Uchaguzi Mkuu wa kwanza uliohusisha vyama vingi vya siasa ulifanyika Oktoba 29, 1995. Hata hivyo matokeo ya uchaguzi katika majimbo yote ya Dar es Salaam yalifutwa na hivyo uchaguzi mwingine kwa majimbo hayo ukapangwa kufanyika Novemba 19 ya mwaka huo.
Huu ulikuwa ni uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi tangu nchi iliporejea kwenye mfumo huo mwaka 1992.
Baada ya uchaguzi kesi mbalimbali zilifunguliwa za kupinga ubunge wa baadhi ya wabunge. Mojawapo ni ile ya kupinga ushindi wa mbunge wa Temeke, Ally Ramadhani Kihiyo. Katika hatua hii tutaendelea kuona mashahidi walivyotoa ushahidi wao. Endelea…
Jumatatu ya Aprili Mosi, 1996 kesi dhidi ya Ramadhani Ally Kihiyo iliendelea Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Dan Mapigano. Kesi hiyo ilifunguliwa na waliokuwa wagombea wa NCCR-Mageuzi, Richard Tambwe Hiza na wa Chadema, Beatrice Mtui na wananchi wengine wanne.
Katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo siku hiyo ilidaiwa kuwa mbunge wa Temeke, Ally Ramadhani Kihiyo alikuwa akiwaeleza wananchi wa jimbo hilo kuwa wenye matatizo ya sukari wawasiliane na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili awasaidie.
Mbunge huyo pia ilidaiwa alikuwa akigawa maji kwa kutumia gari katika mikutano yake ya kampeni na alikuwa akiwaeleza wananchi kuwa wakimchagua hawatakuwa na tatizo la maji tena.
Akitoa ushahidi wake siku hiyo, shahidi wa nne wa upande wa walalamikaji, Sospeter Odhiambo, aliieleza Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kuwa katika mikutano yake ya kampeni, aliyekuwa mgombea wa CCM ambaye ndiye mbunge wa jimbo hilo wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani, alikuwa akiwaeleza wananchi kuwa atawasaidia kutatua matatizo yao na kwamba wale wote wenye shida ya sukari wawasiliane na ofisi za CCM.
Akihojiwa na wakili wa upande wa walalamikaji, Dk Masumbuko Lamwai mbele ya Jaji Mapigano, shahidi huyo alisema kuwa Mbunge Kihiyo aligawa maji kwa wakazi wa eneo la Keko Toroli na kutoa ahadi ya sukari eneo la Keko Magurumbasi.
Shahidi huyo alisema pamoja na Kihiyo kutoa ahadi hizo, alikwenda kwenye mikutano ya kampeni na gari lililokuwa na maji na kusema kuwa wakimchagua wananchi wa sehemu hiyo hawatakuwa tena na shida ya maji kwani hapo awali yeye (Kihiyo) alikuwa mhandisi wa Nuwa (Mamlaka ya Maji Mijini iliyoanzishwa mwaka 1981).
Shahidi Odhiambo alisema kutokana na tatizo la maji katika eneo hilo, kampeni za aina hiyo zilichangia kuvuruga uchaguzi kwa sababu wananchi walihitaji sana mtu anayewaahidi kuwa atawatatulia matatizo yao.
Shahidi huyo alisema pia kwamba pamoja na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Temeke, Abdallah Chenje, kuwaeleza wananchi kuwa wasimchague mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema, kwa sababu ni muuaji, kipindi killichokuwa kinaonyeshwa kupitia kituo cha televisheni cha ITV kilichohusu mauaji ya Rwanda na Burundi pia kilichangia kuvuruga uchaguzi huo.
Alidai pia kwamba vitisho vilivyokuwa vikitolewa na CCM na baadaye wananchi kuona kwenye televisheni matukio ya Burundi na Rwanda kiliwatisha sana wananchi na hivyo wakaingiwa na hofu na kisha wakaogopa kupigia kura vyama vya upinzani.
Odhiambo aliiambia mahakama kuwa mawakala wote na wasimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo hawakupata nafasi ya kupiga kura kwani hawakupewa shahada za utumishi ambazo zingewawezesha kupiga kura katika sehemu walizokwenda kusimamia zoezi hilo.
Alidai pia kuwa kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea kutangaza matokeo ya majimbo mengine ambayo yalikuwa yanaonyesha wagombea wa CCM kushinda, kuliwakatisha tamaa wananchi, hatua ambayo pia ilichangia kuvuruga uchaguzi huo wa marudio.
Akihojiwa na Wakili William Erio, ambaye alikuwa anamtetea Mbunge Ally Kihiyo, aliulizwa kama anadhani kutangazwa kwa matokeo ya majimbo mengine kuliathiri chochote. Katika majibu yake, alisema matangazo ya matokeo katika majimbo mengine yaliwakatisha tamaa wapiga kura.
Erio: Kwa mfano kutangazwa kwa matokeo ya ubunge jimbo la Ileje kuliathiri nini?
Odhiambo: Watu walikata tamaa, kwani walifahamu hata wakimchagua hawataweza tena kuunda serikali.
Wakili huyo wa Kihiyo alisema Mkoa wa Dar es Salaam kwenye jimbo moja, tena wa chama alichotoka shahidi (NCCR Mageuzi) walipata ushindi (jimbo la Ubungo ambalo Masumbuko Lamwai alishinda), hivyo kwa nini athari zitokee Temeke peke yake? Unadhani kwa nini athari hizi zisiwe sehemu nyingine?
Odhiambo: Mazingira ya kisiasa hayako ‘constant’ (hayalingani kila mahali).
Erio: Sasa mimi nakwambia wewe na mgombea wenu mlishindwa kwa sababu chama chenu na mgombea wenu hamkujijenga kisawasawa.
Odhiambo: Unavyojua wewe.
Wakili Erio pia alimuuliza madai yaliyojitokeza mahakamani siku chache zilizopita kuwa mbunge wa jimbo hilo aligawa maji katika mkutano wa kampeni uliofanyika Keko Toroli na kuhoji yaligawiwaje.
Erio: Hayo maji yaliletwa kwa ndoo au kwa pipa?
Odhiambo: Yaliletwa na gari la (kubeba) maji lililokuwa kwenye msafara wake.
Erio: Hilo gari ni namba ngapi na ni mali ya nani?
Odhiambo: Sikumbuki.
Shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Nicolai Nyamangona, alisema pamoja na Tume ya Uchaguzi kutoruhusu kufanyika kwa kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo wa marudio, CCM iliendelea kufanya kampeni nyumba hadi nyumba ambapo alimtaja mtu aitwaye Issa Peter aliyedaiwa kuwa aliendelea kuwashawishi wananchi wa eneo la Mtoni Sabasaba wakichague chama hicho.
Shahidi alisema hatua hiyo ya wajumbe kufanya kampeni za nyumba hadi nyumba ilikuja kutokana na kikao kilichoitishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Tadeus Kasapila, kilichofanyika kwenye Hoteli ya Starlight jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Kamanda wa Vijana wa CCM, Rashidi Kawawa.
Nyamangona ambaye alikuwa ni wakala wakati wa uchaguzi huo alisema pamoja na kwamba kulikuwa na matatizo kwenye vituo vya kupigia kura, walipotaka kuyaeleza matatizo hayo waliambiwa wasubiri watayaandika mwisho wa zoezi la kupiga kura, hatua ambayo baadaye walielezwa kuwa hakuna fomu za kuandikia.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi siku iliyofuata Aprili 2 baada ya wakili wa Serikali, Julius Malaba, kueleza kuwa anasumbuliwa na homa ya malaria. Hata hivyo aliiambia mahakama hiyo kuwa wakili mwingine wa Serikali katika kesi hiyo, Bibi Verdiana Macha, naye hakuweza kufika mahakamani kutokana na kupewa kazi nyingine.
Kutokana na sababu hizo mbili, Wakili Malaba aliiomba mahakama hiyo iahirishe usikilizwaji wa kesi hiyo kwa sababu asingeweza kuendelea kuwapo kwenye mazingira hayo.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa anajisikia malaria baada ya mapumziko kwa ajili ya chakula cha mchana. Lakini kabla ya hapo, wakati wa asubuhi kesi hiyo iliendelea kama kawaida wakati shahidi Odhiambo akitoa ushahidi wake.
Pamoja na hoja hizo kukubaliwa na Jaji Dan Mapigano, pia mawakili wengine wa pande zote walikubali na hivyo kesi hiyo kuahirishwa.