Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KUTOKA LONDON : Watanzania wengi bado hatuelewi nini saladi na faida yake kiafya

39849 Fredy Macha KUTOKA LONDON : Watanzania wengi bado hatuelewi nini saladi na faida yake kiafya

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Labda tungesema ni Uafrika.

Lakini sivyo. Miezi michache iliyopita rafiki yangu fulani, Mtanzania, aliitembelea Msumbiji kikazi akanieleza kule ni kawaida kabisa kula chakula na saladi.

Akasema :“Nilishangaa maana Msumbiji misosi kila mahali inakuja na sahani kubwa la saladi. Tena tamu sana...sisi Wabongo bado tunadhani ni jambo la Kizungu na matajiri.”

Rafiki yangu hakukosea.

Mwaka jana nilifanya utafiti wa haraka haraka. Nilianzia watu wa makamo na wazee. Mmoja aliyepitisha miaka sabini akapayuka : “Mimi bwana sikudanganyi. Kula majani si desturi yangu. Miaka yote hii nimekula nyama na ndizi zangu na ugali wangu na samaki wangu niacheni hivi hivi. Majani mabichi hayanikai. Tuwaachie mbuzi tu!” Akacheka.

Tuendelee.

Kuna Mtanzania mmoja maarufu alitembelea nchi za Ulaya. Siku moja akaalikwa mlo na marafiki wa Kizungu. Alipiga picha kile chakula akatundika Instagram. Maoni ya baadhi ya wapambe yalichekesha.

Neno “majani matupu” lilitumiwa sana. Tena kwa kejeli. Tuendelee.

Vijana wanne waliozaliwa baada ya mwaka 1990 walinitatiza zaidi. Wote hawakuelewa kabisa hilo neno saladi – ambalo asili yake ni Kilatini – Salata (Kitaliano) au Salade ( Kifaransa). Baadaye lilizagaa. Wahindi walivumbua mtindo wao wa saladi waliyoita cachumber- ambayo Waswahili tuliigeuza kuwa “kachumbari”...

Sasa nilipowaeleza kuwa saladi ni kama kachumbari wakadhani saladi ni hiyo kachumbari. Lakini ukweli, kachumbari ni aina moja tu ya saladi. Walichokijua ni vitunguu, nyanya na limau. Mmoja akatathmini kuwa huenda kishaiona hiyo saladi – “ katika hafla na sherehe au harusi...”

Kwa hiyo saladi hapo inahusishwa na utajiri na sikukuu tu, kumbe hakika saladi yatakiwa iliwe pamoja na mlo wa kila siku.

Kifupi mtu wapashwa kula vyakula vyenye virutubishi aina nne kila siku.

Wanga (ugali, viazi, wali, nk) protini (nyama au mboga za kupikwa), vitamini na madini (mbegu, matunda, mboga mbichi). Tunapozungumzia mbegu tuna maana korosho, karanga, mbegu za maboga nk. Hizi zatakiwa mbichi si kukaangwa au kuwekwa chumvi.

Suala la chumvi na pilipili ni suala jingine linalotudhalilisha watu weusi Afrika na Ughaibuni. Mtu mweusi huendekeza ladha ya chakula kuliko afya. Mathalan saladi itajazwa chumvi. Au sukari nyingi katika kila kitu hadi chapati. Sukari si kitu kizuri.

Je tunazungumzia nini hapa?

Ulaji chakula unatakiwa uwe na saladi. Wapo wanaosema ni aghali. Lakini mboga za majani si aghali Afrika. Mboga za majani zimejazana. Nyanya, tango, karoti, mbegu, nazi mbichi (si kuipika kuila hivyo hivyo), majani majani ya aina mbalimbali – brocoli, nk. Mseto huu wa majani na mbegu waweza kubadilishwabadilishwa. Leo, nyanya tupu ...kesho karoti , kesho kutwa karoti na matango nk. Na saladi kidesturi huliwa dakika chache kabla ya mlo.

Saladi yaweza kuwa matunda pia. Mfano mzuri ni maziwa mtindi kwa ndizi kisukari. Au maziwa mtindi kwa nazi iliyokatwa katwa vipande vipande na kuchanganywa na korosho (mbichi) nk.

Zipo Saladi za aina nyingi.

Faida yake ni madini na vitamini. Hujenga mifupa, viungo, kurekebisha damu, kuondoa unene, kujenga kinga maradhi, na kifupi msingi mahsusi wa miili yetu. Milo tuliyozoea yaani protini (nyama) na wanga...faida yake ni ujenzi wa jumla na nguvu tu basi. Havitoshi.

Na ndiyo sababu wastani wa uhai wa Mwafrika seuze Mtanzania ni kati ya 40 hadi 60. Ukipitisha unaitwa mzee ilhali wenzetu wanafikisha tisini kuendelea.

Columnist: mwananchi.co.tz