Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KILIMO MAISHA YETU: Wananchi walivyoishauri Serikali kukuza kilimo

60246 Pic+wananchi

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Washiriki mbalimbali wa Jukwaa la Fikra la Mwananchi wameishauri serikali juu ya namna bora ya kukuza sekta ya kilimo nchini ikiwa ni pamoja na kuanza kufundisha kilimo tangu elimu ya msingi na kuwekeza katika tafiti za kilimo.

Hayo yamesemwa katika jukwaa hilo la nne la Fikra la Mwananchi lililokuwa limebeba mada ya ‘kilimo, maisha yetu’ lililofanyika katika ukumbi wa Kisenga Mei 23, 2019.

Akichangia hoja katika mjadala huo, Honest Mseli kutoka Ansaf amesema zamani kilimo kilianza kufundishwa shuleni na zilikuwepo shule maalumu za kufundisha michepuo ya kilimo, lakini sasa hazipo.

“Elimu yetu ya Tanzania imekuwa ikiwajenga watoto kuwa madaktari, wahasibu, lakini ghafla wakikua tunataka wawe wakulima, ni muhimu tukaanza hivi vitu shuleni, mimi nimesoma shule ya mchepuo wa kilimo lakini hivi sasa hazipo nafikiri ni vyema tukarudi kule chini.”

“Lakini ni wangapi huwa tunakwenda kuwahamasisha vijana kujihusisha katika kilimo, mashirika ya kilimo ni lazima twende katika vyuo kutafuta vijana wakiwa bado wachanga kwa sababu wanasema samaki mkunje angali mbichi.”

“Vijana wanahitaji vitu vitatu ambavyo ni mtaji, mawazo pamoja kuhamasishwa kabla hatujatawanyika, hivyo tuwafuate vyuoni kabla hawajatawanyika, itakuwa ni ngumu.”

Pia Soma

Amesema ni vyema zile adhabu za zamani zilizokuwa zikitolewa vyuoni ikiwemo kuchunga ng’ombe na kulima kubadilishwa ili kuwaondolea ile dhana ya kuwa kilimo ni adhabu.

Mshiriki mwingine, Joseph Nkata amesema ili kupata kilimo chenye tija ni lazima kuwekeza katika tafiti na Serikali kutenga fedha kwa ajili ya suala hilo.

“Watu wengi wanatamani kuwekeza katika kilimo, lakini hakina tija, ujuzi ni mdogo, teknolojia ni ndogo hivyo ni ngumu sana kwa vijana kuwekeza katika upande huo.

“Tunaiomba Serikali iwekeze nguvu zote katika kilimo kupitia tafiti, hivi karibuni tumeona taasisi ya Repoa ikizindua vitabu vya tafiti tunashukuru sana, lakini Serikali inapaswa kuongeza nguvu ili kupatikana ujuzi na teknolojia mpya zitakazotafsiriwa katika sera za umma.”

“Na baada ya kufanya hivyo visibaki tu kwenye makabrasha bali viwafikie wakulima na kufanya hivyo tutaongeza tija na uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa viwanda na hili lisiishie mjini na vyuoni bali kwa wakulima pia maeneo ya vijijini.”

Raphael Ngowi amesema zamani kulikuwa na vyuo vidogo vya wakulima ambavyo vilikuwa vikitoa elimu ya shamba darasa huku maofisa ugani wakifika kwa wakulima kwa wakati jambo ambalo sasa halipo.

“Waziri, kuna vitabu vitatu ukavifanyie kazi, Mkukuta 1, Mkukuta 2 na Mkurabita, wataalamu wamefanyia kazi na wameeleza vizuri na vikifanyiwa kazi kwa vitendo vitatutoa hapa tulipo, tufanye kazi kwa vitendo tukirudi katika makabati hatuna haja ya semini tena wala warsha,” amesema Ngowi.

“Mkukuta 1, Mkukuta 2 na Mkurabita utakusaidia sana katika harakati zako za kurudisha kilimo kile cha miaka ya 1970 ambacho jembe la mkono lilifanya meli za bandarini ziweze kupakia pamba, leo tuna matrekta tunashindwa kuzalisha meli zinakuja zinapakua makontena zinaondoka kupakia mizigo nchi nyingine sisi hatuna cha kupakia.”

“Hela yetu imeporomoka kwa sababu kilimo chenye nguvu hakuna, (shilingi) mia moja ilikuwa na nguvu kwa sababu ya kilimo ambacho kinaenda sambamba na viwanda sera ambayo ni sera ya mwaka 1967 iliyochukuliwa tu kabatini,” amesema Ngowi.

Mohammad Mchiwa amesema vijana wengi wamekuwa wakilalamikia Serikali kuwa haiwapi mwamko bila kujua kuwa ukikaa kuilaumu Serikali siku zote hauwezi kufanikiwa na badala yake ni vyema kujifunza kwa watu wa ndani waliofanikiwa.

“Atakuambia ni mbinu gani zilizomfanya akafanikiwa na aliyeshindwa ni kitu gani kimemfanya ashindwe, kikubwa ni vijana kujitambua na kuthubutu kuingia katika masuala ya ujasiriamali,” amesema Mchiwa.

Kutoka shirika la bima Bumaco, Ekande Kwayu amesema kutokana na uchache wa maofisa ugani ni vyema vyema Serikali kuwapunguzia majukumu kutoka kusimamia kijiji hadi vyama vya ushirika.

“Unaweza ukafanya ofisa ugani akawa siyo kwa ajili ya kijiji bali kwa ajili ya vyama vyote vya ushirika, kuwe kuna mkakati kila chama cha ushirika wa mazao au mambo ya kilimo kuwe na maofisa ugani waliofundishwa ili waweze kuwafundisha wale wanachama wao,” amesema Ekande.

Wini Bashagi kutoka baraza la mchele Tanzania amesema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo mvua kunyesha na jua kuwaka kuathiri wakulima, kuwa na bima za mazao ni jambo la msingi.

“Naishauri Serikali pamoja na mashirika ya bima waanze kuwahamasisha wakulima ili waanze kukata bima za mazao ili kuzifanya benki kushindwa kutoa mikopo,” amesema Wini

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rose Salingwa amesema maofisa kilimo wawe na wasimamizi au wawakilishi ili kuondoa vikwazo wanavyokutana navyo wakulima ikiwemo kupoteza mifugo kwa sababu watu hao husimamia eneo kubwa la makazi ya watu na hawana usafiri wa kuwawezesha kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa uharaka.

Columnist: mwananchi.co.tz