Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KESI YA KIHIYO UCHAGUZI MKUU: Jaji Mapigano adai CCM ilihonga Temeke-12

90307 Kihiyo+pic KESI YA KIHIYO UCHAGUZI MKUU: Jaji Mapigano adai CCM ilihonga Temeke-12

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika hukumu hiyo Jaji Dan Mapigano alisema CCM na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Temeke kwa tiketi ya chama hicho, Ally Ramadhani Kihiyo, walitoa rushwa kuwashawishi wapiga kura katika uchaguzi uliompa ushindi Kihiyo.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Mapigano alisema “imethibitishwa mahakamani” kuwa CCM na mgombea wake walitoa rushwa kwa wapiga kura. Alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa walalamikaji na wa utetezi unaonyesha kitendo cha wananchi kupewa pilau, kanga na fedha ilikuwa ni kutoa hongo kwa lengo la kuchaguliwa.

Hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa 3 na dakika 20 ilieleza kuwa wananchi wa kata ya Bulyaga jimboni humo walipewa pilau kwenye mkutano ambao Kihiyo kabla ya kuhutubia aliwaambia huo ni mwanzo tu na akichaguliwa watafaidi zaidi.

Jaji alisema shahidi wa nne upande wa walalamikaji, Peter Odhiambo, na shahidi wa 16, Selina Ngalipeka, waliithibitishia mahakama juu ya vitendo vya rushwa ambapo maji, kanga na fulana ziligawanywa kwa lengo la kumchagua Kihiyo.

Mbali na tuhuma hizo za rushwa pia Jaji alieleza kuwa sheria za uchaguzi zilikiukwa, wananchi katika kata za 15, 14 na Mtoni Saba Saba walionyeshwa picha za video zilizoelezea mauaji ya Rwanda na Burundi, hali ambayo iliogofya watu.

Jaji alisema pamoja na mashahidi kutoeleza kama picha hizo za video zilikuwa na maana ya kutochaguliwa vyama tofauti na CCM, kutokana na hotuba zilizotolewa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa Philemoni Sarungi; Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Thadeus Kasapila na Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke wa chama hicho, Abdallah Chenja, katika mikutano ya kampeni ilielezea kuwa vyama vya upinzani vikichaguliwa vitaleta vita kama Rwanda na Burundi.

Jaji Mapigano alikataa hoja kuwa kipindi cha kuomba amani kilichokuwa kikionyeshwa na kituo cha televisheni cha ITV kilichangia kuvuruga amani jijini kutokana na kuonyesha picha za vita kabla ya uchaguzi na kusitishwa baada ya muda huo.

Alisema kuwa kituo hicho kina utaratibu wake wa kuonyesha vipindi na kwamba kwa wakati huo yawezekana waliona waielimishe jamii kwa kukumbusha suala la kuendelea kwa amani nchini.

Pia Jaji Mapigano alisema haki nyingine iliyokiukwa katika uchaguzi huo ni maneno ya viongozi wa CCM kuwa chama cha NCCR-Mageuzi ni chama cha Wachagga, hatua aliyoielezea kuwa ni ukiukwaji wa sheria kwani Tanzania hatuna ukabila japo kuna makabila.

Kuhusu madai ya kuwapo askari wengi katika uchaguzi wa marudio wa Novemba 19, 1995, Jaji Mapigano alikubaliana na hoja iliyotolewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ditopile Mzuzuri, kwamba Serikali inawajibika kulinda usalama wa raia kukiwapo hali ya wasiwasi.

Kuhusu suala la Kihiyo kughushi cheti, Jaji Mapigano alimwagiza Mwanasheria wa Serikali amfungulie Kihiyo mashtaka mapya katika Mahakama ya Kisutu kujibu tuhuma hiyo. Wakati wote wa kusikilizwa shauri hilo, Mwanasheria wa Serikali alikuwa Julius Malaba.

Alisema kama mashtaka hayo yatafunguliwa, Kihiyo atakabiliwa pia na tuhuma za kusema uongo mahakamani chini ya kiapo, kuwadanganya wananchi wa Temeke kuwa ana vyeti vya uhandisi na hatimaye kuwa mwakilishi wao bungeni katika njia isiyo halali.

Kuhusu kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo, Jaji Mapigano alibatilisha uchaguzi huo na kumtaka Kihiyo kuulipa upande wa utetezi gharama zote za kuendesha kesi hiyo.

Baada ya kiti cha ubunge wa Jimbo la Temeke kutangazwa kuwa wazi kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wake, Ally Ramadhani Kihiyo, aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1995 kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, Augustine Lyatonga Mrema, Jumapili ya Julai 7, 1996 alitangaza rasmi uamuzi wake wa kugombea ubunge katika jimbo hilo na kusema kwamba anataka kupata tiketi ya kuikosoa Serikali kupitia vikao halali.

Mrema aliyasema hayo wakati akifungua kongamano la siku moja la wanawake wa NCCR-Mageuzi lililofanyika katika ukumbi wa Imasco Center, Temeke jijini. Alisema hawezi kuikosoa CCM akiwa mitaani. Mrema alipitishwa na chama chake kugombea kiti hicho.

Kwa upande mwingine, Julai 7, 1996 Kamati Kuu ya CCM ilimteua Abdul Omari Mtiro maarufu kwa jina la Cisco-Kid, kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Kwa upande mwingine, Julai 10, Richard Hiza Tambwe, ambaye mwaka uliotangulia aligombea kiti hicho kupitia NCCR-Mageuzi, aliamua kugombea kiti hicho kwa mara nyingine kupitia CUF, huku NCCR ikisema kuwa hatua hiyo ya Tambwe kugombea ubunge kupitia CUF imemfukuzisha uanachama moja kwa moja.

Uchaguzi huo ulifanyika Jumapili ya Oktoba 6, 1996. Matokeo ya uchaguzi huo (idadi ya kura ikiwa katika mabano) yalikuwa kama ifuatavyo:

Augustine Mrema kwa tiketi ya NCCR (54,840) ambazo ni sawa na asilimia 59 ya kura zote, Abdul Cisco Mtiro kwa tiketi ya CCM (33,113) ambazo ni sawa na asilimia 36 ya kura zote, Hiza Tambwe kwa tiketi ya CUF (3,324), Alec Che Mponda kwa tiketi ya TPP (515) na Mege Omar kwa tiketi ya UMD (422).

Wengine ni Samson Msambara wa Chadema (217), Legile Msonde wa UPDP (162), Ndembe Abdallah wa Pona (120), Rashid Mtuta wa NRA (114), Brighton Nsanya wa NLD (69), Shabaan Matembo wa UDP (67), Rachel Mutayoba wa TLP (62) na Paul Mtema wa Tadea (54).

Lakini kutokana na kutoelewana kati yake (Mrema) na viongozi wa chama chake na wabunge wenzake wa NCCR, mwaka 1999 Mrema alijiuzulu ubunge wa Temeke na kuamua kuhamia TLP, chama ambacho anakiongoza hadi sasa akiwa mwenyekiti.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliitisha uchaguzi mwingine, safari hii pia Mrema alijiandaa kugombea kwa tiketi ya TLP lakini Mahakama Kuu ya Tanzania ilizuia asigombee baada ya NCCR kumuwekea pingamizi.

Jumapili ya Julai 11, 1999 uchaguzi wa marudio ulifanyika na matokeo yalilirudisha jimbo la Temeke mikononi mwa CCM baada ya John Kibasso wa kupata ushindi wa kura 27,090, Tambwe Hizza wa CUF akiwa wa pili kwa kura 25,742, Abbas Mtemvu wa TLP akipata kura 14,701 na Suleiman Hegga wa NCCR alipata kura 866.

Uchaguzi mkuu uliofuatia, Oktoba 2000, ulishuhudia ushindani mkubwa katika jimbo la Temeke. CUF ambacho kilimsimamisha Tambwe Hizza na kupewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini mgawanyiko wa vyama vya upinzani ulisababisha mgombea wa CCM John Kibaso apate jumla ya kura 60,872 huku vyama vinane vya upinzani kwa ujumla, ikiwamo CUF, vikipata kura 89,665, ambazo ni nyingi kuliko za CCM, lakini vilibwagwa kwa kukosekana umoja baina yao.

Columnist: mwananchi.co.tz