Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KONA YA MALOTO: Kusema wanateuliwa kwa fadhila ni kutowatendea haki

Mon, 7 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watu wanaojitokeza kumsifia au kumtetea Rais John Magufuli, kiutendaji au kwa falsafa yake ya uongozi, huambiwa wanatafuta uteuzi. Wasemaji wa hayo mitandaoni na mitaani hutengeneza taswira kwamba kumsifia Rais Magufuli ni tiketi ya kupata cheo.

Kuna ukweli gani kwamba Rais huteua viongozi kwa sababu ya kumsifia, kujipendekeza au kwa vigezo anavyoona vinakidhi matarajio yake? Nimepata nafasi ya kujiuliza swali hilo, kisha nikaona nijenge tafakuri.

Nikajiuliza, Profesa Joyce Ndalichako alimsifia wapi Rais Magufuli ndipo akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu? Nikapitia pia majina ya watu ambao muda mrefu humpa sifa nyingi Rais lakini mpaka leo hawajateuliwa cheo chochote.

Profesa Kitila Mkumbo mpaka anateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji alikuwa mkosoaji wa Serikali ya Rais Magufuli, lakini akateuliwa. Hiki ni kipimo kwamba si kila mwenye kumkosoa Rais, hawezi kupata nafasi. Kama ndivyo, Kitila angeusikia ukatibu mkuu wa wizara kwenye bomba.

Aliyekuwa Katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba tangu alipohamia CCM ni miaka miwili imepita anaandika makala nyingi za kumsifia Rais Magufuli, lakini mpaka leo hajateuliwa cheo chochote. Tena wengine humsimanga na kumuuliza kwa kejeli, “hujateuliwa tu?”

Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alikuwa mkosoaji wa Serikali ya Rais Magufuli. Alipohamia CCM, hakuchukua muda mrefu kuwa mkuu wa Wilaya ya Tunduru.

Pia Soma

Advertisement
Mpaka hapa unaweza kuona kumbe kumsifia Rais si kigezo cha kupata cheo bali zipo sifa za ziada huzitazama na kuzizingatia.

Mjadala wa aina hiyo ulishika nafasi wiki iliyopita baada ya Dk Benson Bana kuteuliwa balozi hivi karibuni. Kwamba cheo alichopata ni matunda ya kumsifia Rais Magufuli kwa muda mrefu.

Wapo wengi wanaodaiwa hivyo. Tangu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alipoondolewa katika nafasi yake, amekuwa mtetezi mno wa Rais Magufuli.

Hakuna mwana CCM ambaye hupambana na hoja za Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) mitandaoni kama Mwigulu.

Kila Zitto akijenga hoja dhidi ya Rais Magufuli, Mwigulu huijibu. Iwe ya kiuchumi, kiutawala au utekelezaji wa miradi. Zitto akieleza anaoona udhaifu, Mwigulu husifia kwa kusema uimara wake.

Pia yupo George Simbachawene. Huyu alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi ambaye mwaka juzi, alijiuzulu kwa agizo la Rais kutokana na kashfa ya kutowajibika ipasavyo alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini. Baada ya kung’oka alibaki kimya.

Mwaka huu, tena hivi karibuni, ameteuliwa tena na Rais Magufuli kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira akichukua nafasi ya January Makamba.

Kama kigezo cha uteuzi kingekuwa ni kumsifia Rais Magufuli, bila shaka Mwigulu angerejea katika Baraza la Mawaziri kabla ya Simbachawene.

Hiki ni kipimo kingine kuwa kumsifia peke yake Rais Magufuli si hoja ya uteuzi. Bila shaka Rais Magufuli ana jicho lake.

Tumtazame Juma Nkamia, mbunge wa Chemba (CCM). Huyu mbona ana hoja yake ya muda mrefu kuhusu kumwongezea Magufuli muda wa kukaa madarakani? Nkamia anasema miaka mitano ni michache. Tangu alipoanza hoja hiyo, Rais Magufuli ameshabadilisha mawaziri na manaibu mara kadhaa, lakini Nkamia yupo palepale. Hajateuliwa!

Msingi wake upo kwenye matawi matatu; kwanza watu waheshimu jicho la Rais Magufuli. Kusema wenye kujipendekeza, wanaomtetea au kumsifia ndio huteuliwa, ni kumvunjia heshima. Kwamba huwa hazingatii vigezo au sifa anazokusudia, bali akikuona unampamba, basi wewe ndiye kiongozi.

Tawi la pili ni watu wafanye kazi kwa weledi na kujenga nchi katika maeneo yao, kwa vipawa walivyonavyo. Pale ambapo Rais anastahili kusifiwa apewe haki yake na ikibidi kukosolewa, basi watu wafanye hivyo kwa haki na bila kutia chumvi.

Hivi sasa kuna watu mitandaoni wana moto sana. Liwake jua inyeshe mvua, wao wanasifia tu, ni kweli kabisa wamelemazwa na maneno kwamba Rais akikuona unamsifia ndio atakuteua. Hakuna kuongopeana kama huko.

Hivi kuna mtetezi wa Rais Magufuli mitandaoni kama William Malecela ‘Le Mutuz’ ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu na makamu wa kwanza wa Rais, John Malecela?

Mbona mpaka Rais Magufuli anaelekea mwaka wake wa mwisho katika muhula wa kwanza hajawahi kumteuliwa nafasi yoyote ya uongozi? Watu wasijitoe ufahamu kusifia kila kitu kwa sababu ya kutegemea cheo, wafanye hivyo kwa haki.

Tawi la tatu ni watu wanapomsifia Rais Magufuli, wengine waheshimu mawazo yao. Si kuwasema kuwa wanajipendekeza ili wapate vyeo. Katika nchi ya kidemokrasia, uhuru wa mawazo ndiyo oksijeni ya demokrasia.

Kama mtu kwa haki ameona anakunwa na jinsi Rais Magufuli anavyofanya kazi, aachwe asifie. Kama ambavyo mwingine akiona Rais Magufuli ana maeneo hayafanyi kazi ipasavyo, aruhusiwe kukosoa, mradi asitukane wala kuvunja sheria.

Columnist: mwananchi.co.tz