Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kabla ya kuanza kilimo tafuta masoko, fahamu muda wa kuuza bidhaa

61029 KILIMO+PIC

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati mwingine unaweza kulima na kupata mazao mengi kama ilivyokuwa matarajio yako ya siku nyingi lakini ukajikuta ukipata hasara kubwa mara baada ya kuvuna mazao yako.

Hiyo ni kutokana na kukosekana miundombinu rafiki ya uhifadhi mazao baada ya kutoka shambani jambo ambalo hufanya mazao mengi kuharibika kabla ya kufika sokoni au wakati mkulima akisubiri kupata bei nzuri ya mazao yake.

Kutokana na suala hilo wadau wa kilimo wameishauri sekta binafsi kuisaidia Serikali na kuchangia katika kufanya uwekezaji wa kujenga miundombinu ya utunzaji mazao ili kuhakikisha yanayozalishwa yanakuwa katika sehemu salama.

Kufanya hivyo kutawafanya wakulima kutojutia kile wanachokifanya na kuwa na uhuru wa kusubiri bei nzuri ya mazao.

Hayo yamesemwa Mei 23 mwaka huu katika Mwananchi Jukwaa la Fikra la nne lililokuwa limebeba mada ya Kilimo, Maisha Yetu lililofanyika katika ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Kilimo Tanzania, Timothy Mmbaga amesema kabla ya kufanya uzalishaji ni vyema kuangalia masoko yaliyopo na muda wa kuuza bidhaa kwa sababu ni kitu muhimu kinachopaswa kuzingatiwa.

Pia Soma

Amesema miundombinu ya utunzaji mazao inatakiwa kuwekewa mkazo kwa sababu ili kupata masoko ya kuuza bidhaa kwa faida ni lazima kuwe na mahali pa kuhifadhi.

Mmbaga amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya jitihada za kujenga miundombinu hiyo lakini sekta binafsi pia inapaswa kuona suala hilo kama fursa na kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao.

“Ukiangalia wakati mwingine sera ya kuzuia kuuza mazao inashindikana kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya kuhifadhi chakula, ingekuwepo tungehifadhi chakula kingi.”

“Mi nimekaa wizarani kwa muda mrefu, mwaka ambao wananchi wamepata njaa tuwagawie chakula tuligawa tani 50,000 tu na hatukuzidi 100,000 sasa kama tungekuwa na miundombinu ya kuhifadhi chakula angalau tani 500,000 ingekuwa vizuri.”

“Hata tukipigwa na njaa kwa miaka mitatu au minne mfululizo bado hatutazuia watu wetu kuuza chakula kwa sababu tunajua tunacho cha kutosha na watu watakula, hivyo suala ni miundombinu ya uhifadhi.”

Akitolea mfano katika sekta ya uvuvi amesema jinsi hali ilivyo hivi sasa ni ngumu kwa mvuvi kuachia baadhi ya samaki pindi anapotoka kuvua baharini au ziwani kwa sababu anaamini kufanya hivyo kutamtia hasara.

“Akija na tenga lake la samaki ni lazima aliuze kwa sababu hana mahali pa kuhifadhi, katika upande wa bidhaa za maua na mbogamboga hatuna, (cold chain facilities) watu mpaka wanapeleka Nairobi, hizi zote tunaziona kama ni changamoto kwetu lakini hizi zote ni fursa kwa sekta binafsi kuwekeza.”

Akizungumzia kuhusu malalamiko ya kukosekana kwa masoko ya ndani amesema watengenezaji wengi wa bidhaa nchini wamekuwa wakizalisha kwa kuzingatia viwango vya nje ya nchi kuliko vile vya ndani.

“Hoteli nyingi za Tanzania zinanunua bidhaa kutoka nje ukiuliza sababu kubwa ni vigezo na ubora wa uzalishaji wetu hautoshi lakini nikawa najiuliza si kuna Watanzania wanauza mboga nje, wameweza vipi kutimiza vigezo na tunauza katika supermarket nje tena tani nyingi.”

“Sasa tunajiuliza kama tuliweza kukidhi vigezo vya kuuza katika soko la nje, supermarket na hoteli kubwa zinazotambulika duniani tumeshindwaje kutumia mbinu sawa kuziuzia hoteli za ndani ya nchi.”

“Tujiulize, lakini ukweli ni kwamba tuna uwezo, japo hatuna vifaa vya kutosha lakini kama tumeweza kuingia soko la Ulaya tunaweza kuingia katika soko la hoteli za ndani lakini kuna kitu kinakosekana hapa, tunalikandamiza sana soko la ndani,”

“Tunaweza kutumia akili na kupunguza utumiaji wa bidhaa za nje katika mahoteli yetu ambao hadi sasa ni asilimia 95 ya bidhaa zote zinatoka nje wakati na sisi tunasafirisha kwenda nje bidhaa hizo zinazoingizwa.”

Akizungumzia suala la wakulima wengi kulalamikia kutopata mikopo katika benki ili waweze kukuza uzalishaji na kufikia masoko ya nje, meneja mwandamizi kutoka benki ya NMB anayeshughulikia masuala ya kilimo, Carol Nyangaro amesema yapo masharti ambayo wanapaswa kuzingatia kabla ya kufanya hivyo ikiwemo kuandaa dhamana.

“Hii ni kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na miongoni mwa masharti hayo ni kujisajili kupitia wizara ya viwanda kupitia Brela ili uwe kampuni au mtu binafsi, uwe mjumbe wa bodi ya wadhamini, uwe katika chama cha ushirika na kuandaa dhamana.” Amesema Nyangaro

“Unapokopa benki na kupewa asilimia 100 ya mahitaji ya hiyo pesa kwa mfano shamba lako linahitaji Sh3 milioni na hautaki kuweka dhamana hii inamaanisha kuwa mradi huo unakuwa wa benki na si wako tena.”

“Umiliki wa kutaka kushiriki katika uwekezaji inatakiwa uwe na dhamana na uwekezaji lakini pia ni vizuri kuwa na mahesabu yaliyokaguliwa,” amesema.

Akizungumzia namna benki zilivyogawana katika utoaji wa mikopo Nyangaro amesema benki za maendeleo zina jukumu la kuhimiza uwekezaji wa kimaendeleo ikiwemo kilimo cha umwagiliaji na miradi inayochukua muda mrefu.

“Kwa dizaini yao na sharia zao inawaruhusu wao kujielekeza huko na wasipofanya tutawauliza kwa nini hamfanyi kwa sababu ndiyo hasa jukumu lao.”

“Kwa Benki za biashara jukumu lake ni kuhimiza uwekezaji usiokwenda mbali sana,” amesema Nyangaro.

Columnist: mwananchi.co.tz