Ligi iliyo bora huwezesha kupata wachezaji bora watakaounda timu bora ya Taifa itakayoweza kufanya vizuri kimataifa na pia kupata klabu zitakazotuwakilisha vyema katika mashindano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu.
Kama tutakuwa na ligi bora itakayotuwezesha kuwa na timu bora ya Taifa na klabu bora zitakazotuwakilisha vyema kimataifa, basi mafanikio hayo yataweza kukuza na kuendeleza kiwango cha soka katika nchi yetu.
Ninaamini kabisa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanafahamu na wanaamini kuwa soka ni mchezo wenye nguvu, unaopendwa na watu wengi duniani na unaoweza kuvutia watu wengi kuwekeza katika mchezo huo.
Na ndiyo maana TFF huweka kanuni na sheria katika Ligi Kuu kwa ajili ya kuufanya mchezo wa soka uwe na ladha katika kuucheza na pia uwe na ladha katika kuuangalia na hivyo kuufanya uwe na burudani zaidi.
Sasa tatizo tulilonalo katika Ligi Kuu yetu ni kuhakikisha kanuni, taratibu na sheria za soka zinafuatwa na kuheshimiwa na pia kanuni za uchezaji wa kiungwana zinazingatiwa na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi, mashabiki, n.k.
Ndiyo, nafahamu TFF wamekuwa wakiziagiza klabu, makocha, wachezaji na waamuzi kuzisoma kwa makini kanuni za ligi na kuhakikisha zinaeleweka na kufuatwa kwa faida ya mchezo wa soka nchini, lakini sidhani kama wahusika wamekuwa wakilichukulia suala hili kwa uzito mkubwa na hapa ndiyo tatizo la chanzo cha kukosa ligi bora nchini linapoanzia.
Ni wazi kuwa klabu, makocha, wachezaji, waamuzi na mashabiki wanatakiwa kuelewa soka kama ilivyo michezo mingine yote inalindwa na sheria pamoja na Kanuni.
Bila sheria na kanuni mchezo wa soka utakuwa ni vurugu tupu, pia utakuwa hauna heshima, uadilifu, adhabu hazitatolewa na mshindi hatapatikana uwanjani kihalali bali kwa kutumia njia chafu zisizokubalika.
Kwa mtazamo wangu, klabu za soka nchini zinatakiwa kuhakikisha kanuni hizi zinaeleweka vizuri kwa wachezaji na mashabiki wake na kuzitekeleza kwa asilimia mia moja.
Ndiyo, kama wachezaji wakizielewa vyema kanuni za ligi zitawasaidia kuwa wachezaji bora zaidi na wataepuka kuadhibiwa kwa makosa ambayo yanaweza kuepukika na nidhamu yao ndani na nje ya uwanja itakuwa kubwa.
Inaeleweka kwamba TFF huwa inazifanyia marekebisho kanuni za ligi ili kuziboresha ziendane na wakati.
Mabadiliko hayo lengo lake kuu ni kuwa na ligi iliyo bora zaidi, ambayo italeta ushindani kwa timu shiriki na pia kutoa burudani zaidi kwa watazamaji.
Pia ni pamoja na kuchochea wadhamini zaidi kujitokeza kwa ajili ya kudhamini ligi na timu shiriki.
Mimi ninaamini kwamba inachokifanya TFF kwa kuweka kanuni hizi hasa za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ni kitu kizuri ila ningewashauri wahakikishe wanazisimamia kanuni hizo kwa kiwango cha juu bila kumuonea mtu haya wala upendeleo.
Pia, ninao ushauri mwingine kwa TFF ambao ni kuhakikisha tunakuwa na ligi nyingine nyingi za ngazi ya chini ambazo zitakuwa na kanuni kali za kusimamia ligi hizo.
Ninasema hiyo kwa sababu kama tutakuwa na program nzuri za kuendeleza makocha au za kuendeleza vipaji vya wachezaji katika ngazi za chini halafu hatuna ligi mbambali bora kwa ajili ya makocha na wachezaji hao.
Tutakuwa hatujafanya jambo lolote la maana kwa makocha na wachezaji hao, kwani wachezaji wanahitaji mechi nyingi za ligi bora.