Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KESI YA KIHIYO UCHAGUZI MKUU 1995: Kesi 128 zafunguliwa, imo ya kupinga ubunge wa Kihiyo Temeke-1

89233 Kihiyo+pic KESI YA KIHIYO UCHAGUZI MKUU 1995: Kesi 128 zafunguliwa, imo ya kupinga ubunge wa Kihiyo Temeke-1

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kesi ya kupinga ushindi wa mbunge wa Jimbo la Temeke katika uchaguzi wa Novemba 1995 ilifunguliwa na waliokuwa wagombea wa NCCR-Mageuzi, Richard Tambwe Hiza na wa Chadema, Beatrice Mtui na watu wengine wanne ambao ni wananchi wa kawaida.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Machi 25 na Kihiyo akajiuzulu Mei 28, 1995 kwa madai kuwa alikuwa na matatizo ya kiafya.

Kujiuzulu kwa Kihiyo kulikuja siku mbili kabla ya siku ambayo msajili wa Chuo cha Ufundi Dar es Salaam (DTC) ambacho sasa kinaitwa DIT, Clement Kato kufika mahakamani kutoa ushahidi ambao ulionyesha kuwa Kihiyo hakuwahi kusoma katika chuo hicho.

Kato, ambaye alikuwa shahidi wa 30 wa upande wa utetezi katika kesi hiyo alipofika mahakamani aliieleza mahakama hiyo mbele ya Jaji Dan Mapigano kwamba katika orodha ya wanafunzi waliotakiwa kufanya mitihani ya kumaliza kozi ya ufundi katika chuo hicho mwaka 1986, mwaka ambao Kihiyo alidai ndio alimaliza, jina la Kihiyo halikuwamo.

Alisema hata kwenye orodha ya kutoa vyeti waliyopokea Baraza la Mitihani la Taifa (BMT), jina la Kihiyo halikuwamo na kwamba alikuwa pia na orodha ya wanafunzi waliomaliza kozi ya FTC (Full Technician Course) mwaka 1986 katika chuo hicho na pia orodha ya majina ya wanafunzi waliofaulu na walioshindwa kama walivyoyapokea kutoka BMT, lakini pia hakukuwa na jina la Ally Ramadhani Kihiyo.

Katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika Oktoba 1995 Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipata upinzani mkali kutoka NCCR-Mageuzi kilichompokea Augustine Lyatonga Mrema kutoka CCM na kumpa uenyekiti na baadaye kumpa fursa ya kugombea urais.

Mrema, alikuwa waziri wa Mambo ya Ndani na naibu waziri mkuu katika Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Akiwa amebadilishwa kuwa waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Mrema alisimama bungeni Jumatano ya Februari 22, 1995 na kutangaza kwamba hakubaliani na msimamo wa Serikali kuhusu sakata la Chavda.

Kashfa hiyo iliwahusu ndugu na wafanyabiashara waliojulikana sana V.G. Chavda na P.G. Chavda ambao walipata mkopo wa dola 3.5 milioni kutoka kwenye Debt Conversion Program (DCP) mwaka 1993.

Jumatatu ya Februari 27, ikiwa ni siku tano baadaye, Rais Ali Hassani Mwinyi alitangaza kumfukuza Mrema katika Baraza la Mawaziri kutokana na kukosa uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility).

Ijumaa ya wiki hiyo, Machi 3, Mrema alitangaza kuondoka CCM. Baadaye alitangaza kujiunga na chama cha NCCR-Mageuzi na kugombea kiti cha urais.

Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 1995, mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa, ambaye alipigiwa debe na Mwalimu Julius Nyerere alipata kura 4,026,422 (sawa na asilimia 61.82), wakati Mrema alipata kura 1,808,616 (asilimia 27.77) ya wapiga kura 6,846,681 waliojiandikisha.

Mingoni mwa wabunge walioshinda katika uchaguzi huo ni Kihiyo aliyeshinda ubunge Jimbo la Temeke ingawa alijiuzulu Mei 28, 1996 na hivyo kufanyika uchaguzi mdogo ambao Mrema aligombea na kushinda.

Wakati Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1995 ukiendelea, shughuli ya kupiga kura kwa majimbo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam ilisimamishwa. Uchaguzi wa marudio ukafanyika Novemba 19 mwaka huo.

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na Novemba 1995, jumla ya kesi 128 zilizohusu Uchaguzi Mkuu huo zilifunguliwa Mahakama Kuu.

Wafungua mashitaka walikuwa wanapinga matokeo ya majimbo hayo kwa madai ya haki kukiukwa wakati wa uchaguzi.

Mgawanyiko wa kesi hizo kikanda (idadi ikiwa katika mabano) ulikuwa kama ifuatavyo: Arusha (13), Dar es Salaam (21), Tabora (21), Ruvuma (9), Mtwara (1), Mwanza (14), Kilimanjaro (5), Mbeya (16), Kagera (10) na Dodoma (9).

Hata hivyo, Mahakama Kuu, Jumanne ya Februari 26, 1996 ilifuta kesi nane zilizohusu kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1995 baada ya wafungua mashtaka kuwasilisha maombi ya kuondoa kesi hizo.

Kwa upande mwingine, Machi 25 kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni ilifutwa baada ya wakili wa upande wa mashtaka, Dk Masumbuko Lamwai, kutoonekana mahakamani.

Richard Masanja na wenzake waliofungua kesi hiyo nao hawakufika mahakamani. Jaji aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo, Agusta Bubeshi akaifuta kesi hiyo. Waliokuwa walalamikiwa katika kesi hiyo ni Peter Kabisa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ingawa kesi nyingi zilifutwa, kesi iliyofunguliwa kupinga ushindi wa Kihiyo, haikufutwa. Hiyo ilikuwa miongoni mwa kesi 128 za uchaguzi zilizowasilishwa Mahakama Kuu.

Ilipoanza kusikilizwa, Machi 27 shahidi wa kwanza wa upande wa walalamikaji alikuwa Richard Tambwe Hiza.

Katika ushahidi wake alisema kauli zilizotolewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ditopile Mzuzuri na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwindadi Ally, zilichangia kuvuruga uchaguzi huo wa marudio.

Hiza alisema siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu, Mkuu wa Mkoa alitoa tangazo kwenye vyombo vya habari kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanataka kuvuruga uchaguzi wa marudio uliofanyika Novemba 19, 1995.

Shahidi huyo alimkariri Ditopile akisema kuwa kufuatia njama hizo, Serikali iko makini na wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu usalama wao.

Katika ushahidi wake, Hiza pia alisema Kamanda Ally alisema Jeshi la Polisi limejiandaa vizuri na kwamba kila mpiga kura atakuwa analindwa na askari saba, kauli ambazo, aliiambia mahakama, kuwa zilikuwa ni za vitisho.

Hiza alisema siku ya uchaguzi aliona askari wengi wametanda sehemu mbalimbali, jambo ambalo kwake halikuwa la kawaida na liliwatisha wapiga kura.

Jaji aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo, Dan Mapigano alimuuliza shahidi anaichukulia vipi taarifa ya mkuu wa mkoa na ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa.

Jaji: Unadhani taarifa hiyo ilikuwa ya uongo?

Shahidi: Ndiyo. Kwa sababu hapakuwa na mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na taarifa hizo.

Shahidi huyo ambaye pia alikuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia NCCR-Mageuzi alisema hakuona sababu zozote za kufutwa uchaguzi wa Oktoba 29 kwa sababu hakukuwa na mgombea hata mmoja aliyekwenda kuulalamikia uchaguzi huo.

Shahidi wa pili alikuwa Beatrice Mtui ambaye alidai kuwa pamoja na kwamba jina la chama chake lilikosewa, badala ya Chadema likaandikwa Chadea kwenye karatasi za kupigia kura, pia alisema polisi waliwatishia wapiga kura siku ya uchaguzi wa marudio.

Shahidi huyo alisema kuwa baada ya kupiga kura siku hiyo aliondoka, lakini alikutana na makundi mengi ya askari wa kutuliza ghasia (FFU).

Akimhoji shahidi huyo, Mwanasheria wa Serikali, Julius Malaba aliuliza:

Malaba: Wewe umesema unawaogopa polisi?

Beatrice: Ndiyo. Nawaogopa kwa sababu sipendi kuhusishwa na polisi.

Malaba: Kutopenda kuhusishwa na polisi ulianza lini. Ni wakati wa uchaguzi au ni toka awali?

Beatrice: Siwapendi kutokana na vitendo vyao tangu walipowakamata na kuwatesa watoto wa Kibasila.

Katika kesi hiyo, upande wa walalamikaji ulikuwa unatetewa na mawakili Julius Ndyanabo, Balozi Frederick Rutakyamirwa na Dk Masumbuko Lamwai. Kesi hiyo iliahirishwa.

Columnist: mwananchi.co.tz