upya mabadiliko ya Katiba yatakayowapa wananchi nguvu ya kurasimisha haki na usawa.
Mabadiliko ya Katiba yatawaongezea nguvu wananchi kudai haki zao, tofauti na sasa tunaona viongozi wa Serikali wamekuwa na nguvu kuliko hata sheria na Katiba yenyewe.
Hata wale wasioutaka mfumo wa vyama vingi wajitoklewe kwenye mabadiliko ya Katiba waseme. Sijui kwa nini mchakato wa Katiba unaogopwa kiasi hiki, lakini ndiyo mwarobaini wa usawa na haki za binadamu nchini.