Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KONA YA HOJA: Ruge ajengewe mnara, makumbusho ndogo

45861 Mtatiro KONA YA HOJA: Ruge ajengewe mnara, makumbusho ndogo

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati taifa zima likizizima kwa kuondokewa na mjasiriamali na mfundaji mahiri wa vijana Ruge Mutahaba, nimekaa na kutafakari sana kwa nini hakuwa mshauri rasmi wa Rais juu ya masuala ya vijana? Unajua, watu wenye vipaji maalumu vya kuleta matokeo kwa jamii wanapaswa kusogezwa zaidi karibu na jamii pana, kuliko kuendelea kuleta uchanya kupitia mipango ya sekta binafsi.

Wakati bado nahangaika na tafakari hiyo, rafiki yangu mmoja ameniambia, ni bora Ruge hakuwa chini ya Rais moja kwa moja, hapa tunaongelea marais kama Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli ambao wamekuwa madarakani kipindi ambacho Ruge alikuwa akifanya kazi kubwa ya kuhamasisha vijana waamke na kulipigania taifa kwa kutumia vipaji na uwezo waliopewa na Mungu. Hoja yake ni kuwa huenda alihitaji sekta binafsi kusimamia mawazo yake kwa haraka. Nakubaliana na mawazo ya rafiki yangu huyu pia.

Malezi bora ni msingi

Nilikuwa na mawazo mengine zaidi, kwamba cheo cha ubosi ambacho alipewa na watu waliomzunguka, kama jina lake la utani, kingelimfaa zaidi. Nafsi nyingine inaniambia Ruge alikuwa ni zaidi ya bosi, maana ofisi nyingi zinao mabosi, mabosi ambao hawana ubunifu na uthubutu aliokuwa nao. Nilipopata nafasi ya kuzungumza na kaka yake, msibani Mikocheni, nilimwambia, “hongereni, mlilea binadamu mwenye roho kubwa sana, familia nyingi hazina vijana kama Ruge, yeye ni zao la malezi ya familia yenu”.

Sote tunatoka kwenye familia mbalimbali, na tunajua kuwa familia ambazo zinatoa malezi bora kwa watoto, ndizo familia zinazozalisha watoto wenye uwezo mkubwa zaidi, wenye fikra za hali ya juu na wenye uthubutu. Malezi bora siyo utajiri, ni ile hali ya wazazi na walezi kuwa na uwezo wa kumjenga mtoto wao na kumpa uwezo wa kujiamini, kuthubutu, kujiamini, kutenda wema na kufanya mambo ambayo yanaleta chachu na mapinduzi kwenye jamii.

Hebu fikiria mambo haya

Ni nani alitarajia kuwa muziki wa Kicongo utakimbizwa na kuondolewa hapa Tanzania kwa kasi kubwa kama ilivyotokea? Ni nani alitarajia kuwa vyombo vya habari na hasa redio na televisheni vitageuka kuwa chanzo cha elimu kubwa ya bure kwa vijana kuthubutu na kutumia vipaji vyao? Ni nani alitarajia kuwa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva) utageuka kuwa ajira inayowapa mamia ya vijana mamilioni ya fedha na maisha ya hali ya juu? Ni nani alifikiria kuwa muziki wa Bongo Fleva utasambaa katika bara lote la Afrika na duniani?

Haya yote ambayo mwanadamu yeyote aliyekuwepo mwaka 1995 angeliyaona ni ndoto ngumu, kwa Ruge yalikuwa masuala halisi, yalikuwa ni ndoto halisi inayotekelezeka.

Leo unaweza kuona yanafanyika matamasha makubwa sana ya muziki na utoaji wa elimu kwa vijana, matamasha kama fiesta, Wasafi Festival na mengine mengi. Yote haya yamewezekana leo kwa sababu Ruge alithubutu kufungua macho na akili za vijana. Hapa sijazungumzia fursa za kijasiriamali na elimu ya maendeleo ambayo kina mama na vijana wameipata na wakifikishiwa bure. Ruge ameondoka na hatuna cha kumdai tena.

Kazi kubwa iliyoko mbele

Ruge amelea vijana wengi na kuwafunda, amewafundisha kazi wengi, amewafundisha uthubutu na mbinu wengi, hakuenda peke yake! Walau huyu ni binadamu ambaye aliyaishi maisha halisi kwa maana ya maisha ambayo mwanadamu anapaswa kuishi. Ruge aliwarithisha wengine yale aliyokuwa anayajua, hakuacha kitu. Ametuachia wana mikakati wa vijana wengi, wafundaji wengi, wasanii wengi, wanamuziki wengi, redio nyingi zenye vipindi bora, televisheni nyingi zenye maudhui ya vijana. Tutamlipa nini Ruge?

Taasisi zote ambazo zilifanya kazi na Ruge lazima zikae chini na kwa haraka zianze kufanyia kazi mafunzo yake na maono yake, na kwa sababu aliacha miradi mkakati mingi iliyokuwa bado kwenye ngazi ya fikra, waliokuwa karibu naye waibue mikakati hiyo tusonge mbele, tufumbe macho, tuamini kuwa sisi ndiyo Ruge na tuchukue nafasi yake. Taifa letu linahitaji ari na morali ya Ruge visife, alianza vizuri na amemaliza vizuri, hakuishia katikati kwa sababu safari yake imefika mwisho.

Huu ni mtihani kwa familia yake, serikali, kampuni zake na washirika wake. Tuanze kukusanya kila kazi alizofanya Ruge, zisipotee. Tuzisake kokote kule ziliko, tumtengenezee makumbusho, hata ya chumba kimoja ambamo vijana wajao mbeleni watajifunza kuwa maendeleo ya vijana wa taifa hili yaliwahi kutiwa chachu na mtu anayeitwa Ruge Mutahaba.

Serikali iruhusu mnara ujengwe mahali popote pale, hasa Dar es Salaam, mnara wa Ruge! Mnara huu uwe ishara ya kujali mchango wa vijana wa Kitanzania waliowahi kujitolea kupigania maendeleo ya taifa letu. Mnara huu uwe uthibitisho kuwa taifa linathamini na linapenda vijana wengi zaidi wajitokeze na kulipigania, na kupigania maendeleo yake.

Wakati tumemzika Ruge, vijana wote tujifunze mambo makubwa aliyokuwa nayo; wema, uthubutu, mbinu na uwezo wa kutumia vipaji vyake. Tangulia Ruge, sisi tunafuata!

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtaalamu Mshauri wa Miradi, Utawala na Sera. Pia Mtatiro ni Mtafiti, Mfasiri na Mwanasheria. Simu; +255787536759 \ Barua Pepe; [email protected])



Columnist: mwananchi.co.tz